MGOMBEA urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli, ameanza mkakati wa kukusanya kura kutoka vyama tofauti, ikiwemo vyama vinavyounda kundi la Ukawa.
Kwa muda mrefu sasa baada ya kuelezea sera za CCM na namna zitakavyogusa maisha ya wananchi, kuanzia katika afya, elimu na miundombinu mpaka katika kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja na kuboresha makazi, Dk Magufuli amekuwa akiomba kura kutoka vyama hivyo.
Katika mikutano mbalimbali ikiwemo ya Mvomero mkoani Morogoro na wa Kilindi, Tanga juzi, Dk Magufuli alisema maendeleo hayana chama na kuwataka wananchi wa vyama mbalimbali, kumpigia kura ili awatumikie.
Huku akitumia sifa zinazomtambulisha zaidi kwa wananchi kuliko ilivyo kwa wagombea wengine za uadilifu na uchapakazi, Dk Magufuli amekuwa akiwataka wanachama wa Chadema, wanaposalimiwa kwa neno ‘peoples’ na wanapojibu ‘power’, wakumbuke kumpa kura Magufuli ili akawatumikie.
Kwa wanachama wa CUF, ambao wakisalimiana hukunja ngumi yenye vidole vitano, amewataka wakati wakikunja ngumi kuhakikisha wanakwenda kumpigia kura yeye awe Rais wa Awamu ya Tano.
Kwa wanaCCM ambao huonesha alama ya kidole gumba, alichosema kuwa ni alama ya namba moja, nao amewataka wanapokwenda kupiga kura, wampigie kura na kuhakikisha anakuwa namba moja.
Akielezea sababu za kutoa salamu za vyama tofauti katika mikutano yake wakati yeye ni mgombea wa CCM, Dk Magufuli amekuwa akisema kuwa kwanza hakuna Mtanzania hata mmoja aliyezaliwa na kujikuta akiwa katika chama fulani cha siasa.
Pili, Dk Magufuli alisema wanaokwenda katika mikutano yake si wana CCM peke yao, bali pia wapo wanaChadema, wanaCUF, wanaACT na wa vyama vingine na wasio na vyama.
Dk Magufuli pia alisisitiza umuhimu kwa wananchi kutunza umoja, amani na mshikamano wa Watanzania kwa sababu bila vitu hivyo, hakuna kitakachofanyika kuanzia siasa, shughuli za kijamii wala za kiuchumi.
Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Yusufu Makamba, aliwataka wananchi katika uchaguzi huu kutazama sifa za mgombea na sifa za chama. Akitaja baadhi ya sifa za Dk Magufuli, mbali na uadilifu na uchapakazi, Makamba alisema mgombea huyo pia ni msomi kuliko wagombea wengine kwa kuwa ndiye mwenye shahada ya uzamivu (PHD).