MGOMBEA urais wa Tanzania anayewakilisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), Edward Lowassa amesema hana muda wa kujibu matusi na kejeli zinazotolewa na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) dhidi yake.
Badala yake amesema anatumia muda uliobaki wa kampeni kutafuta kura kwa wananchi kwa kunadi ilani ya chama chake.
Akizungumza kwenye mikutano ya hadhara, Bunju na baadaye Mbezi mkoani Dar es Salaam, Lowassa alisema kila alichoahidi ataanza kukifanyia kazi punde tu baada ya kuapishwa:
“Nitajenga viwanda kukabiliana na ajira, ada za shule na mengine ndani ya siku hizo.
“Nikiingia madarakani, hakuna mgeni atakayefanya biashara bila kuingia ubia na wazawa. Lazima tuwajali vijana wetu kwa kuwajengea mazingira wezeshi,” alisema mgombea huyo aliyewasili Bunju saa 9.30 alasiri akitokea Tabora.
Ili kufanikisha hayo, aliwataka vijana kulinda kura zao siku ya uchaguzi ili zisiibwe.
Akizungumza katika mkutano wake uliofanyika kwenye Uwanja cha Shule ya Msingi Bunju ‘A’, Lowassa alisema wananchi wana wasiwasi na NEC kwamba haitatenda haki kwa sababu ya ukaribu wake na CCM.
Aliwataka vijana kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi na kufanya kazi mbili, kwanza kupiga kura na pili ni kulinda kura zao huku akisisitiza kwamba ana uhakika kwamba hataibiwa kura ng’o.
Aliwataka wananchi kufanya uamuzi mgumu kuiondoa CCM madarakani ili wajihakikishie huduma bora za jamii katika serikali ya awamu ya tano.
Alisema zimebaki siku 48 kwa wananchi kuamua hatima ya maisha yao yajayo akiwataka kuwachagua wagombea wa Ukawa ili waondoe msongamano wa magari jijini, kuboresha mfumo wa elimu kuanzisha viwanda vitakavyotengeneza ajira kwa wananchi.
Awali, akimkaribisha Lowassa, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye alisema ili kuepuka vurugu, lazima CCM wakubali kushindwa na kupisha serikali mpya ya Ukawa.
Alisisitiza kuwa ameihama CCM baada ya kubaini kuwa mabadiliko hayawezi kupatikana ndani ya chama hicho.
Alimtaka mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli kuzungumzia kashfa mbalimbali zinazoikabili Serikali ya sasa ambazo ni pamoja na usafirishwaji wa twiga, dawa za kulevya na pembe za ndovu.
“Ndani ya CCM huwezi kufanya chochote, CCM ni shida,” alisema Sumaye na kuongeza kuwa uchumi umeshuka tofauti na miaka 10 iliyopita.
Alisema Ukawa ikiingia madarakani, itahakikisha fedha zote zilizofichwa nje ya nchi zinarudishwa na wahusika wake kuchukuliwa hatua za kisheria.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema: “NEC watasababisha machafuko kwa kuibeba CCM. Chama hicho kwa sasa hakibebeki, sasa wameanza kuwatumia watu kumchafua Lowassa.”
Alisema ziara ya kampeni za umoja huo katika mikoa saba, imeonyesha kwamba wananchi wako tayari kwa mabadiliko na kuipokea serikali ya Ukawa.
Awali, mgombea ubunge wa Jimbo la Kawe (Chadema), Halima Mdee alimtaka Lowassa kusaidia kutatua migogoro ya ardhi katika jimbo hilo hasa eneo la Boko.
Alisema uhakiki wa majina katika daftari la kudumu linaendeshwa kihuni kwa sababu wananchi wakienda kwenye vituo hawalioni.
Mgombea huyo wa urais alihitimisha kampeni zake Bunju saa 10.30 jioni na kuelekea Mbezi kwa ajili ya mkutano mwingine ambao ulimalizika saa 12.15 jioni.
Akiwa Mbezi
Baada ya kuwasili Mbezi saa 11.15, Lowassa aliwaomba wakazi wa Jimbo la Kibamba wamchague pamoja na mbunge na madiwani wa Ukawa ili waweze kumsaidia kuleta mabadiliko yatakayoboresha maisha ya wananchi.
Alisema kumekuwa na tuhuma nyingi dhidi yake, lakini akasema ataendelea kufanya kampeni za kistaarabu ili kuwaeleza wananchi nini anataka kukifanya.
“Wananikashifu kwa maneno mengi, eti wanashangaa mimi kupanda daladala sasa, lakini hawashangai twiga kupanda ndege,” alisema.
Awali, Sumaye alisema hawezi kujibizana na aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Yusuph Makamba kwa sababu naye ataonekana amepungukiwa.
Sumaye alisema Chadema ikishinda uchaguzi, kazi ya kwanza itakuwa kutaifisha na kurudisha fedha zilizowekwa na vigogo wa serikali nje ya nchi.
“Kazi ya kwanza itakuwa kurudisha fedha zilizoibwa na vigogo wa Serikali ya CCM, tutazirudisha na kuziweka katika Hazina yetu,” alisema.
Sumaye ambaye mara kwa mara alitumia kaulimbiu ya “CCM” na wananchi kumjibu ni “shidaaa”, alisema tangu Lowassa ajiuzulu kashfa za ufisadi wa fedha za Serikali umeongezeka.
Mbowe ambaye pia Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, aliwataka wananchi hao kuhakikisha wanatunza vitambulisho vya kupigia kura ili waweze kufanya uamuzi sahihi Oktoba 25.
“Mlivyohamasika mnaonyesha kwamba mmekubali mabadiliko, hivyo jambo la msingi ni kutunza vitambulisho vyenu ili siku ya uchaguzi muweze kuwachagua viongozi wa Ukawa,” alisema.
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Kibamba (Chadema), John Mnyika aliomba kura kwa wagombea wote wa Ukawa ili waweze kuleta maendeleo.
“Umati huu unaonyesha kwamba wananchi mna imani na viongozi wanaogombea kupitia Ukawa, tunaomba mtuchague,” alisema.
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Ubungo kupitia chama hicho, Saed Kubenea aliwaomba wananchi wawachague viongozi wa Ukawa ili waende bungeni kuwatetea wananchi
Ilivyokuwa
Wafuasi wa Ukawa walianza kufika katika Uwanja wa Bunju A tangu saa nne asubuhi wakiwa wamejipamba kwa mavazi ya sare za vyama vinavyounda umoja huo.
Baadhi ya wafuasi hao wakiwa na bendera za vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi, muda wote walikuwa wakiimba na kucheza nyimbo za Chadema.
Wafuasi hao walikuwa wakipuliza matarumbeta kwenye barabara inayopita jirani na uwanja huo huku baadhi ya magari yaliyokuwa yakipita eneo hilo, yakiunga mkono kwa kupuliza honi.
Madereva wengi kati ya hao, walikuwa wakinyanyua mikono juu na kuonyesha alama ya vidole viwili ambayo inatumiwa na Chadema.
Wafuasi wa chama hicho walipouona msafara wa Lowassa ukiwasili katika viwanja hivyo saa 9.30 alasiri walishangilia kwa sauti ya juu huku wakiimba rais, rais, rais.
Baada ya mkutano kumalizika kwenye viwanja hivyo na msafara wake kuanza safari ya kuelekea Mbezi, saa 10.40 jioni, karibu kila eneo alikopita, wananchi walionekana wakiwa wamejipanga kando ya barabara wakimshangilia, wengi wao wakionyesha alama ya vidole viwili.
Mbali ya kujipanga barabarani, katika baadhi ya maeneo, wananchi walipanda juu ya miti ili wapate kuuangalia vyema msafara huo ulipitia Goba hadi Mbezi.
Huko Mbezi, wananchi walikuwa wamefurika kwenye uwanja wa mkutano tangu saa nane mchana.
Sababu za kuchelewa
Akizungumzia sababu ya kuchelewa kwa mikutano hiyo ambao wa Bunju ulipangwa kuanza saa nne asubuhi na Mbezi saa tisa alasiri, Mbowe alisema hiyo ilisababishwa na kuunganisha safari jana hiyohiyo kutoka Tabora kupitia Dodoma.
“Tunawaomba radhi kwa kuchelewa kuanza kwa sababu ya safari ndefu,” alisema Mbowe.
Pamoja na mkutano huo kumalizika dakika 15 zaidi ya muda uliowekwa na NEC, Polisi waliokuwapo hawakuonekana kuchukua hatua yoyote.