Askari Magereza Aliyepanga Mauaji Stakishari Auawa

MAPYA tena! Aliyekuwa askari magereza wa Gereza la Dondwe, Wilaya ya Mkuranga, Pwani, Juma Rashid ambaye Uwazi liliwahi kumripoti kuwa, ndiye ayechora ramani yote ya uvamizi na mauaji ya askari wa Kituo cha Polisi  Stakishari, Dar imebainika kwamba ameuawa, Uwazi linazidi kukokotoa.
Uchunguzi wa kina uliofanywa na gazeti hili umebaini kwamba askari huyo ndiye yule aliyeuawa siku ya tukio lililojiri Julai 12, mwaka huu nje ya kituo cha Stakishari ambaye alijulikana kwa jina maarufu la Osama.

HAIKUJULIKANA
Hata hivyo, baada ya muaji hayo, taarifa zilienea kwamba, aliyeuawa eneo la tukio ni mmoja wa majambazi hao bila kujulikana kuwa ndiye askari magereza mstaafu mpaka hivi karibuni ambapo, mke wake, Fatuma Hassan (37) alipoanika ukweli kwa gazeti hili.

Uchunguzi zaidi umebaini kuwa, siku chache kabla ya tukio la uvamizi huo, marehemu Osama alionekana kwenye baa moja iliyopo maeneo ya Stakishari na kuwanunulia pombe baadhi ya polisi huku akichunguza sehemu zinazohifadhiwa silaha na jinsi gani polisi wanavyokaa katika lindo pia ni siku gani inafaa kwa uvamizi ambapo alibaini ni Jumapili.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, timu ya Uwazi ilifunga safari hadi kwenye Kijiji cha Dondwe na kufikia nyumbani kwa marehemu Osama ambaye aliacha kazi akiwa na cheo cha koplo na kufanya mahojiano na mke wake, Fatuma.

Mwanamke huyo ambaye alianza kwa kukiri kwamba marehemu Osama alikuwa mumewe, alisimulia maisha yake na mwanaume huyo hadi anauawa. Alikuwa na haya:
“Tulifunga ndoa na Juma mwaka 1999 huko Kigoma alikokuwa akifanyia kazi katika Gereza la Kwitanga. Tulipendana sana. Mume wangu alikuwa mpole, msikivu, sikutegemea kama angeweza kuuawa katika mazingira kama haya ya aibu.
“Mwaka 2009, akatakiwa kuja kuripoti Gereza la Ukonga (Dar) halafu akapangiwa kuja hapa Gereza la  Dondwe (ni tawi la Gereza la Ukonga).”

AANZA KUBADILIKA TABIA
“Akiwa hapa Dondwe, ghafla mume wangu alianza kubadilika tabia, akawa anafuga ndevu tofauti na taratibu za kazini kwake. Akaonywa na viongozi wake lakini hakubadilika.
“Lakini pia alinitaka mimi nianze kuvaa nguo za kufunika mwili  mzima mpaka mikono na kubaki uso tu. Hilo sikukubaliana nalo.

“Tuliendelea kuishi mpaka mwaka 2012, akasema anataka kuacha kazi. Mimi sikukubaliana naye kwa sababu tuna watoto, yeye akasema lazima aache kazi. Nilimuuliza anataka kufanya kazi gani na kwa nini aliamua kuacha kazi? Akasema aliamua hivyo kwa sababu imani ya dini yake haikuwa ikimruhusu kufanya kazi ya uaskari ambayo aliitafsiri kuwa ni ya ukafiri.
“Kweli. Siku ilifika, akaandika barua ya kuacha kazi, lakini pia akaniandikia mimi talaka moja kwa sababu sikumuunga mkono kwenye matakwa yake.”
“Maisha yalianza kuwa magumu. Akawa anauza maji mitaani kwa kubeba madumu kwenye baiskeli. Baadaye akanunua pikipiki ya magurudumu matatu, akaendelea na biashara hiyo.”

