UVCCM: Magufuli akubalika asilimia 85


CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeonesha mafanikio makubwa kwa mgombea wake wa urais, Dk John Magufuli kukubalika kwa wananchi katika kampeni zake mikoani, huku Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ukisema mgombea wake, Edward Lowassa anakubalika vivyo hivyo.

Hatua hiyo imekuja baada ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), kusema imefanya tathmini ya mgombea wake urais, Dk. John Magufuli na kubaini kuwa amekubalika kwa asilimia 85 kwenye maeneo aliyopita kufanya kampeni.

Tathmini hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Katibu wa Hamasa, Sera, Utafiti na Mawasiliano wa UVCCM, Egla Mamoto kuwa baada ya Dk. Magufuli kuzunguka katika maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya kufanya kampeni CCM imezidi kukubalika zaidi kwa wananchi.

“Wiki mbili zilizopita utafiti wetu ulionesha CCM inakubalika asilimia 78, lakini baada ya Magufuli kuanza kuzunguka maeneo mbalimbali CCM imekubalika kwa asilimia 85, hii imechangiwa na mambo mengi ukiachilia mbali rekodi nzuri ya uadilifu na uchapakazi wa mgombea wetu,” alisema.

Alisema kilichosababisha tathmini hiyo kupanda ni kutokana na ilani ya uchaguzi mwaka huu na uwezo mkubwa wa Dk. Magufuli katika kutoa suluhu ya matatizo yanayowakabili wananchi.

Mamoto alisema hadi sasa Dk. Magufuli ametembelea mikoa sita ambayo ni Mbeya, Ruvuma, Njombe, Katavi, Rukwa na Mtwara pamoja na majimbo yote yaliyopo katika mikoa katika kampeni ya kuomba wananchi wamchague Oktoba 25, mwaka huu.

Alisema katika mikoa hiyo aliweza kufanya mikutano ya hadhara zaidi ya 49 na mikutano 126 ya barabarani ambayo wananchi walikuwa wakimsimamisha ili wamsalimie na kumueleza matatizo yao.

“Maeneo yote hayo amezunguka kwa kutumia mitumbwi, gari na kutembea kwa miguu kwa zaidi ya kilometa 5,900 na bado matazunguka na kutembea mikoa yote na majimbo yote,” alisema.

Lowassa kaingia mitini

Katika hatua nyingine, Mamoto alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ilitoa ratiba ili kila mgombea kuwafikia wananchi na kunadai sera zao, lakini baadhi ya wagombea wamekuwa wakienda kinyume cha ratiba.

“Kwa mfano, Edward Lowassa ambaye ni mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ameshaanza kuonesha dalili za kuchoka ma kushindwa kufika katika maeneo aliyohitajika afanye mikutano,” alisema.

Katibu huyo alisema Lowassa alitakiwa afike Ludewa (Njombe) na Tunduru (Ruvuma), ambako wananchi walikwisanyika wakimsubiri wamsikilize sera zake lakini hakuonekana.

“Jambo hili limewaudhi wananchi wale na hakika wameapa kutompa kura maana amewadharau, kutokana na kitendo cha yeye kuchagua baadhi ya maeneo muhimu ambayo ndiyo atakayoyafikia tu.

“Hali hiyo imeanza kuwatia mashaka Watanzania kuwa ni mbaguzi, amekosa hoja za kuzisimamia baada ya wimbo wa ufisadi kupamba moto kila kona, ama amechoka au ni uoga uliyowaingia kuona dalili za kutokukubalika,” alidai.

Chadema

Pia, alisema tuhuma ambazo zinasambazwa nchi nzima kuwa wao ndiyo wanapanga vurugu kwa kuwachafua Chadema si za kweli.

“CCM ni chama ambacho kinaamini katika maadili, hivi sasa tunajikita katika kutafuta kura na si kukaa na kupanga kufanya vurugu,” alisema.

Alisema Chadema wasimtafute mchawi, mchawi wanao wao wenyewe, wao wakae wasubiri ushindi wa kishindo kutoka CCM na kwamba wanaosambaza taarifa hizo wapuuzwe.

Mamoto alisema udhaifu wa wapinzani ndiyo utakaowafanya washindwe katika uchaguzi huu, kwa sababu muda mwingi wanatumia kujitetea na kujisafisha badala ya kuzungumzia matatizo ya wananchi.

Mwito kwa Watanzania

Katibu huyo alitoa mwito kwa Watanzania kuwa waungane pamoja bila kutazama tofauti zao za udini, rangi na ukabila na kuwataka watu wanaowagawa mafisadi, wala rushwa na wanaoamini kuwa wanaweza kuwanunua Watanzania wawapuuze.

Ukawa

Katika hatua nyingine, vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) umesema utashinda kwa asilimia 80 katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema katika uchaguzi huo hakutakuwa na ushindi wa kupishana kwa asilimia moja au mbili kama ilivyozoeleka na badala yake umoja huo kupitia mgombea wao urais, Edward Lowassa watashinda kwa kishindo.

Mbatia alisema wameendelea kufanya uchunguzi katika kila mahali ambapo hadi sasa wagombea wao wamefika na kuona namna wanavyopokelewa. Alisema umoja huo umejipanga, umejiratibu, umesimamia na kuelekeza vizuri hivyo wana uhakika wa kushinda.

Kampeni

Akizungumzia kuhusu hali ya kampeni za vyama hivyo inayoendelea katika mikoa mbalimbalali nchini, alisema tangu walivyoanza kampeni zao na hali ya kupokelewa kwao kuna matumaini makubwa ya kufanya mabadiliko.

“Kwa namna tunavyopokelewa kuna matumaini makubwa ya kushinda na kufanya mabadiliko kwani kwa umoja wetu tumesimamia mabadiliko,” alisema.

Alisema hata kule ambako iliaminika ni ngome za CCM wamekubalika na kubainisha kuwa hiyo ni raundi ya kwanza, lakini vyama vingine vitegemee cheche kwani hizo ni rasharasha.

Mweyekiti huyo alisema mbali na mwanzo huo lakini wamejipanga kuhakikisha Ukawa wanazunguka mikoa yote kwa kugawanyika kuhakikisha wanamnadi mgombea wao na kutangaza sera na ilani yao.

Agenda

Mbatia alisema kuwa pamoja na kuzunguka katika mikoa mbalimbali nchini agenda yao kuu ni sauti ya umma na umoja wa katiba ya wananchi kwani wanahitaji Watanzania wapate katiba wanayoitaka na yenye maridhiano yao.

“Tutaondoa katiba hii iliyoundwa na muungano wa ASP na Tanu kandamizi na tutaleta katiba itakayobadilisha mfumo mzima wa katiba hii kwani maendeleo yanaletwa kwa kujenga mfumo ambao mtu hawezi kuuvunja,”alisema.

Alisema kuwa ilani na agenda yao kubwa ni kuwa na katiba mpya ya Tanzania.

Uchochezi

Akizungumzia hali ya vurugu zinazojitokeza na zilizojitokeza katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu, Mbatia alisema licha ya ukimya wao wanaona ni vema Serikali ikaona umuhimu wa kuangalia maslahi ya taifa na si ya chama.

“Kuna mambo hapa yametokea yanatia hasira, yanajenga chuki na kusababisha uchochezi katika imani za kidini, ukabila, ukanda, misingi ya itikadi katika vyama vya siasa na kutotenda haki katika kusimamia amani.

“Ndiyo kwanza uchaguzi umeanza sasa mambo haya tukiyaacha ukiangalia bado kuna siku nyingi hadi kuukaribia uchaguzi tunaweza kupata matatizo,” alisema.

Alisema katika hali iliyotokea Dar es Salaam juzi, vijana waliojitokeza kufanya vurugu kumpinga Lowassa huku wakijitambulisha kuwa ni vijana wa Chadema lakini cha kushangaza watu wema wamesema si wa chama hicho na badala yake ni vijana waliotengenezwa kufanya vurugu.

“Hali hii ni kama ile iliyojitokeza nchini Kenya kwa uchochezi ambapo mbali na nchi hiyo, pia katika nchi nyingi hali kama hii hutokea mara tu inapotokea chama tawala kinapoondoka madarakani,” alisema.

Hata hivyo, alisema kuwa licha ya uwepo wa matukio ya uchochezi lakini Jeshi la Polisi halichukulii hatua jambo ambalo linashangaza.

Alisema kutokana na matukio hayo hadi hivi sasa jopo la wanasheria katika umoja huo tayari wameanza kuchukua vielelezo hivyo kama ushahidi kwani mambo hayo si ya kufumbiwa macho kwani haijulikani kesho itatokea nini.

Pia aliongeza kuwa vitu vyote vinavyojitokeza katika kipindi hiki tayari wamefikisha Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Polisi lakini la kushangaza havichukuliwi hatua.

“Mfano Agosti 23 wakati CCM inazindua kampeni zake walimaliza saa moja kasoro lakini jana mgombea wetu wa ubunge Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema amezidisha dakika 6 tu amekamatwa jamani vitendo hivi vinaongeza chuki,” alisema.

Alisema vitendo hivyo vinakiuka sheria na haki za binadamu kwa kiasi kikubwa kutokana na kutawala kwa matusi, kashfa, udhalilishaji unaofanyika katika maeneo mbalimbali na hata vituo vya habari lakini bado havichukuliwi hatua.

Mbatia alisema jambo lingine ambalo waliwahi kuliripoto katika mamlaka husika ni pamoja na kuchanwa kwa mabango ya wagombea wao pamoja na kukamatwa kwa watu wanaobandika mabango katika Mkoa wa Iringa na kukataliwa kwa baadhi ya maeneo kutoyabandika.

Alisema pamoja na mambo hayo yote wasifikiri upole wao na ukimya wao lakini ikifika wakati watasema hapana wamechoka.

“Sisi tunaambia Watanzania wasifanye vurugu pamoja na kuwasimamia vizuri lakini ikifika mahali tutawaachia Watanzania wafanye uamuzi wao. Tayari tumeitaarifu NEC, na wanasheria wetu wanashughulikia mambo haya na tutayapeleka mahakamani,” alisema Mbatia.

Aliwataka Watanzania wasichoke na kwamba CCM itakapotangaza uchochezi, uvunjifu wa amani, chuki Ukawa utatangaza amani na kudumisha umoja.

Top Post Ad

Below Post Ad