Ruge Afunguka Kwanini Baadhi ya Wasanii Wanamchukia...Adai Lady Jay Dee Waliniumiza Kichwa Sana

Ruge Mutahaba anaweza kuwa ametajwa kwenye masakata mengi ya ubaya dhidi ya wasanii, akibebeshwa lawama kuliko mtu mwingine yeyote kwenye tasnia ya muziki, lakini kwake ni mambo matatu tu ndiyo anaona yamemsumbua sana.

Mtaje Mr ll, mtaje Lady Jay Dee na mtaje Q Chief, utakuwa umemkumbusha mbali mkurugenzi huyo wa vipindi wa Clouds Media, ambaye pia amefanya kazi ya kusimamia wasanii wengi na ndiye kiongozi wa chuo cha Tanzania House of Talents (THT).

Katika makala haya, Ruge anazungumzia mambo mbalimbali kwenye sanaa na kutaja migogoro mitatu ambayo hataisahau tangu aanze kujihusisha na shughuli za burudani.

Endelea…

Swali: Baadhi ya wasanii ambao waliwahi kufanya kazi na wewe wamekuwa akilalamika mara baada ya kutoka katika uongozi wako, kwamba uliwanyonya, walidhulumiwa na mengine mengi kuna ukweli kuhusu haya?

Ruge: Sidhani kama kuna mtu ambaye anaweza kusema jambo hivihivi. Mfano THT haina tofauti na chuo kingine.

Inatakiwa uhitimu na uende. Ukiamua kuendelea kufanya mambo yako pale hukatazwi na wala hakuna anayekufukuza, lakini lazima uondoke na wengine wapate nafasi.

Sasa ukiona mtu ameondoka na kisha anashuka kimuziki ni yeye mwenyewe ameshindwa kujisimamia.Nimefanya kazi na wengine wengi kama kina Patricia Hilary ambao walifanikiwa kujenga nyumba zao. Iweje starehe zako unilalamikie mimi?

Swali: Unadhani ni kwanini wanakutusi?

Ruge: Nilichokigundua ni kwamba hawa wasanii wanaopita kulalamika huko pembeni wanashindwa kujisimamia kutokana na mambo wanayoyafanya. Wengi wao ni kama watoto wanatafuta pa kulilia hawapapati, wanatafuta mtu wa kuongea naye lakini hawana.

Mwingine alisema anapata Sh40 milioni kwa mwezi aliviambia vyombo vya habari kwamba kila wiki anatengeneza Sh10 milioni, wewe mtu wa kupata hizo kwa mwezi ni wa kunilalamikia mimi?

Sasa kama alipata milioni 40 kwa mwezi, kwa mwaka mzima hukuwekeza usinilaumu. Jilaumu kwa sababu kwa mwaka ni Sh480 milioni, mimi mwenyewe siwezi kupata faida hiyo kwenye biashara zangu.

Ninavyoona waandishi wengi hawafanyi tathmini kuhusu hawa watu wanaolalamika, kuna watu wakubwa ambao nilishawahi kufanya nao kazi, leo hii nikiwaitia kazi wanakataa nisiwalipe fedha. Kuna kina Issa Matona, Bi Shakira, Mwanahela, Patricia Hilarry mnawaangalia hawa au hao wengine?

Juma Nature amemtukana Fella mara ngapi? Kina Keisha, MB Dogg wamemtukana Tale mara ngapi? Mb Dogg alikuja na malapa hapa na wimbo wake wa “Latifa”, Tale akaniambia tumsimamie huyu kijana.

Swali: Ni kweli kwamba wasanii wakiondoka katika usimamizi wanabaniwa katika vituo vyenu vya redio na sehemu nyingine?

Ruge: Ninarudi palepale hawawezi kujisimamia. Wengine wanachosahau ni kwamba walikosea hawakupata baraka.

Mwishowe wanarudi na kusema kwamba walionewa, wanabaniwa kwa sababu ya mtu fulani, si sahihi. Mimi mwenyewe napoona mtu anamtukana mwingine, naangalia mpaka nakasirika.

Hii kitu ipo kila mahali sema ni habari zaidi ikitokea kwenye muziki wa bongo fleva. Kwanini Clouds? Mbona Mengi aliwapiga stop Ali Kiba na Ray C kwa sababu hakwenda kwenye hafla ya walemavu, mbona haikuwa dili? Magic FM walimpiga stop Diamond kwa miaka miwili?

Kwanini sisi tukiamua kwamba hatupigi wimbo wa msanii fulani inakuwa ni ishu kubwa na ndiyo habari ya mjini? Kama ni sera ya ndani ya Clouds, kwa nini Ruge Mutahaba anakuwa wa kwanza kulaumiwa?

Swali: Ni bifu ngapi tano za wasanii ambazo zilikusumbua zaidi?

Ruge: Mimi nimekuwa nikichukulia kama kunisumbua kwa sababu sijawahi kuwa na bifu na msanii, lakini wao wanakuwa nazo kwangu. Nawashangaa watu wenye mabifu. Mfano kwangu bifu lililonishangaza au kunisumbua ni lile la ANTI VIRUS.

Si kwa sababu ya Sugu, bali wale waliomfuata. Kwa sababu kuna watu ambao waliingia kiasi kwamba nikawa nashangaa hata walitokea wapi. Kwa sababu nusu yao sikuwa nawajua ni kina nani.

Nilishangaa ni kina nani ambao wanaweza kuingia kwenye ugomvi na mtu wasiyemjua? Wapo katika maisha gani ya kuambiwa tu ‘gombana na mtu fulani’, na wewe ukagombana na tena unatukana? Kilichokuwa kinanitatiza ni chanzo ambacho (hao watu) hawakukijua na wala hawakutaka kukijua.

Na kwa sababu nilikuwa najua tatizo la Sugu, haikunisumbua. Tatizo ni hao wengine ambao sikujua wametoka wapi.

Kwangu mimi sikuwa na ugomvi na mtu. Bifu ni kitu ambacho kipo pande zote mbili. Kama kwako hauna bifu kunakuwa hakuna, labda kama upande wa pili umeamua kuwe na bifu.

Ugomvi wa pili ni dhidi ya Lady Jaydee. Ilikuwa ya ajabu sana kwa sababu maneno mengi yalianzia mitandaoni hadi tukaamua kufungua kesi, ambayo hadi leo haijaisha mahakamania. Kinachotakiwa sasa ni yeye kuomba radhi, lakini mahakamani hatokei.

Haya mambo ni bahati mbaya yalishatokea, kwa hiyo mtu yeyote akitaka kusema jambo lolote lenye malalamiko lazima amtaje Ruge ili kitu chake kijulikane zaidi.

Pia Q Chief aliwahi kunitukana sana kipindi cha msiba wa Mangwea, nikamfuata na kumwambia unanitukana, nitukane basi mpaka hamu yako iishe nikiwa hapa hapa. Niliwahi kuambiwa kwamba nimezuia kibali cha (mwimbaji kutoka Nigeria) Davido Basata, siyo kweli. Kwa bahati mbaya najua vitu vingi.

Mtu anaweza kufanya jambo akakataliwa Basata mimi nikaenda nikafanikiwa akadhani kwamba nimembania, kumbe hajui sheria na mipaka ya Basata ni ipi. na kwingine ni kupi.

Sisi tulitaka kunyimwa kibali, tukawaambia Basata kwamba wakitunyima tunakwenda mbele kwa waziri ndiyo utaratibu. Sasa mwingine akinyimwa anadhani tumewabania.

Tags

Post a Comment

3 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Maelezo ya uongo utayajua tu, laana hiyo!

    ReplyDelete
  2. Ruge anatudanganya tu hapo. Ww kaa na hao unaowanyonya.

    ReplyDelete
  3. Uzuri wa nchi yetu ni kwamba ina uhuru wa kujieleza,na mtu anajieleza acha ajieleze msimkatalie mwenye ukweli ni yeye na huyo lady jd.

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad