Ni LOWASSA Kila Kona ya Nchi....Mpaka Watoto Lowassa Lowassa

Hakuna shaka kwamba jina la Edward Lowassa (pichani), ndilo linalozungumzwa zaidi kwenye kampeni za urais zinazoendelea sasa;iwe kwa mazuri au mabaya.

Wakati Chadema na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), vikiendelea kulinadi jina la Lowassa kwa mazuri katika mikutano ya kampeni, CCM na vyama vingine vimekuwa vikeleza kuwa mgombea huyo wa Ukawa hafai kuwa Rais.

Mbali na vyama hivyo, katibu wa zamani wa Chadema, Dk Willibrod Slaa naye amekuwa gumzo katika siku za karibuni, akipinga chama hicho kumkubali Lowassa kuwa mgombea urais, hali kadhalika, mchambuzi maarufu wa siasa, Humphrey Polepole ambaye amekuwa akieleza mara kwa mara kuwa Ukawa imevunja misingi ya kuanzishwa kwake kwa kumpokea Lowassa na kumpa fursa hiyo.

Anavyotajwa CCM
Kwenye kampeni za CCM, Lowassa huwa hatajwi na mgombea urais wa chama hicho, Dk John Magufuli, lakini makada ambao hutangulia kuzungumza kabla yake, wamekuwa wakiporomosha tuhuma nzito kujaribu kushawishi wananchi kuwa waziri huyo mkuu wa zamani hafai.

Miongoni mwa makada hao ni mgombea ubunge wa Kyela, Dk Harrison Mwakyembe ambaye alidiriki kusema kuwa Lowassa anaweza kushtakiwa wakati wowote kutokana na kuhusika kwake kwenye sakata la mkataba wa uzalishaji umeme wa dharura baina ya Serikali na kampuni ya Richmond Development ya Marekani.

Pia, katibu mkuu wa zamani wa CCM, Yusuf Makamba amekuwa akieleza udhaifu wa Lowassa katika mikutano ya hivi karibuni, huku mgombea ubunge wa Mtera, Livingstone Lusinde akirusha makombora kuhusu hali ya mgombea huyo wa Ukawa.

Anavyotajwa Ukawa
Lakini Ukawa na Chadema, ambayo ilijipatia umaarufu kutokana na kupiga vita ufisadi, wamekuwa wakimtaja Lowassa wakati wakimtetea dhidi ya kashfa za ufisadi, huku wakimtangaza kwa kutumia msemo wa “Lowassa, mabadiliko; mabadiliko Lowassa”.

Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, ambaye alitangaza kuondoka CCM na kujiunga na harakati za Ukawa bila ya kutaja chama anachohamia, amekuwa akijaribu kuwashawishi wananchi kuwa CCM ndiko kuliko na ufisadi mwingi zaidi ya huo wanaomtuhumu Lowassa, huku akimtetea kuwa katika sakata la Richmond alifanya hivyo kwa maelekezo ya mkuu wake.

Amekuwa akijenga hoja yake kwa kutumia ufisadi uliotokea baada ya Lowassa kujiuzulu uwaziri mkuu mwaka 2008, kama kashfa ya wizi wa fedha kwenye Akaunti ya EPA, uchotwaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow, utekelezaji mbovu wa Operesheni Tokomeza na uchelewashaji wa malipo ya makandarasi wa barabara ulioligharimu Taifa Sh900 bilioni.

Maoni ya wadau
Kashfa hizo na kampeni za kumnadi, zimelifanya jina la Lowassa kutajwa zaidi kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

“Ni kweli viongozi wa CCM wanatumia muda mwingi kumshambulia Lowassa,” alisema kada wa chama hicho, Aman Ngowi alipoulizwa kuhusu sababu za jina la waziri mkuu huyo kutamba kwenye karibu mikutano ya vyama vyote.

“Lakini pia, vyombo vya habari vinachangia. Viongozi wetu kwenye msafara wa mgombea wa CCM, Dk Magufuli wanaweza kuzungumza mambo mazuri 20, lakini likitajwa moja tu linalomhusu Lowassa, magazeti yote kesho yake ni Lowassa,” alisema Ngowi.

Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Makongoro Nyerere na ambaye amekuwa akisimama kwenye kampeni kumshambulia Lowassa, alisema Tanzania inakabiliwa na tatizo la ufisadi na rushwa.

Makongoro, ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya kampeni ya CCM, alisema kwa kuwa ufisadi bado ni tatizo, wataendelea kuwaeleza Watanzania katika kampeni zao kuwa mgombea huyo wa Chadema ni fisadi.

“Hatuwezi kunyamaza wakati tunamwona fisadi anaomba nafasi ya urais, ni lazima tuwaeleze Watanzania kuwa huyo ni mtu hatari kwenu,” alisema.

Alidai viongozi wa Chadema wamenunuliwa ndiyo maana hawakemei tena ufisadi wakati ndiyo walioanza kumwita kwa jina hilo.

Alisema siyo Chadema pekee yao ambao hawazungumzii ufisadi, bali vyama vyote vinavyounda Ukawa.

“Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi wako kimya hawataki kusikia neno ufisadi kwa sababu wamehongwa,” alisema.

Kauli ya Makongoro iliungwa mkono na Lusinde ambaye alisema kwa kuwa Chadema hawazungumzii tena ufisadi, CCM wataendelea kuwaambia wananchi kuwa mgombea huyo ni fisadi.

“Tunayemtafuta hapa ni Rais, ndiyo maana tunasema tutaendelea kuwaeleza Watanzania kuwa Lowassa ni fisadi na wasimchague,” alisema.

“Muda huu ndiyo natoka Bagamoyo kwenye mkutano wa kampeni, nimewaeleza wananchi kuwa wamwogope Lowassa kama ukoma kwa sababu akichukua nchi itakuwa ya mafisadi na wala rushwa.”

Lakini, Dk Benson Bana wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) anatetea hali hiyo akisema ni vigumu wanasiasa kuepuka kutaja udhaifu wa wapinzani kwenye mikutano yao.

Alisema Watanzania ni lazima wakubali kwamba katika kipindi hiki cha kampeni, wagombea watatangaza sera zao, lakini hawawezi kuacha kutaja udhaifu wa washindani wao

“Ndiyo sababu ya kumtaja Lowassa,” alisema mkuu huyo wa kitengo cha sayansi ya siasa.

“Chadema ndiyo walioanza kumwita Lowassa fisadi na wanachokifanya CCM hivi sasa wanarudia tu. Lakini waasisi wa hilo ni Chadema.

“Unategemea leo CCM wataacha kusema kwenye kampeni kuwa Lowassa ni fisadi wakati kuna ushindani mkali?”

Alisema jambo la muhimu hapo ni matumizi ya lugha yenye staha na vyama kufanya kampeni za kistaarabu.

Lakini Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Ruco), anaona kutajwa huko kwa jina la Lowassa kunatokana na mgombea huyo wa urais wa Chadema kuwa tishio kwa CCM.

Alisema kinachotakiwa ni kuwaeleza wananchi sera za vyama vyao ili kuwashawishi, lakini utaratibu wa siasa za kupakana matope hauna maana kwa wananchi.

“Kila siku Lowassa fisadi, hizi ni siasa za majitaka, wananchi wanahitaji kufahamu mtawafanyia nini endapo mtachaguliwa,” alisema.

Maoni kama hayo yalitolewa na mwenyekiti wa zamani wa CCM mkoani Kilimanjaro, Peter David ambaye alieleza kutofurahishwa na aina hiyo ya kampeni.

Alisema kampeni zinazofanywa na baadhi ya makada wenzake wa CCM za kuchafuana majina majukwaani, si nzuri na akataka wanadi sera.

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Hellen Kijo - Bisimba alisema CCM haijiamini, ndiyo maana hivi sasa inazungumzia mtu badala ya masuala.

“Muda wote Lowassa fisadi, Lowassa fisadi, watu hawajui vyama vitasimamia masuala gani. Waache kushughulika na mtu, waeleze hoja, waseme watafanya nini kama watachaguliwa,” alisema.

“Ukiona wanazungumzia mtu, ujue hali ni ngumu kwao lakini watu wanaojiamini huzungumzia hoja.”

Alisema wagombea kuzungumzia kashfa za ufisadi kila siku badala ya sera, matokeo yake watajikuta wanaangushwa kwenye uchaguzi.

“Watu wanawapima kwa sera zenu, sasa kama muda mwingi unautumia kuwatuhumu watu utajikuta huna sera ulizoziuza kwa wananchi,” alisema.

Wakili wa kampuni ya MM Law Chamber, Mohamed Menyanga alikuwa na maoni kama ya Kijo-Bisimba.

“CCM inamwogopa Lowassa ndiyo maana kila wakati inamhusisha na kashfa ya ufisadi wakati haina ushahidi,” alisema Menyanga.

“Muda mwingi wautumie kuwaeleza wananchi kwa nini ahadi walizozitoa hawajazitekeleza na siyo kila wakati Lowassa fisadi. Hii haitawasaidia wananchi,” alisema.

Aliungana na Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Dk Emmanuel Mallya aliyesema ushindani ni mkali katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu ndiyo maana wagombea wanatumia kila aina ya ‘silaha’ ili kuwashinda washindani wao.

Alisema wananchi wana haki ya kusikia sera za vyama badala ya kashfa za ufisadi kuanzia mwanzo wa kampeni hadi mwisho.

Wakili mwingine wa kujitegemea, Carnelius Kariwa wa Dar es Salaam, alisema anachokiona kwa sasa, kampeni za CCM zinapoteza mwelekeo na malengo.

“Polepole wameanza kupoteza malengo ya msingi ya kampeni. Lengo la kampeni ni kuuza sera siyo kuchafuana. Wamelenga mtu badala ya kuangalia nini Watanzania wanataka.

“Walidhani wakipiga propaganda dhidi ya Lowassa, Sumaye na makada wa CCM waliohamia Ukawa wangechafuka lakini wameshindwa kusoma alama za nyakati nini wanachokitaka Watanzania,” alisema.

Wakili Kariwa, alikwenda mbali akisema Watanzania walio wengi wanataka mabadiliko, hivyo hata Dk Magufuli angekuwa anagombea kwa tiketi ya Ukawa na Lowassa CCM, Dk Magufuli ndiye angeng’ara.

Mawazo ya Wakili hiyo yanatofautiana na yale ya kada wa ACT – Wazalendo, Buni Ramole aliyesema CCM imetambua kuwa adui yao mkubwa katika suala la urais kwa sasa ni Lowassa na ndiyo maana inatumia nguvu kubwa kumshambulia.

“Kwa hali ya kawaida, chama kikongwe kama CCM kilichokaa madarakani kwa miaka zaidi ya 50 hakikupaswa kujinadi kwa kuwasema watu, bali kujinadi kwa mafanikio wala siyo ahadi tena,” alisema Ramole.

Askofu Mkuu wa Kanisa la Kilutheri Afrika Mashariki (KKAM), Jesse Angowi alisema kitendo cha makada wa CCM kutumia muda mwingi kumshambulia Lowassa hakimchafui, badala yake kinamng’arisha.

Hata hivyo, Askofu huyo alisema kwa jinsi mwelekeo wa kampeni ulivyo, ni dhahiri rais atatoka ama CCM au Chadema kupitia Ukawa.

Askofu Angowi alisema haridhishwi na namna CCM ilivyobadili mwelekeo wa kampeni na kutumia muda mwingi majukwaani kumshambulia Lowassa badala ya kutumia muda huo kunadi sera zake.

“Lowassa na Sumaye walikuwa mawaziri wakuu walikuwa wasafi walipokuwa CCM hadi wakashika nyadhifa hizo. Leo ghafla wamekuwa makapi na kushambuliwa hivyo?”

Lowassa amekuwa na nia ya kugombea urais kwa muda mrefu tangu mwaka 1995 wakati jina lake lilipokatwa. hakuchukua fomu mwaka 2005 wakati Jakaya Kikwete, aliyekuwa rafiki yake wa karibu, alipogombea.

Lowassa alisema kuwa walikubaliana na Kikwete kwamba waunganishe nguvu ili awamu inayofuata iwe zamu ya mbunge huyo wa Monduli.

Hata hivyo, mwaka huu jina la Lowassa lilikatwa na ya makada wengine 33, na ndipo akaamua kujiunga na Chadema kuendeleza ndoto yake ya kuingia Ikulu.

Top Post Ad

Below Post Ad