CCM Wakinukisha..Watoa Kauli Kuhusu Lowassa Kujipigia Kampeni Kanisani kwa Kudai Tanzania Haijawahi Kuongozwa na Mlutheri

Katika hali ya kushangaza na kusikitisha tarehe 6/09/2015 siku ya Jumapili mjini Tabora mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chadema Ndg. Edward Lowassa aliamua kutumia udini kuomba kura.

Ndg. Lowassa akihudhuria ibada katika kanisa la Kilutheri (KKKT) mjini Tabora amenukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo mitandao ya kijamii akidai kuwa, kwa kuwa toka nchi ipate uhuru hajawahi kutokea Rais kutoka dhehebu la Kilutheri hivyo mwaka huu ni zamu ya Walutheri.
Chama Cha Mapinduzi kinalaani matumizi ya lugha zinazoligawa Taifa letu kwa misingi ya udini, ukanda, ukabila na ubaguzi wa aina yeyote kisa tu kutafuta madaraka.
Kauli hii ya Ndg. Lowassa licha ya kuwa ni kinyume na Sheria za Uchaguzi za nchi yetu, kinyume na Kanuni za Maadili ya Uchaguzi zilizosainiwa na vyama vyote, lakini ni kinyume kabisa na mila na desturi za Kitanzania katika kuhakikisha Taifa hili linabaki kuwa Taifa moja lenye umoja, amani na mshikamano.
Kwa mfano, Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya Mwaka 2015, yaliyotolewa na Tangazo la Serikali Na. 294 la tarehe 27/7/2015 chini ya kifungu cha 124A cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi sura ya 343, ukurasa wa 5 kifungu 2.1(k) kinasema:-
“Viongozi wa vyama vya siasa, wagombea au wafuasi wao wahakikishe kuwa majengo wanayotumia kufanya kampeni sio ya Ibada. Vile vile, vyama vya siasa vihakikishe kuwa havitumii viongozi wa dini kupiga kampeni kwa ajili ya vyama vya siasa au wagombea wao”.
Lakini katika maadili hayo hayo, ukurasa wa 7, kifungu 2.2(i) kinasema:-
“Vyama vya siasa au Wagombea hawaruhusiwi kuomba kupigiwa kura
kwa misingi ya UDINI, UKABILA, JINSIA AU RANGI.”
Kwa kuwa Ndg. Lowassa siku hizi tabia ya kusahau inaongezeka kwa kasi nimeona ninukuu vifungu hivi kwa rejea yake na wenye tabia kama yake.
Lakini matamshi hayo ni uthibitisho tosha kuwa Ndg. Lowassa, Chama chake cha CHADEMA na vyama vinavyomuunga mkono chini ya UKAWA ni wabaguzi, wachochezi na waroho wa madaraka wasiojali masilahi mapana ya nchi yetu. Kwao madaraka ni muhimu kuliko nchi yetu.
Hii si mara ya kwanza kwa Ndg. Lowassa, Chama chake cha CHADEMA na makada wenzake kutoa kauli na kufanya vitendo vya kibaguzi, kwa kutumia ukanda na sasa wameamua kutumia udini kama njia ya mkato ya kutafuta madaraka.
Chama Cha Mapinduzi kinaamini huu si msimamo wala utamaduni wa Watanzania, bali ni uroho binafsi wa madaraka wa Ndg. Lowassa na chama chake, hasa baada ya kuona kuwa hoja zake za kutafuta nafasi ya juu kabisa ya uongozi wa nchi yetu zimekataliwa na wananchi.
Mwalimu aliwahi kutuonya juu ya wanasiasa wanaotumia udini na ukabila kama hoja ya kutaka kupata madaraka kuwa ni wanasiasa walifilisika kisiasa lakini ni watu wa hatari sana kwa mustakabali wa amani, umoja na mshikamano wa nchi yetu.
Hivyo basi, Chama Cha Mapinduzi kinalaani kauli hii na tunaamini inapaswa kulaaniwa na wote wanaoipenda nchi yetu. Lakini CCM inaamini vyombo vinavyohusika na hasa Tume ya Taifa ya Uchaguzi itachukua hatua zinazostahili kuondoa mbegu hii ya kansa inayoletwa na Ndg. Lowassa kwenye nchi yetu. Maneno ya Ndg. Lowassa ni kansa mbaya kwa nchi yetu na lazima yakemewe na kukomeshwa kabisa.
Maneno na vitendo vya Ndg. Lowassa, chama chake, na makada wenzake wa CHADEMA na vyama shirika vya UKAWA toka wameanza kampeni katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu na kwa nyakati tofauti zimejaa ghiriba na ubaguzi uliokithiri. Tabia hizi za Ndg. Lowassa ni moja ya sababu iliyopelekea CCM kutompa nafasi ya kugombea kupitia Chama hichi.
CCM inatoa wito kwa wadau wote na Watanzania wote kuwa ni vizuri kuwa makini wakati huu wa Uchaguzi, kuhakikisha hakuna jambo linaligawa Taifa letu. Tuendeshe kampeni bila kuligawa na kuliangamiza Taifa letu. Tanzania yetu ni muhimu. Tanzania kwanza mengine baadae.
Imetolewa na;-
Nape Moses Nnauye,
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA
ITIKADI NA UENEZI
08/09/2015
Tags

Top Post Ad

Below Post Ad