MKE ARUDI KWAO
“Ilinibidi mimi niondoke kurudi kwetu Singida. Baadaye nilikwenda kwao kuwaeleza ndugu zake akiwemo baba yake mzazi. Walishangaa sana, aliitwa lakini hakwenda. Wakanishauri nirudi hapa Dondwe ili niwatunze watoto. Majirani zangu hapa nao walinipigia simu wakisema nirudi, watoto wanateseka.
“Nilirudi, lakini nilipofika ikawa kila mmoja analala katika chumba chake. Hakunijali kwa chakula wala kwa mavazi.
“Kitu kilichonishangaza ni kwamba, aliniambia kuwa anataka kuwatoa watoto kwenye shule za serikali na kuwapeleka za dini. Nilikwenda kwa mtendaji wa kijiji nikamweleza. Aliitwa ofisini lakini hakwenda. Kuanzia hapo akaacha kuwahudumia.”
MAAJABU ZAIDI

“Mimi nilianza kuamini mume wangu hakuwa yule baada ya watu aliokuwa akiswali nao, walipokuwa wakija hapa nyumbani aliwaambia mimi si mke wake. Isitoshe hata baba yake mzazi alipofariki dunia Aprili mwaka huu hakwenda.”

STAKISHARI
“Nakumbuka siku hiyo ya tukio la kule Stakishari, aliondoka hapa jioni akisema anasafiri kwenda kwao Singida. Nilimuuliza mbona unaondoka na pikipiki, utaitunza wapi? Akasema ataiacha kwa ndugu zake wa Dar.
“Hata hivyo, nilipata wasiwasi. Lakini sikuwa na la kusema. Aliondoka zake. Ilipofika usiku nilimpigia simu ikawa haipatikani. Kwa kweli sikupata usingizi. Kesho yake nikapiga tena simu pia hakupatikana.
“Niliamua kuwapigia simu kwao, wakasema hawana taarifa ya ujio wake. Jioni nikampigia dada yake ambaye yupo Singida mjini, akasema hawajamuona.

MAMBO HADHARANI
“Nilikuwa najiuliza maswali mengi sana lakini bila majibu. Baada ya siku kama tatu kupita, ikatangazwa na jeshi la polisi kwamba kuna jambazi mwenye madevu ameuawa na picha yake ikawa mtandaoni. Mtendaji wa kijiji chetu, Said Mohamed Mfume naye akawa amepata taarifa hizo akaniita ofisini kwake.
“Mtendaji akaniambia kwamba kuna picha ya mtu aliyeuawa katika tukio la Stakishari anafanana na mume wangu lakini hakunionesha. Picha hiyo ilisambaa hadi kwao Singida.
“Kuna ndugu yangu akaja mpaka hapa Dondwe akanionesha hiyo picha, nikagundua ni yeye mume wangu. Katika magazeti waliandika jina la Ustadhi Rashid.
“Marafiki zake nao baada ya kupata taarifa walikuja hapa na kuniambia eti mume wangu ameuawa lakini ni kama amepata shahada. Wakimaanisha kwamba amekufa kishujaa katika kutetea dini.”

MKE AENDA STAKISHARI
“Ilitulazimu kwenda Kituo cha Polisi Stakishari ili kupata taarifa kamili. Kufika wakaniweka ndani siku tano kwa mahojiano. Hivi ninavyozungumza na wewe  simu yangu bado iko pale kituoni.
“Niliporudi hapa nyumbani, niliwaambia watoto juu ya kifo cha baba yao, kwa kweli walijisikia vibaya sana ingawa alikuwa hawataki waziwazi.”

MWILI WACHUKULIWA
“Agosti 4, mwaka huu, mimi na watu wengine hapa  tulikwenda kuuchukua mwili Muhimbili. Kufika tukapata taarifa kwamba kuna watu walikwenda jana yake kuutaka mwili lakini walizuiwa. Mimi  nilijua ni wale marafiki zake.

“Baada ya kuuchukua mwili tulishindwa mahali pa kwenda kuuzika kutokana na tukio alilolifanya. Ilibidi tukamzike kwenye Makaburi ya Kijiji cha Mazinda, Mbuyuni, Chanika ambako kuna dada yangu kaolewa huko. Mumewe alisema kumzikia Dondwe haitatoa picha nzuri kutokana na aina ya kifo.

