Kikwete: CCM Si Chama Cha Mchezo.......Wapinzani Watakiona cha Mtema Kuni Mwaka Huu

MWENYEKITI wa Taifa wa CCM, Rais Jakaya Kikwete amesema chama hicho sio chama cha mchezo na kuvionya vyama vya upinzani kuwa watakiona cha mtema kuni katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Amesema CCM itapata ushindi katika uchaguzi huo kwa kuwa imejipanga kwa hoja na imeleta maendeleo nchini, huku akieleza kuwa wapo watu wenye tamaa ya uongozi ambayo imekithiri.

Aliungwa mkono na Mgombea Urais wa CCM, Dk John Magufuli aliyesema chama hicho kitashinda na haoni wa kuwashinda, huku akiahidi kuwa atakuwa mtumishi wa Watanzania kwani anazijua shida zao.

Rais Kikwete aliyasema hayo jana katika Ofisi Ndogo za CCM, Mtaa wa Lumumba, Dar es Salaam ambako alikuwapo kumpokea Dk Magufuli na Mgombea Mwenza Samia Suluhu Hassan baada ya kutoka kuchukua fomu katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) katikati ya Jiji ili kuomba kuidhinishwa kuwa wagombea.

“Sasa kazi ndio imeanza rasmi. Dodoma zile zilikuwa rasharasha. CCM sio chama cha mchezo. Watakiona cha mtema kuni. Kama ni mpira wa miguu, basi tumefunga bao wakiwa wamesimama. Tumejiandaa vya kutosha na kushinda tutashinda. Uzoefu, maarifa na uwezo wa kushinda tunao,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:

 “Nawataka wanaCCM kujipanga, msimdharau yeyote hata mpinzani akiwa mdogo shughulikeni naye. Tumejipanga kwa hoja, tunazo hoja za kuzungumza. Nchi tulivu na maendeleo yanaonekana na duniani kote wanajua kuwa Tanzania inafanya vizuri. Tunao utawala bora, demokrasia na uhuru wa habari.

“Hata duniani wanajua hilo na wanaona fahari kushirikiana na Tanzania. Lakini wapo watakaokuwa na tamaa tu, duniani wapo watu wameumbwa hivyo, wengine wanayo tamaa hadi imekithiri, imevuka mipaka,” alieleza Rais Kikwete mbele ya maelfu ya viongozi, wanachama na mashabiki wa chama hicho tawala.

Rais Kikwete aliyefuatana na mkewe Mama Salma, alikatiza hotuba yake na kuliomba kundi la Tanzania One Theatre (TOT) kuimba wimbo wa “Waache waseme CCM ina wenyewe,” ambao alishiriki kucheza na mwisho wa wimbo huo, alisema: “Ni ushindi wa uhakika, hauna hatihati. CCM shangilia ushindi unakuja.”

Kabla ya kumkaribisha Dk Magufuli na Samia, Mwenyekiti huyo wa CCM alisema uzinduzi wa kampeni za urais kwa chama hicho utafanyika Agosti 22, mwaka huu na watatangaza wapi uzinduzi huo utafanyika kwani Viwanja vya Jangwani kwa sasa havina fursa hiyo kwa kujengwa miradi ya mabasi ya haraka na wafanyabiashara wadogo.

Alishuka jukwaani saa saba kamili mchana baada ya kuwatambulisha wagombea hao wawili, ambapo Samia kwa upande wake alisema haoni sababu ya CCM kushindwa kutokana na jinsi kazi ya jana ya kwenda kuchukua fomu ilivyokusanya maelfu ya wanachama, wapenzi na mashabiki wa chama hicho tawala.

Lakini, Dk Magufuli ambaye aliwasili Lumumba saa 4.47 asubuhi ili kwenda kuchukua fomu hizo, alisisitiza kauli ya Rais Kikwete kuwa CCM itashinda kwani chini ya uongozi wa rais huyo anayemaliza muda wake kikatiba, mambo mengi mazuri yamefanywa ambayo yanawafanya watembee kifua mbele.

“Kujitokeza kwenu kwa wingi leo ni ushahidi mwingine kuwa CCM itaendelea kutawala. Niwathibitishie kuwa shida za Watanzania nazijua, mategemeo ya Watanzania ninayo, na ipo misingi mizuri imewekwa chini ya Rais Kikwete.

“Nawaahidi nitakuwa mtumishi wenu sababu ninazijua shida za Watanzania. Watanzania wana tatizo la ajira, hawataki kero za ovyo kama kukimbizana na mama ntilie na bodaboda. Wanataka uchumi wao uwe mzuri, wanataka maisha mazuri zaidi. Nitayasimamia, nawahakikishia sababu kero hizo nazijua,” alisema Dk Magufuli.

“Nimekuwa mbunge kwa miaka ishirini na nimekuwa Waziri. Nimepata uzoefu kwa Rais Kikwete, Mzee Mwinyi, Mzee Mkapa, Mzee Nyerere, na viongozi wengine. Niko tayari kukipokea kijiti kwa mikono miwili. Nataka Mwenyekiti kukuhakikishia kuwa tutashinda, sioni wa kutushinda,” alisema Dk Magufuli huku akirudia maneno ya “sioni wa kutushinda” mara tatu.

Alisema atakuwa mtumishi wa Watanzania wote bila kujali dini, kabila, itikadi kwa sababu maendeleo ni ya wote, lakini akawataka wadumishe umoja na amani, na kuwaahidi kuwa hatawaangusha.

Post a Comment

6 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. CCM NDIO WATAKIONA CHA MTEMA KUNI. WEWE SI UNAJIVUNIA KUTUMIA VYOMBO VYA DOLA KUFUNGA GOLI LA MKONO? SISI TUNAKUAMBIA, UKAWA HATULALI MPAKA KIELEWEKE

    ReplyDelete
  2. Mbona umepanick jk?tatizo lenu mlikuwa hamjazoea upinzani wa kweli sasa mmeupata na bado ndo kwanza tumeanza

    ReplyDelete
  3. Dah watanzania wasipompitisha magufuli kwa kweli watajilaumu maana huyu jamaa ana dili na kila anaejaribu kuharibu au kuchelewesha maendeleo ya wananchi na historia yake iko safi na wazi kabisa mungu watie fahamu watanzania na uwabariki

    ReplyDelete
  4. CCM lazima wanyooke,mungu ni mkubwa sana mmetuibia sana nyie binadamu halafu bado mnataka kuachiana madaraka ya watoto wenu mpaka wajukuuzenu BIG NOOOOO hatukabli lazima muondoke Tanzania shida kila sehemu za huduma za jamii kila kitu kimelala kisa viongozi wasiojali.

    ReplyDelete
    Replies
    1. uzowef , maarifa ,utawala bora alicho sahau hapo rushwa tu tatizo ktk ccm hususan viongoz wa juu ktk serikali

      Delete
    2. uzowef , maarifa ,utawala bora alicho sahau hapo rushwa tu tatizo ktk ccm hususan viongoz wa juu ktk serikali

      Delete

Top Post Ad

Below Post Ad