Sakata la Walimu wa Kike Kuingiliwa Sehemu zao Za Siri Kishirikina Lachukua Sura Mpya

SAKATA la walimu wa Shule ya Msingi Nambaza iliyopo Jimbo la Mwibara, Wilaya ya Bunda, mkoani Mara, kufanyiwa vitendo vya kishirikina wakidai kuingiliwa kimwili, kuibiwa mali na fedha, sasa limechukua sura mpya.

Hali hiyo inatokana na Mkuu wa Wilaya hiyo, Joshua Mirumbe kuagiza watuhumiwa (wachawi), ambao wananchi waliwabaini kuhusika na vitendo hivyo kwa kupigiwa kura, wakamatwe haraka na kufikishwa katika vyombo vya dola.

Mirumbe alitoa agizo hilo jana ofisini kwake katika kikao ambacho kilimshirikisha Mbunge wa jimbo hilo, Kangi Lugola, viongozi wa Serikali ya Kijiji cha Nambaza na Kata ya Nansimo.

Alisema vitendo vya kishirikina wanavyofanyiwa walimu hao ni udhalilishaji mkubwa ambao hauwezi kuvumiliwa na kumlalamikia Ofisa Tarafa ya Nansimo, Bw. Jonas Nyeoja kwa kuzembea na kutochukua hatua za haraka.

Alisema Bw. Nyeoja alipaswa kuwakamata watuhumiwa 15 ambao wanalalamikiwa kuwatesa walimu kwa kuwafanyia vitendo vya kishirikina na kuwafikisha katika vyombo vya dola.

"Nimemuagiza Ofisa Tarafa (Nyeoja), akawakamate watuhumiwa ambao orodha ya majina yao ninayo na wafikishwe kwenye vyombo vya dola wakati tukiandaa maeneo ya kuwahamisha kwani wamekosa sifa za kuishi kijijini hapo na wenzao hawawataki," alisema.

Aliongeza kuwa, kuendelea kuwakumbatia watu hao ni kusababisha machafuko kijijini kwani upo uwezekano wa wananchi kuchukua sheria mkononi na kuwaweka walimu katika hofu, kukosa molari wa kazi.

Kwa upande wake, Bw. Lugola ambaye alilazimika kusitisha vikao vya bunge na kwenda jimboni kwake kushughulikia tatizo hilo, akiwa katika mkutano wa hadhara alioufanya kijijini hapo, alitokwa na machozi baada ya kuelezwa jinsi walimu hao walivyofanyiwa vitendo vya kinyama kwa kuwadhalilisha na kuwaondolea utu wao.

Katika mkutano huo, wananchi mbali na kuwataja wahusika wa vitendo hivyo hadharani, walimtaka Bw. Lugola ahakikishe watu hao wanahama haraka jimboni humo kabla hawajachukua sheria mkononi hatua ambayo itakuwa na madhara, umwagaji damu.

Bw. Lugola aliwaeleza wananchi hao kuwa yuko pamoja nao ili kuhakikisha watu hao wanahama jimboni kwake, lakini kwa kuwa hana mamlaka ya kufanya hivyo kesheria, atalifikisha suala hilo kwa Mkuu wa Wilaya mwenye uwezo wa kufanya hivyo kisheria.

Katika mkutano huo, pia alikuwepo Diwani wa Kata ya Nansimo, Sabato Mafwimbo, Ofisa Tarafa (Nyeoja), Ofisa Mtendaji Kata ya Nansimo, Bryceson Mashauri, Mratibu Elimu Kata, Pius Kijoriga na Mwenyekiti wa Kijiji cha Nambaza, Leonard Mtelalilwa.

Jana Bw. Lugola aliongozana na viongozi hao pamoja na polisi kwenda kijijini Nambaza kuwakamata watuhumiwa hao kutokana na agizo la Mkuu wa Wilaya na kusema kama polisi watasita kuwakamata watuhumiwa kwa lengo la kuwalinda, yeye atamkamata hadi mtu wa mwisho.

Watu hao wanadaiwa kuwaingilia kimwili na kuwafanyia walimu vitendo hivyo usiku wakiwa wamelala pamoja na kuchukua nyaraka zao mbalimbali zikiwemo vitambulisho na kadi za benki (ATM) kwa njia za kishirikina.

Pia wachawi hao wamekuwa wakijisaidia haja kubwa na ndogo katika vitanda vya walimu hao, kuweka vyakula, unga na mboga na wakati mwingine walimu hujikuta wamelazwa chini wakiwa utupu na chakula hubadilishwa kishirikina ambapo kama walikuwa wakila wali na nyama ya kuku, ghafla unakuwa ugali na maharage.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad