Idara ya Uhamiaji kuhoji Uraia wa Zitto ni Matusi kwa Dola na Watanzania

Habari zilizoripotiwa kwenye vyombo vya habari juu ya Idara ya Uhamiaji kuanza kuchunguza Uraia wa ndugu Zitto Kabwe zinapaswa kuhojiwa kwa kuwa zinazua maswali mengi ya kuudhi

Ni kitu gani hasa kilichoisukuma idara hiyo leo kuanza kufuatilia Uraia wa Zitto?

Turejee historia kwa ufupi:

Mwaka 2010 Mgombea wa Upinzani jimbo la Nyamagana Ezekiel Wenje alitangazwa kuwa si Raia. 

Mwaka huo huot Mgombea wa CCM jimbo la Nzega Hussein Bashe aliyekua kinyume na kambi ya mwenyekiti taifa ambae ni Rais alitangazwa si Raia wa Tanzania

-Baada ya Rais Mkapa kuingia madarakani,alipokosolewa vikali Mwanasiasa na mwanaharakati nguli Jenerali Ulimwengu alitangazwa kuwa si Raia

Je,Hili la ndugu Zitto halina unasaba na siasa za majitaka?

Ni nani mwenyehatimiliki ya nchi kiasi kwamba anaweza kuitumia idara nyeti ya umma kuchokonoa,kutishia haki ya msingi ya mtu kwa sababu za kisiasa?

Zitto amekua Mbunge kwa zaidi ya miaka 10 na Amekua Mwenyekiti wa PAC na Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni ambazo ni nafasi nyeti. 

Je,Uhamiaji wanataka kutangaza kuwa Idara ya Usalama wa Taifa hawafanyi kazi yao ipasavyo hadi kumuachia mtu ambae hajulikani alipotoka kuwa na access ya nyaraka nyeti za nchi baada ya kuongoza taasisi muhimu?

Niliwahi kuandika kuwa ukitaka kuthibitisha kama wewe ni raia wa nchi hii basi ikosoe serikali ya Tanzania,gombea ubunge au urais halafu uwabane vilivyo watawala.Kama umezaliwa maeneo ya mipakani au kama rangi yako ya ngozi ni ya asili ya nje ya mipaka yetu utakiona

Hii tabia haipaswi kufumbiwa macho hata kidogo. Ni lazima Idara ya Uhamiaji ieleze msingi wa uchunguzi huo unatokana na nini. Tabia ya kuviziana na kutumia dola ikiachwa iendelee hakuna atakaebaki salama

Cha ajabu watu wenye rekodi ya kupambana na ufisadi na kuonyesha uzalendo kwa nchi ndio wanaokua wa kwanza kutiliwa mashaka juu ya Uraia wao.Inachekesha sana

Hakuna mpinzani wa kweli atakayeunga mkono udhalimu huu.Zitto amekua Naibu kiongozi wa Upinzani na kiongozi wa ngazi ya juu kwa vyama vyote viwili vya upinzani alivyowahi kuwa mwanachama.

Kama tunafika Mahali Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Tanzania anamuomba Mkongomani orodha ya walioficha fedha za Tanzania nchini Uswisi basi Mkongomani huyo uzalendo wake ni zaidi ya ule wa viongozi wakuu wa vyombo vya Dola na hata Rais wa nchi.

Usishangae kukuta kuwa suala hili linaibuka kumnusuru Mgombea wa CCM huko Kigoma mjini.Yaani ili kuzua hisia hasi dhidi yake kutoka kwa wapiga kura tu.

Maslahi ya kisiasa yametamalaki kama yalivyotamalaki katikat mradi wa unyanyasaji aliofanyiwa Jenerali Ulimwengu,Hussein Bashe na Ezekiah Wenje mwaka 2010 na hapo kabla

By the way, Katika Kitabu kilichopigwa marufuku cha "The Dark Side of Julius Nyerere " cha Ludovick Mwijage kulikua na tuhuma ambazo hazikuwahi kujibiwa kuhusu uraia wa Mwalimu Nyerere.Au jibu la Serikali ndio kukifungia kitabu kile?

Mch.Christopher Mtikila aliwahi kuibua tuhuma kuhusu Uraia wa Rais Mkapa kuwa sio Mtanzania .Hazijawahi kujibiwa kiufasaha

Serikali ya CCM wana waziri Mwenye tuhuma za kuwa na Uraia wa Marekani na pia chama kilimkabidhi fomu za Urais. Waziri ni mjumbe wa Baraza la Mawaziri la kumshauri Rais wa Nchi. Lazaro Nyalandu hajawahi kukanusha tuhuma hizi na hata idara ya uhamiaji

Ipo siku wanamuziki Alli Kiba,M wasiti na Wengineo kutoka Kigoma au Mipakani watakapotumia nyimbo zao kuelimisha jamii na kugusa maslahi ya watawala wataanza kuonekana kuwa sio watanzania. Tusikubaliane na ujinga huu

Tuhoji ,Tukosoe na kulaani jaribio lolote la kutumia idara nyeti za nchi kutisha sauti kinzani dhidi ya watawala au watu wachache kwa maslahi yao binafsi. 

Tanzania ni yetu sote,Hakuna mwenyehatimiliki ya nchi hii

Mungu Ibariki Tanzania,Mungu Ibariki Afrika...

Aluta Contimua,Victory Ascerta....

Ben Saanane

Top Post Ad

Below Post Ad