VIONGOZI mbalimbali wa dini nchini wameandaa maandamano kwa lengo la kumuona Rais jakaya kikwete ili kumuomba alifanyie mabadiliko makubwa Jeshi Polisi.
Mabadiliko hayo ni pamoja na kubadili mawaziri wote wa mambo ya ndani, mkuu wa jeshi hilo (IGP) na MA-CP wawili ambao wametajwa kuendesha jeshi hilo kimtandao kinyume na taratibu za kijeshi.
Maandamano hayo yamefikiwa na Maaskofu na Mashekhe 160 wa mjini Dodoma jana chini ya Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili, amani na haki za binadamu ya Madhehebu ya Dini Nchini Askofu William Mwamalanga.
Mwamalanga alisema viongozi hao wamepokea taarifa ya kuuwa kwa askari polisi wanne wa kituo cha stakishari cha jijini Dar es Salaam kwa masitikito.
“Tumepokea taarifa ya vifo vya askari hawa kwa masikitiko, hali hii haikubaliki kila mara vituo vimekuwa vikivamiwa na hadi sasa takriban Askari 47 wameuwawa,” alisema Mwamalanga.
Huku akibubujikwa na machozi ya Uchungu Askofu Mwamalanga amehoji ukimya wa Waziri wa Mambo ya Ndani Mathias Chikawe na IGP Erinest Mangu kwa vifo vyote ambavyo vimekuwa vikitokea tangu mwaka huu uanze.
“Uvamizi huu na mauaji ya askari wa chini unatisha na hatuoni hatua yoyote ya maana iweje wahalifu wawe na nguvu kuliko jeshi hasa kipindi hiki ambacho dunia inakabiliana na makundi ya wahalifu hatari wakiwemo al shabab,” alihoji.
Kufuatia hali hiyo, ASkofu Mwamalanga amemuomba Rais kikwete kuwaongeza askari wangazi ya chini mishahara kwa kiwango cha Millioni moja ili walingane na wenzao wa nchi za afrika mashariki na kusini.
Alisema hatua hiyo itawawezesha askari hao kukabiliana na changamoto za maisha kama ilivyofanya kwa wafanyakazi Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) ambapo ilisema hiyo itawaondolea tamaa za Rushwa.
“Kwa Polisi ni zaidi kwani kitendo cha kuuwawa kama tembo porini bila mshahara mzuri kunawakatisha tamaa na ari ya kufanya kazi,” alisema.
Askofu Mwamalanga ambaye ni Mwanaharakati Mtafiti wa haki za jamii alisema idadi kubwa ya Maaskofu na Maashekhe nchini wamelaani Mauaji hayo yanayoendelea dhidi ya polisi.
“Tayari zaidi ya askari 47 wameuwawa na wengine wamebaki vilema, silaha lukuki zimechukuliwa vituoni na kutokomea kusikojulikana, hili lina dhihirisha kuwa Taifa letu lipo pabaya. Ndiyo maana tunaona ipo haja tena muhimu kwa rais kwachukilia hatua za haraka wanaosababisha uzembe huo ikiwa ni pamoja na kulifanyia ukarabati jeshi hili,” alisema.
Aliwakumbusha watanzania kuliona jeshi hilo kuwa ni chombo chao cha kuwalinda wao wawe salama dhidi magenge ya uhalifu duniani hivyo wana wajibu kama raia wema kuhakikisha wanawalinda askari hao kwa hali na mali ikiwa ni pamoja na kuwapa taarifa muhimu ili kuwakamata wauaji wote pamoja na silaha zote zilizoporwa.
Aidha viongozi hao walihoji kuondolewa kwa vizuizi [ berial] barabarani kulikuwa na maslahi gani kwa usalama wa nchi kwani hivi sasa wahalifu wametumia nafasi kutoroka kirahisi pale wanakuwa wamefanya uhalifu.
“Tunataka vizuizi hivyo virudishwe mara moja kwa barabara zote nchini,” alisema.
Kwa upande wake shekhe Athumani Mukambaku ambaye ni Mwenyekiti mwenza wa Kamati hiyo na mjumbe wa BAKWATA halmashauri ya mkoa wa dar es Salaam alishauri serikali itunge sera mahususi ya raia wote kuwalinda polisi baadala ya dhana iliyojengeka kuwa ni polisi pekee ndiyo wenye wajibu wa kulinda raia, jambo linalojenga chuki pale ambapo polisi wanaposhindwa kusimamia haki za raia sawasawa.
“Katika kipindi hiki cha kulelekea uchaguzi mkuu jeshi linapaswa kuimarisha vituo vyake vyote ikiwa ni pamoja na kufunga kamera maalumu za cctv ili kuweka rekodi ya watu wote wanaotembelea vituo hivyo pamoja kuvunja kanda maalumu za kipolisi ambazo hazionesha juhudi ya kupambana na uhalifu na baadala yake zimeongeza gharama kwa jeshi hilo,” alisema Shekhe Mukambaku.
Alisema rais anapaswa ateue makamanda wabunifu wanaokwenda na wakati na kwamba kila mkoa uwe maalumu kwa kuimarisha vitendea kazi vya askari ikiwa ni pamoja kuwapatia motisha wale walio ngazi ya chini ambao hukesha vituo kuimarisha ulinzi.
Tukio la Kituo cha Polisi Kutekwa: Viongozi Wa Dini Wacharuka.......Wamtaka Rais Kikwete Afanye Mabadiliko ya Jeshi la Polisi
0
July 14, 2015
Tags