Magufuli Apata Wakati Mgumu Kuwanadi Wabunge

Mgombea wa urais kupitia CCM, Dk John Magufuli ameanza kuonja shubiri ya kuwanadi baadhi ya wabunge wa chama hicho baada juzi, akiwa Kalambo mkoani Katavi, baadhi ya wananchi kuguna pale alipompandisha jukwaani mgombea ubunge wa jimbo hilo, Josephat Kandege.

Baada ya kuona hali hiyo, Dk Magufuli alisema: “Nawaombeni jamani, hatuchagui malaika, kila mtu ana tatizo lake. Inawezekana wengine mmechoka hata kumwangalia, lakini mkitaka mimi nifanye kazi vizuri nileteeni huyu bwana,” alisema akimnadi mgombea huyo.

Kwa nyakati tofauti tangu aanze kampeni mikoani, mgombea huyo amekuwa akiwaambia wananchi kuwa baada ya kumchagua yeye, wawachague wabunge hao na kuwasamehe makosa yao ili apate urahisi wa kuunda Serikali na kuleta maendeleo.

Alisema anatambua wakati wa mchakato wa kura za maoni, kulikuwa na wagombea wengi wa ubunge lakini wananchi wasife moyo kwa sababu kuna kazi nyingi za kufanya iwapo atachaguliwa kuwa rais.

Ili kumaliza kabisa miguno iliyokuwapo, Dk Magufuli alimwita mmoja wa waliokuwa wagombea wa ubunge ili kuwaeleza kuwa anamuunga mkono Kandege na alipopanda jukwaani na kusalimia wananchi walimshangilia kwa nguvu.

Akiwa Sumbawanga Mjini juzi, Dk Magufuli alimnadi mgombea ubunge wa jimbo hilo, Aeshi Hilaly kwa kumuita jembe huku akiwataka wananchi “wampigie tena kura hata kama amewakosea.”

“Nimesema hatuchagui malaika kila mtu ana kasoro zake. Tuache kasoro, tuangalie maendeleo. Nataka Sumbawanga muwe maalumu mkinichagulia huyu (Aeshi),” alisema Dk Magufuli wakati akihutubia katika Uwanja wa Nelson Mandela juzi.

Katika Jimbo la Kwela – Rukwa, aliwataka wananchi wamsamehe mgombea ubunge, Ignas Malocha kwa makosa aliyowatendea na kuwa atafanya kazi vizuri kwenye utawala wake.

“Msianze kugombana baadaye mkakosea kwa kumchagua mtu mwingine kwa sababu nahitaji mtu atakayeniambia shida katika wilaya yake.
 
"Hatuchagui malaika ndugu zangu, hatuchagui sura, hata mimi sura yangu ni mbaya sana na nywele zinatoka lakini Watanzania wamenichagua,” alisema Dk Magufuli akiwa katika Kijiji cha Laela.
 
“Tumsamehe, tumjaribu afanye kazi mimi nikiwa rais tuone kama hatafanya kazi vizuri.”

Kauli hiyo ya kumnadi Malocha ilijitokeza tena alipokuwa Kata ya Lusaka aliposema wampigie kura hata kama amewakosea, wamsamehe ili apate kiunganishi kwani asipopita atashindwa kufanya kazi.

“Wewe nenda tu hata kama humpendi fumba macho lakini umpigie nani?” aliuliza Dk Magufuli na kujibiwa “Malochaaa”

Baadhi ya wakazi wa Laela walimwambia mwandishi wetu kuwa wanampenda Dk Magufuli lakini Malocha hajawatekelezea ahadi nyingi alizotoa.
 
Akiwa katika Jimbo la Momba mkoani Mbeya, Dk Magufuli alimpigia kampeni kwa muda mrefu mgombea wa CCM, Dk Lucas Siame na madiwani wa eneo hilo na kuwataka wananchi wasifanye makosa safari hii, bali wachague chama tawala.

Akihitimisha ziara yake mkoani Rukwa, Dk Magufuli aliahidi kuanzisha mamlaka maalumu ya kusimamia masilahi ya polisi.

Akizungumza na wakazi wa Mji wa Laela, Dk Magufuli alisema anataka kuboresha masilahi ya askari ili waache vitendo vya rushwa na kudhibiti wimbi la majambazi na wizi... “...unamwona huyo ofisa amekonda kama mimi ni kwa sababu anafanya kazi,” alisema Dk Magufuli huku akimwonyesha mmoja ya polisi waliokuwapo mkutanoni hapo.

Alisema atawaongezea mishahara hata wafanyakazi wengine ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi na kuondoa vitendo vya kutamani rushwa na kuwaonea wanyonge.

