Ray Chunga Sana Hiyo Bastola Yako Broo!

WAKATI mwingine kazi yetu hii ni ya lawama, kwa sababu kuna wakati unalazimika kuandika kitu cha kweli kuhusu rafiki, ndugu au jamaa yako, lakini ukijua fika hatakipenda na huenda, ikaweza hata kuharibu uhusiano wenu.

Vicent Kigosi maarufu kama Ray, ni mmoja wa watu ambao nimewahi kuwa naye karibu kikazi, kiasi kwamba tulijenga aina flani ya ushkaji, ingawa ukaribu wetu kwa miaka ya karibuni umedorora kutokana na wakati, kwani majukumu ya kila mmoja yameongezeka na aina ya maisha pia imebadilika.

Nilimfahamu kutokana na kazi yake, kwani ukiniambia kuhusu waigizaji waliofanya kazi kubwa kuifikisha sanaa hii ilipo, Ray ni miongoni mwao. Kazi yake kubwa katika filamu Bongo haiwezi kudharaulika hata kama siyo muigizaji mahiri kuliko yule unayempenda.

Alianzia maigizo katika vikundi kwenye televisheni hadi sinema ziliporejea rasmi, zikiasisiwa na Filamu ya Girl Friend mwanzoni mwa miaka ya 2000. Leo hii, Ray ni mmoja wa waigizaji wakubwa wanaoweza kutamba pasipo shaka juu ya mchango wao uliotukuka katika ‘game’.

Lakini kuna jambo moja ambalo nilishawahi kulizungumzia kuhusu huyu jamaa, ambalo kwa maoni yangu, halipendezi, hasa kwa kijana kama yeye mwenye nyendo nyakati za usiku, katika sehemu za burudani na mikusanyiko ya watu wengi.

Ray anamiliki bastola, bila shaka kihalali. Lakini ana tatizo la kutembea nayo bila kuipa hifadhi vile sheria inataka. Katika kumbi za starehe na mijumuiko mbalimbali, bastola ya Ray huonekana akiwa ameichomeka kiunoni.

Kama mara moja au mbili, magazeti ya Global yaliwahi kuandika juu ya jinsi anavyohifadhi bastola yake katika mikusanyiko ya watu wengi. Lakini tukio la Jumapili usiku wiki hii katika Hoteli ya Regency, kulikokuwa na sherehe ya wasanii wenzake, linazidisha hofu juu ya umakini wa muigizaji huyu katika uhifadhi wa silaha hiyo ya moto.

Katika hali ya kawaida, mtu anaweza kumzungumzia kwa namna anavyopenda. Wapo wanaoweza kumwita mshamba, mwenye kutaka kuwaonesha watu kuwa yeye anamiliki bastola, lakini inawezekana kabisa pia kuwa kinachotokea ni bahati mbaya.

Sipo katika makundi ya watu hao, lakini nina ujumbe wangu kwake na pengine jeshi la polisi nchini, ambalo ndilo hutoa kibali kwa watu wanaostahili kumiliki bastola. Ninavyojua, silaha hiyo aliichukua ili imsaidie kujilinda dhidi ya maadui tusiowafahamu.

Katika hali ya kawaida, mwenye hofu na usalama wake, huficha silaha anayoitegemea kumlinda, maana busara haitoi nafasi kwa mtu mwerevu kuwaonesha. Maadui wakijua zana unazotumia kujilinda, si ni rahisi kutafuta njia nzuri ya kukuangamiza?

Na adui siyo yule tu mwenye kutaka kukudhuru mwili, mwingine angependa tu kukuona ukipatwa na misukosuko, maana wapo baadhi ya wenzetu mafanikio yao ni kuwaona wenzao wakitaabika. Katika sehemu za starehe, watu wanapiga mitungi na ikishapanda, busara kidogo hupotea.

Ni rahisi mtu kumuudhi Ray na yeye, katika kumkanya kwamba asiingie anga zake kirahisi, akaamua kumuonesha bastola, hata kama lengo lake siyo kumtishia maisha. Kama hafahamu, kisheria kumuonesha mtu silaha ni kosa linaloweza kumtia hatiani.

Nina uhakika, katika ‘viwanja’ ambavyo Ray anakwenda na kuonesha bastola yake kiunoni, wako makumi ya watu pia wenye silaha kama hiyo, nyingine zikiwa za kisasa na bora zaidi kuliko anayoionesha, lakini wamezihifadhi kwa namna isiyoweza kuonekana kirahisi.

Na kwa jeshi la polisi, nadhani huu ni wakati muafaka wa kumwita na kumwelekeza namna ya kuishi na bastola yake. Huenda kanuni na maadili ya mwanzo ya jinsi ya kuishi na silaha ya moto hakuyaelewa vyema.

Chanzo: GPL
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad