Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Manyara, imemhusisha Mbunge wa Babati Mjini, Kisyeri Chambiri (pichani kulia), na tuhuma za kutoa hongo katika kura za maoni ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Takukuru inadai kuwa mbunge huyio alinusurika kukamatwa juzi usiku akiwa na wapambe wake waliokuwa wanagawa rushwa.
Kamanda wa Takukuru mkoani Manyara, Mogasa Mogasa, alisema Chambiri akiwa na wezake watatu ambao wanashikiliwa na taasisi hiyo, alinusurika kwa kutimua mbio usiku majira ya saa nne na kuacha kitita chaSh. 500, 000 alizokuwa nazo katika kijiji cha Kiongozi akitaka kuzigawa kwa baadhi ya watu wake.
Pia taarifa ya kamanda huyo ilieleza kuwa Chambiri alifanikiwa kukimbia akiwa na viongozi kadhaa wa kijiji hicho ambao kamanda huyo hakuta kuwataja majina, akisema kuwa wanaendelea kutafutwa na kumtaka Chambiri ajisalimishe.
Kamanda huyo aliwataja waliyokamatwa kuwa ni Samuel John Barani ambaye ni Katibu wa Uchumi na Fedha CCM wilaya; Thomas Cosmas Darabe na Ally Ayubu Ramadhani, ambao walikuwa na mgombea huyo katika harakati hizo.
Kamanda Mogasa aliongeza kuwa baada ya watuhumiwa hao kukutwa katika eneo hilo na Chambiri kutokomea, walifanikiwa pia kukamata makaratasi yenye majina ya watu waliokuwa wameandaliwa kwa ajili ya mgawo huo.
Hata hivyo, alisema wanaendelea na mahojiano watuhumiwa hao na kwamba baada ya taratibu kukamilika watafikishwa mahakamani na kuongeza kuwa wanalishikilia gari la mbunge huyo.
Chambiri alipoulizwa, alikana kuhusika na kudai kuwa ni mbinu zinazotumiwa na baadhi ya watu wasiyomtakia mema.
Aidha, alidai kuwa yeye kama mgombea na mtetezi wa jimbo hilo, amekuwa akipata taarifa mara kwa mara za kupangiwa njama kama hizo ili kudhoofisha juhuddi zake za kurejea madarakani.
“Hivi walishindwaje kunikamata wakati wanadai walitukuta tukiwa ndani kama siyo uzushi, mimi nafahamu kuna watu wamewekwa kunichunga hata kama naenda nyumbani kisa tu mimi nisichanguliwe, na hiyo ni baada ya kuona watu wameonyesha upendo kwangu,” alisema Chambiri