Kufuatia kutokea sintofahamu iliyopelekea mkutano wa Mwenyekiti wa CUF Profesa Ibrahim Lipumba na Waandishi wa Habari kuahirishwa jana asubuhi hatimaye, mida ya saa nane mchana Prof. Lipumba alijitokeza na kukana kujiulu.
Katika mitandao mbalimbali ya kijamii kuanzia juzi zilienea taarifa kuwa Prof. Lipumba amejiuzulu, suala lililopelekea jana kuitishwa mkutano na Waandishi wa Habari katika ofisi zao zilizopo Buguruni jijini Dar es salaam lakini ghafla mkutano huo uliahirishwa.
Sababu ya kuahirishwa mkutano huo inadaiwa kuwa ni wazee wa chama hicho kumtaka Prof. Lipumba kuwaeleza kile alichopanga kuzungumza na waandishi .
Wazee kadhaa walichaguana na kwenda kuonana naye kujua alichokuwa amekusudia kuzungumza na waandishi wa habari hasa baada ya kuwapo kwa tetesi za kutaka kujiuzulu.
Akizungumza mara baada ya kufanya kikao na wazee hao Prof. Lipumba alisema kuwa hajajiuzulu na kuwataka wanachama kuhakikisha kuwa wanakijenga chama cha CUF.
“Mwaka 1995 nilikuwa mwanachama wa kawaida nilipogombea urais kwa tiketi ya CUF na mwaka 1999 nilikuwa mwanachama wa kawaida nilipoongoza kampeni za Jimbo la Temeke na Ubungo ambapo tulishinda lakini wakatuibia kura.
“Chama ni taasisi na tukijenge kama taasisi, ni wajibu wa kila mwanachama bila kujali nafasi aliyonayo kukijenga,” alisema na kuhitimisha kwa salamu ya; “hakiii” na kujibiwa “kwa wote,”