Mzindakaya: Msipige Kura kwa Ushabiki


MWANASIASA mkongwe nchini na kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Chrisant Mzindakaya amewataka Watanzania wasikubali kupiga kura kwa ushabiki. Ameonya kuwa upigaji kura kwa ushabiki, utaligharimu taifa hivyo Watanzania wapige kura wakijua wanachagua kiongozi ambaye atawakilisha nchi kitaifa na kimataifa.

Mzindakaya alisema hayo jijini Dar es Salaam jana katika mkutano wake na waandishi wa habari. Alisema ameamua kujitokeza kutoa ushauri kwa Watanzania, kama mwananchi wa kawaida na pia kama kiongozi ambaye anawafahamu kwa ukaribu wagombea wote wanaowania kiti cha Urais.

“Naomba Watanzania, wapiga kura wenzangu wasikubali kupiga kura kwa ushabiki, wapige kura wakijua wanachagua kiongozi wa Mungu, kiongozi ambaye atawakilisha nchi yetu kitaifa na kimataifa, na katika hili mimi sina maslahi yoyote,” alisema Dk Mzindakaya.

Mzindakaya alisema yeye ni mstaafu baada ya kutumikia taifa kwa muda mrefu, hivyo hana maslahi yoyote binafsi katika kutoa ushauri huo kwa Watanzania, ambao ndio wapiga kura watakaomchagua kiongozi.
 
“Mimi ni mstaafu, sina maslahi yoyote katika hili, sihitaji kuteuliwa uwaziri au ukuu wa mkoa wala nafasi yoyote ile, lakini naipenda nchi yangu na ninayaona mafanikio ya nchi yangu ambayo yako waziwazi,” alisema Mzindakaya.

Dk Mzindakaya alimpongeza Rais Jakaya Kikwete kuwa na mipango madhubuti ya kuliletea taifa maendeleo na kufanya mabadiliko makubwa, ambayo yanaonekana na kuwanufaisha watu wengi.
 

Lakini, alisema kuna baadhi ya watu hawapendi kuona na kusifu maendeleo ya nchi yao, badala yake wanaendelea kubeza kwamba hakuna kilichofanyika.

Alisema kuna watu wanaingiza ushabiki kwa kisingizio cha kutaka mabadiliko. Aliwashauri vijana wajue kuwa nchi hii ni mali yao, hivyo hata kama wanataka mabadiliko waangalie ni kiongozi gani wanataka kumkabidhi nchi awaletee mabadiliko.

“Vijana chungeni nchi hii ni mali yenu, ni nchi yenu msipige kura kwa ushabiki nawapeni ushauri na ushauri huu hauna gharama, ila usipozingatiwa mtakuja kuona gharama yake baadaye, sisi ni wazee tumetumikia taifa hili na sasa tumestaafu,” alisema.

Dk Mzindakaya alisema Ikulu ni mahali patukufu kwa sababu serikali za dunia zinatambuliwa na Mungu, hivyo Rais anamwakilisha Mungu duniani.
 
 Alisisitiza kuwa nchi inahitaji kuwa na Rais, ambaye sio tu atakuwa na uwezo mzuri wa kuongoza nchi, lakini pia awe na mikono safi.

Alisema amekuwa mbunge kwa miaka 44 na viongozi wote wanaotafuta urais, anawafahamu kwa sababu amefanya nao kazi, hivyo anajua vizuri utendaji kazi wao kwa undani zaidi.
 
 Mzindakaya alisema mamlaka ya Rais ni makubwa mno, ambayo yanahitaji mtu makini asiye na pupa na mcha Mungu, ambapo yeye alisema ukilinganisha na wagombea wengine, kwa maoni yake, anaona mgombea wa kupitia CCM, Dk John Magufuli anaweza kuwa kiongozi mzuri.

“Tusipige kura ya ushabiki baadaye tukaja kujuta, kura ya rais inatufanya tuchague kiongozi atakayewakilisha nje pia ya mipaka ya nchi, na kwa maoni yangu naona Magufuli anafaa sana,” alisema Mzindakaya.

Alisema katika kipindi cha miaka mitano hadi kumi ijayo, nchi hii itakuwa tajiri barani Afrika kutokana na misingi iliyowekwa na viongozi waliopita kuibua vitu, ambavyo vitapandisha uchumi wa nchi, kama vile uchimbaji wa gesi, kiwanda cha chuma cha Liganga na uzalishaji wa magadi soda.

Top Post Ad

Below Post Ad