“Agosti 8, mwaka huu, tulikwenda kujengea kaburi lake, tukakuta kifuu cha nazi kilichoandikwa maneno ya Kiarabu. Ilinishangaza sana mimi. Hivyo ndivyo ilivyokuwa au ninavyomjua marehemu Rashid Juma baba wa watoto wangu wanne.”
Baadhi ya askari magereza wa Gereza la Dondwe ambao walikuwa wakifanya kazi na marehemu walipohojiwa na Uwazi walisema wanamtambua marehemu ambapo kazini alikuwa akitumia jina la Antony Gembo.

La Juma Rashid lilikuwa la dini lakini aliamua kuacha kazi kwani alibadilika akawa tofauti na taratibu za kijeshi. Alipoambiwa ajirekebishe aliamua kuacha kazi lakini cha kushangaza hakuchunguzwa anakwenda kufanya kazi gani na kwa nini alikuwa na kiburi hicho cha kuacha kazi.
Baadhi ya wanakijiji waliohojiwa kuhusiana na maisha ya marehemu huyo walisema hakuna aliyejua angeweza kujiunga na tabia hiyo ya kihalifu na hata siku alipouawa haikujulikana mara moja kuwa ni yeye.

Vyanzo vyetu vilieleza kwamba, marehemu kabla  hajabadilika tabia alikuwa akiswali katika nyumba moja ya ibada. Baada ya muda kukatokea kundi la watu ambao ni marafiki zake kutoka kijiji jirani.
Hata hivyo, waumini wa madhehebu waliyokuwa wakiswali waliwashtukia kutokana na elimu ya dini waliyokuwa wakiitoa ambayo ilikuwa ya kihalifu zaidi, wakatimuliwa.
Inadaiwa kuwa, baada ya kutimuliwa, watu hao wakiwa na marehemu walielekea Kijiji cha Mandikongo ambapo kulikuwa na ngome yao. Na ndiko ambako baada ya uvamizi wa Stakishari, jeshi la polisi lilikuta bunduki 15 na shilingi zaidi ya milioni mia moja na sabini elfu zikiwa zimefukiwa ardhini.
Kamishna wa Polisi Kanda Maalum Dar, Suleimani Kova (pichani), aliliambia gazeti hili kwamba baadhi ya watuhumiwa wa tukio hilo wameshakamatwa.

MTENDAJI WA KIJIJI
Mtendaji wa Kijiji cha Dondwe, Mfume alipohojiwa na waandishi wetu alikiri kumtambua marehemu kwani alikuwa mkazi wake na mke wake walikuwa wakifika ofisini kuelezea mambo aliyokuwa akifanyiwa na marehemu.

Post a Comment

4 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. serikali inapaswa kulitazama hili kwa undani zaid, lazima kuna mtandao mkubwa nyuma yao, na hao rafiki zake wanakiwa wabanwe kweli kweli vinginevyo tutajikuta wametuweka kati

    ReplyDelete
  2. Asante jeshi la Polisi na poleni wanandugu mliopotelewa na ndugu zenu katika tukio la Stakishari,Mungu azirehemu riho za marehemu...Amina

    ReplyDelete
  3. Huyu alikuwa kashapewa pepo (jini) la kumfanya awe muuaji yaani mfia dini, kubadilika isingekua rahisi ila kifo kimkute kama hivyo ndio inakua salama ya raia wema waliobaki. Ukitaka kuwajua watu kama hao angalia macho yao kwa makini utagundua ni mtu hatari sana japo kwa nje anaonekana ni mpole na mnyenyekevu! ila ndani ni Lucifer mwenyewe anafanya kazi.

    ReplyDelete
  4. Mara nyingi wenye misimamo ya ajabu kwenye dini ndio huwa wanataka kuwaaminisha na wengine kwa kile wanachokiamini wenyewe, ni kweli hawa rafiki zake watakuwa wanajua kitu.....

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad