Gazeti la Mwanahalisi Lafungulia Rasmi.......Kubenea Ashinda Kesi Mahakama kuu

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania imesema Waziri wa Habari, Dk. Fennela Mkangara hakufuata utaratibu wa kisheria katika kulifungia gazeti la MwanaHALISI Julai 30 miaka mitatu iliyopita.

Jaji Salvatory Bongole amesema Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 aliyoitumia kufungia gazeti hilo lililokuwa linachapishwa kila Jumatano na kampuni ya Hali Halisi Publishers Ltd (HHPL), inaelekeza kuwa pamoja na hatua nyingine kutaka maelezo ya utetezi kwa mchapishaji.

Katika uamuzi wa shauri lililofunguliwa mara baada ya MwanaHALISI kufungiwa, Jaji Bongole amesema gazeti hilo liko huru kuchapishwa kuanzia sasa.

Jaji huyo amesema pamoja na uamuzi huo, kampuni iliyolalamika imepewa mafao yote iliyoyaomba katika kufungua shauri hilo la mapitio ya uamuzi wa Waziri – prerogative orders.

Miongoni mwa maombi ya faida ni HHPL kulipwa gharama za kesi pamoja na fidia kutokana na hasara iliyopatikana kwa muda wote wa gazti hilo kuwa kifungoni.

Wakati Waziri alipofungia gazeti la MwanaHALISI, alieleza kwamba sababu ni kuandika habari na makala za uchochezi.

Habari hasa iliyoikera serikali hata kujilazimisha kuchukua hatua hiyo katili, ilikuwa ni iliyohusu uchunguzi wa tukio la kutekwa na kuteswa hadi karibu na kifo kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari Tanzania (TMA), Dk. Steven Ulimboka.

Dk. Ulimboka alikumbwa na mkasa huo mnamo Juni 2012 alipotekwa usiku eneo la Tazara, karibu na viwanja vya Leaders Club, Kinondoni, ambako aliitwa na mtu aliyemtaja kuwa ni ofisa wa Ofisi ya Waziri Mkuu, ambaye alikuwa na mawasiliano ya karibu naye kwa saa kadhaa siku chache na usiku huo siku ya tukio.

Daktari huyo aliyekuwa mtumishi wa taasisi ya Marekani nchini, alifika eneo la Tazara akifuatana na daktari mwenzake aitwaye Deo, ambaye mara baada ya tukio hilo, wakati wa alfajiri, alimpigia simu Mhariri wa MwanaHALISI, Jabir Idrissa, kumjulisha kuhusu kutekwa kwa Dk. Ulimboka.

Kufuatia habari za kuachiwa huru kwa MwanaHALISI, Mhariri huyo amesema amefurahishwa na uamuzi wa mahakama ya Tanzania, kwa kuwa umethibitisha kosa la serikali la kujichukulia maamuzi mkononi chini ya kuvunja sheria ilizoahidi kuzilinda.

“NImefurahi sana kuthibitishiwa kwamba serikali ilikosea katika kufungia gazeti. Uamuzi wa jaji umesema waziri hakufuata hatua za kisheria alizopaswa kuchukua kabla ya kufungia gazeti, ikiwemo ya kuwapa wamiliki na mhariri nafasi ya kujitetea,” amsema Idrissa.

“Lakini pia uamuzi huu unatakiwa uwe funzo muhimu kwa utawala kwamba hauwezi kudumu na kudumu kwa msisitizo wa kuhifadhi na kufurahia sheria zilizopitwa na wakati ambazo miaka kadhaa nyuma zilishatangazwa kuwa ni sheria kandamizi,” alisema.

Mhariri amesema anawasiliana na mmiliki na mchapishaji wa MwanaHALISI, kampuni ya HHPL, kukamilisha taratibu za kuchapisha toleo la kwanza haraka iwezekanavyo. Gazeti hilo lilikuwa likichapishwa mara moja kwa wiki siku ya Jumatano.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad