Tanzania yang'ara kwa Amani! Ya kwanza East Africa...

TANZANIA imeelezwa kuwa nchi yenye amani zaidi na utulivu mkubwa kuliko nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ikishikilia nafasi ya 55 duniani kati ya nchi 162 ambako utafiti kuhusu hali ya amani na usalama umefanyika.

Utafiti huo unaojulikana kama The 2013 Global Peace Index (GPI) uliofanywa na Taasisi ya Kimataifa ya Uchumi na Amani, ambayo madhumuni yake ni kuchochea maelewano zaidi duniani katika maeneo ya uchumi, biashara na amani, unaonesha kuwa Uganda ni ya pili kwa EAC ikiwa inashikilia nafasi ya 106, Kenya ya 136 na Burundi ni ya 144.

Wakati Tanzania iking’ara kwa mujibu wa ripoti hiyo, Rwanda ni moja ya nchi za mwisho duniani ikionekana kukosa utulivu na amani. Kwa miaka sita iliyopita, Rwanda imewekwa kundi moja na nchi hatari zaidi duniani za Syria na Libya kwa ukosefu wa amani na utulivu.

Kwa kuiweka Rwanda katika nafasi ya 135 miongoni mwa nchi 162 zilizotafitiwa, ripoti hiyo inapingana na msimamo wa Serikali ya nchi hiyo ambayo imekuwa ikisema ni miongoni mwa nchi zenye amani na utulivu zaidi duniani.

Waandishi wa ripoti hiyo wanasema nchi za Ulaya za Nordic ambazo pia zina demokrasia iliyokomaa na kutulia zaidi, ndizo zenye amani na utulivu mkubwa duniani na kuthibitisha uhusiano kati ya utawala wa sheria na ushiriki wa wananchi katika kuwapo ama kutokuwapo kwa amani.

Tanzania imekuwa inapata alama za juu kabisa katika suala la utulivu na amani kwa miaka mingi na zamu hii watafiti wanasema sababu ya kuendelea kwa amani na utulivu huo ni viongozi kuheshimu misingi ya utawala bora likiwamo suala la kuheshimu vipindi viwili vya urais na ukweli, kwamba Tanzania haijapata kukabiliwa na zahama kubwa ya mapambano ya ndani tofauti na nchi jirani.

Ripoti hiyo inasema: “Nchi tatu ambazo zimekuwa na mabadiliko makubwa kwa kuongezeka kwa amani katika miaka sita iliyopita, ni Chad, Georgia na Haiti wakati nchi zilizorudi nyuma kwa haraka na kwa kasi zaidi ni Syria, Libya na Rwanda.”

Lakini hata hivyo, ripoti hiyo imepokewa kwa hisia tofauti nchini Rwanda. Wakati Serikali inaonesha kupingana na matokeo hayo, watu wengine wanayaunga mkono.

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa chuo kikuu nchini humo, alisema kuna tofauti kati ya amani na usalama, akisisitiza kuwa kutokuwapo vita hakuna maana kuwa wananchi wanaishi kwa amani.

“Amani maana yake ni watu kupata fursa ya maendeleo na kujiendeleza.” Anaongeza: “Watu wanataka kushiriki uendeshaji wa nchi yao. Angalia Bunge letu, si la uwakilishi. Ni jambo la kuchekesha kwamba tuna Rais aliyechaguliwa, lakini si Bunge lililochaguliwa na wananchi.

“Hatuna uhakika na mchakato wa mpito kutoka utawala wa sasa kwenda mwingine. Tunabanwa pia kutokana na uhusiano wetu na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC)…kuweza kutembea usiku bila silaha hakutoshi.”

Aidha, Rwanda inashutumiwa kwa kukandamiza vyombo vya habari na wapinzani wa kisiasa. Inarudi nyuma kwa sababu ya ushiriki wake katika kuchochea uasi ndani ya DRC na ongezeko kubwa la vitendo vya kigaidi na mauaji ndani ya Rwanda yenyewe.

Hivi karibuni, Rwanda imeshuhudia milipuko ya mabomu ambayo Serikali inasema yalilipuliwa na wapinzani wake.

Kuhusu hatua za Serikali ya Rwanda kubana vyombo vya habari na wapinzani wake, maana yake ni kwamba inashuhudia kile kinachoelezwa kwenye Ripoti hiyo kuwa ni ongezeko la kiwango cha vitisho vya kisiasa ikiwa na idadi kubwa ya watu waliofungwa jela, kuyumba kisiasa, kiwango kikubwa cha mauaji na vitendo vya kigaidi.”

Taasisi ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani wa Waandishi Wasio na Mipaka (RWB)inakadiria kuwa uhuru wa vyombo vya habari nchini Rwanda ni mbaya na kuifanya nchi hiyo kuwa moja ya nchi 10 mbaya zaidi duniani ikishikilia nafasi ya 168 kati ya nchi 179 zilizofanyiwa utafiti mwaka jana.

Chanzo: HabariLeo - Juni 25, 2013
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad