Mzee Makamba |
Makamba amesema hayo jana katika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, alipopewa nafasi ya kusalimia wananchi wa Morogoro, ambapo aliamua kutoa baadhi ya siri ambazo hazijawekwa hadharani.
Alimtuhumu Waziri Mkuu huyo wa zamani kwa ufisadi wa kupora ranchi za taifa katika mikoa ya Tanga na Arusha na kumpatia zabuni zote dada yake katika Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, ambako Lowassa alikuwa mbunge.
Akizungumzia madai ya Lowassa kwamba anachukia umasikini wa Watanzania, Makamba alisema Lowassa hachukii umasikini wa Watanzania, bali anachukia umasikini wa kwake na ndio maana hajaacha kujilimbikizia mali.
Makamba alidai kuwa Lowassa alipokuwa Waziri wa Maji na Mifugo, alipora iliyokuwa Ranchi ya Taifa ya Mkata iliyopo Tanga, ambayo imezungukwa na vijiji vya Tototwa, Mabwegere, Kiduhu na Tambara.
Katibu Mkuu huyo alihoji kama Lowassa alikuwa na uchungu na wananchi, kwa nini hakuwapa wananchi wa vijiji hivyo, badala yake akaichukua yeye na rafiki yake aliyedai ni wa Hoteli ya Nam.
Ranchi ya pili anayodaiwa kuipora ni ya Mzeri iliyopo Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, ambayo Makamba alidai kuwa ranchi hiyo iliyokuwa ya Ushirika, Lowassa aliipora na ina ng’ombe ambayo akiitembelea hawezi kuimaliza bila kutumia helkopta.
Makamba alikwenda mbali zaidi na kusema mkoani Arusha wakati akiwa Katibu Mtendaji wa CCM, Lowassa alipora tena ranchi nyingine ya Leteni.
Mbali na uporaji huo wa ardhi, Makamba alisema Lowassa pia amempa dada yake, ambaye hakumtaja jina, zabuni zote za Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, mpaka zabuni za kuiuzia halmashauri hiyo penseli.
Baada ya kutoa tuhuma hizo, Makamba alisema ameweka akiba maneno mengine na kumtaka Lowassa, atoke hadharani aseme hayo ili na yeye Makamba ajibu mahali pengine.
Alisema Lowassa alitaka kujitoa CCM mwaka 1995 wakati alipokatwa katika kinyang’anyiro cha kumpata mgombea urais wa CCM mkoani Dodoma.
Makamba alidai kuwa walipokwenda katika kikao cha NEC ambacho kilihudhuriwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alihoji kwa nini jina la Lowassa halikuletwa miongoni mwa wagombea watano wenye sifa.
“Nilijibiwa Lowassa ni kijana mdogo, lakini ana utajiri mkubwa ambao haujulikani alikoupata. Nikauliza ameulizwa nikajibiwa hapana nikasisitiza aulizwe maana ndio utaratibu wa chama. Lakini Mwalimu Nyerere alinijibu Lowassa akija muulize wewe mwenyewe.
“Lowassa alipoingia katika kikao, nikaitwa Makamba ulikuwa na hoja, nikasimama nikamwambia bwana wewe Lowassa umekatwa jina lako kwa kuwa una utajiri ambao haujulikani ulipoutoa,” alidai Makamba.
Kwa mujibu wa madai ya Makamba, Lowassa alijibu kuwa ni kweli ana utajiri lakini ni kama wa watu wengine na alishindwa kutoa maelezo ya kutosha kuhusu alikotoa mali hizo