Tofauti na siku tatu zilizopita, msafara wa mgombea huyo ulisimama mara nyingi kusalimia wananchi, hasa baada ya baadhi ya wanavijiji kufunga barabara ili awasalimie.

Hata hivyo, aliposimama katika Kijiji cha Ndalambo wilayani Momba jana, kilizuka kikundi cha vijana wasiozidi 40 na kuanza kunyoosha vidole kwa alama ya V inayotumiwa na Chadema na wakati Dk Magufuli akiendelea kumwaga sera kikundi hicho kiliendelea kupiga kelele na kupinga baadhi ya ahadi kuwa hataweza kuzitekeleza huku wengine wakisema “Lowassa, Lowassa.”

Hata hivyo, mgombea huyo hakuwajali na kuendelea kuwahutubia waliokuwa wakimsikiliza na kumshangilia hasa aliposema ataunda Serikali na kuleta maendeleo ambayo hayatabagua watu kwa itikadi za vyama, dini, makabila wala mahali watokako.

Katika eneo la Tunduma alipata mapokezi makubwa hadi akasema: “Mapokezi haya ni ya hatari, ni tsunami. Kama ni ya namna hii leo nitalala kwa raha.”

Post a Comment

2 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. NA BADO MGOMBEA EA CCM ATAENDELEA KUBEZWA KIIILA MAHALI KWA SABABU AMEGUNDULIKA ANACHOONGEA NI UONGO HADAA NA AHADI HEWA AMBAZO ILANI LUKUKI ZA CCM ZILIZOPITA HAZIKUTEKELEZWA.UONGO MBELE YA WAELEWA WA TANZANIA YA LEO.SHULE NYINGI ZA MSINGI WANAKALIA MAWE AU MAGOGO NYINGINE WANASOMA CHINI YA MITI HOSPITALI TUNAKOSA MADAWA MUHIMU KUOKOA MAISHA MAOFISINI UTORO UMEZIDI RUSHWA NJE NJE BARABARA ZOOTE VIJIJINI YANAKOTOKA MAZAO NA MATOKEO NI KUPANDA BEI YA MAZAO NA ATHARI ZAKE NI KUHARIBU UCHUMI NA KUFANYA MAISHA KUENDELEA KUWA MAGUMU NA YANAYOKATISHA TAMAA

    ReplyDelete
  2. Kuna watu respectable wenye CV zao za maana duniani…lakini walivyojihusisha na CCM wamechafua CV zao;
    Mfano;
    Getruda Mongela mwanamama aiyeongoza mkutano wa Beijing unajua kashfa za rushwa zilizokuja kumkumba
    Sospeter Muhongo-A respectable Journalist unajua Amefanya nini kwenye ESCROW
    Omar Nundu mtaalamu wa dunia wa usafiri wa anga unajua ni nini kimemtokea
    Prof Anna Tibaijuka mama aliyeongoza shirika la Umoja wa mataifa unajua nini kimemtokea
    Daudi Balali a respectable IMF and World Bank Economist unajua nini kimemtokea baada ya kujihusisha na CCM.
    Ukiachana na hao…Jakaya Kikwete wakati anaingia madarakani alikuwa mtu mchapa kazi…Katika wizara alizopita kabla ya hapo alikuwa mwadilifu na Mchapa kazi…alichaguliwa kwa 80% kumbuka….Nini kimetokea baada ya kuwa Ikulu?
    Benjamin Mkapa..Jembe la Nyerere aliingia kama mzee wa kazi ameondoka na kujimilikisha mgodi wa Kiwira.
    Magufuli anayegombea urais wa CCM Alishiriki kikamilifu katika kuuza nyumba za serikali….Ameshiriki kuiingiza hasara serikali majuzi kwenye kivuko ca kigamboni shs Bilioni 8…Kivuko hakina muda wa miezi mitano lakini hakifanyi kazi ….ameiingiza hasara serikali kwa maamuzi mabovu mengi aliyofanya.
    Ndio maana kwa tunaotazama mambo kwa umbali ni bora CCM ikakaa pembeni tuanze upya (Sio kwamba wapinzani ni wazuri sana)…Kutakuwa na maumivu ya miaka 5 lakini baada ya hapo tuta endelea kama taifa.
    Kama taifa inabidi tuweze kufanya maamuzi magumu kwa mustakabali wa vizazi vyetu vijavyo.
    Mfano kulikua na haja gani ya kumilikisha kampuni za wazungu gesi yetu kwa miaka 99…tena kwa mikataba ya siri…….
    Utakuwa kichaa kudahani magufuli ataipitia hio mikataba na kuifumua…You must be mad

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad