TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema waangalizi wa uchaguzi mkuu utakaofanyika 25 Oktoba, mwaka huu wataruhusiwa kushiriki katika uangalizi wa hatua zote za upigaji kura, kuhesabu na kutangaza matokeo ya uchaguzi katika vituo vya kupigia kura.
Waangalizi wa kimataifa 600 wanatarajiwa kusimamia zoezi la uchaguzi mkuu wa tano tangu kurudishwa mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1992 ambapo uchaguzi wa ulifanyika kwa mara ya kwanza mwaka 1995.
Katika uchaguzi wa mwaka huu, Watanzania wapatao milioni 23.7 ndani ya nchi na waliotimiza masharti ya kupiga kura, wanatarajiwa kuchagua viongozi ngazi za udiwani, ubunge na urais.
Uchaguzi huo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na kuungana kwa vyama vinne vya upinzania vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
Vyama hivyo ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), National League for Democracy (NLD), Chama cha Wananchi (CUF) na NCCR – Mageuzi.
Pia sababu nyingine inayotajwa katika kuchochea ushindani mkali ni mawaziri wakuu wastaafu wawili, Edward Lowassa na Frederick Sumaye kujiunga na upinzani wakitokea Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho ndio chama tawala.
Akizungumza katika mahojiano maalum na MwanaHALISI Online, leo mchana, Kaimu Mkurugenzi wa Sheria NEC, Emmanuel Kawishe amesema “Kati ya watu watakao ruhusiwa kuingia ndani ya chumba cha kupigia kura ni waangalizi wa uchaguzi kutoka ndani na nje ya nchi.
“Watazamaji hawa watashiriki katika kila hatua za upigaji kura, kuhesabu na kutangaza matokeo katika vituo vya uchaguzi, ili mradi wawe na kibali kinachowatambulisha kutoka NEC,” amesema Kawishe.
Hata hivyo Jumanne wiki iliyopita, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe akizungumza na mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao Tanzania aliwataka waangalizi hao kutotoa tamko lolote linalohusu kampeni au uchaguzi kabla ya NEC kufanya hivyo.
Kawishe amesema watu wengine watakaoruhusiwa kuingia ndani ya chumba cha kupigia kura ni msimamizi mkuu wa uchaguzi katika kituo na wasaidizi wake wawili kutoka NEC na mawakala wa vyama vya siasa ambapo kila chama kinachoshiriki katika uchaguzi kitawakilishwa na wakala mmoja.
“Pia nje ya kituo kutakuwepo na askari polisi. Askari hawa hawataruhusiwa kuingia ndani ya chumba cha kupigia kura. Watakaa nje kuangalia hali ya usalama. Na ataruhusiwa kuingia ndani ya chumba cha kupiga kura iwapo atatakiwa kufanya hivyo na msimamizi wa uchaguzi katika kituo na si vinginevyo,” amesema Kawishe.
Aidha, nje ya kituo kutakuwepo na karani mmoja kutoka NEC ambaye atakuwa na kazi ya kutoa maelekeo kwa wapiga kura ikiwemo ni hatua gani wafuate baada ya kufika katika kituo cha kupigia kura.
MUNGU IBARIKI TANZANIA
ReplyDelete