KAMA kawaida yetu katika kolamu hii kuwaleta mastaa mbalimbali na kubananishwa na wasomaji wetu katika mambo tofauti yanayohusu maisha yao kiujumla, siku ya leo tunaye staa wa filamu Bongo, Aunt Ezekiel ambaye anafunguka mambo kedekede aliyoulizwa na mashabiki wake.
Msomaji: Naitwa Kuruthumu, napenda nije kuwa muigizaji mkubwa kama wewe, nifanyaje?.
Aunt: Nakushauri ujikite kwenye vikundi vya maigizo mpaka pale utakapokuwa fiti na kukubalika kwa waigizaji wakubwa, basi hapo utakuwa umepata chansi ya kutoka.
Msomaji: Umejipangaje kuwaelimisha vijana kuwa Ukawa siyo chama cha vijana kama wengi wanavyofikiri?.
Aunt: Siwezi kuliongelea hilo sababu mimi si Ukawa, nimeshatoka huko sera zao sikuzielewa.
Msomaji: Nakumbuka miaka ya nyuma ulikuwa na baa kubwa na ilikuwa inafanya biashara nzuri maeneo ya Kinondoni, kwa nini uliifunga na umeihamishia wapi? Nilikuwa mteja wako..
Aunt: Biashara huwa upepo unabadilika, kweli mwanzo ilikuwa inafanya vizuri baadaye nikaona haifanyi vizuri inanitia hasara nikaamua niachane nayo.
Msomaji: Dada Aunt, hivi mpaka sasa bado upo kwenye ndoa yako, nilisikia umepewa talaka ni kweli?.
Aunt: Sipendi kuongelea mambo ya ndoa yangu, tunajuana wenyewe mimi na mume wangu.
Msomaji: Hivi Aunt wakati unaigiza Miss Bongo kwenye lile tukio la kumtoroka Baba Haji, kwa nini ulitokomea na gari la watu moja kwa moja mpaka Mbezi, ulimaanisha nini?.
Aunt: Nilikuwa nimechoka halafu nalazimishwa kuendelea kuigiza ndiyo nikaona niondoke na gari lilikuwa langu si la watu.
Msomaji: Aunt hufikirii ipo siku mumeo atakusumbua urudi kwake na wewe ndiyo umeshazama kimalovee kwa Iyobo?.
Aunt: Sitaki kuliongelea hilo.
Msomaji: Kwa nini ulivyokuwa na mimba ulikuwa unaenda hospitali umejifunika uso?.
Aunt: Sikupenda kuona watu wananishangaa nilikuwa naona kero, ndiyo maana nikawa navaa ninja kuficha sura.
Msomaji: Napenda kujua kabila lako na jina la Cookie la mwanao lina maana gani?.
Aunt: Mimi ni Mnyakyusa kwa baba na mama ni Mhaya, jina la Cookie nililiona mtandaoni kwenye Google likanivutia baada ya kuangalia maana yake kuwa ni kitu kitamu, sababu nampenda mwanangu haniishi hamu muda wote nikaona nimpe jina hilo.
Msomaji: Kwa nini hutaki kumuonesha sura mwanao?.
Aunt: Sababu yeye siyo msanii hakuna ulazima wa kufanya hivyo, kumuanika mwanangu kwa sasa watu watatumia vibaya picha yake kwenye vyombo vya habari na mitandaoni kila mtu ataongea lake, nitaumia sana sitajisikia vizuri ndiyo maana namuacha akue kidogo, sifikirii kumuanika leo wala kesho.
Msomaji: Napenda kujua dini yako, je Moze akitaka kukuoa utabadili dini kama ulivyofanya kwa mumeo?.
Aunt: Mimi ni Muislamu na nimekulia dini zote mbili, baba Mkristo na mama ni Muislamu hivyo yote yanawezeka kwani kila jambo linapangwa na Mungu.
Msomaji: Hongera kwa kuitwa mama, hivi ni kweli ulihongwa gari na Buthelezi?.
Aunt: Aaa wapi hakuna kitu kama hicho, yeye alikuwa anauza magari akaniomba nimsaidie kutangaza biashara yake.
Msomaji: Jina la Gwantwa na Aunt yametokana na nini na wewe ni mtoto wa ngapi?.
Aunt: Jina la Gwantwa kwa kawaida ya kabila letu lazima upewe jina la kimila na nilipewa na bibi yangu lina maana ya mtoto wa Mungu kwa hiyo kule kwetu mimi ndiyo kama mama yao kimila na jina la Aunt baba yangu yeye yupo mwanaume peke yake, sasa dada zake walikuwa wanagombania kila mmoja aniite jina lake na katika kumaliza utata ndiyo ikabidi niitwe jina hilo kwa maana ya shangazi ili kuwaridhisha wote.
Msomaji: Kwa nini unapenda kuvaa nguo fupi, hata ulipokuwa na mimba ulikuwa unavaa hivyo?
Aunt: Tangu mdogo mama yangu alinizoesha mavazi hayo, kama nguo ndefu utotoni kwangu nakumbuka nilivaa siku moja nilipokuwa natimiza miaka 12 au 13 kama sikosei.
Msomaji: Unamuweka upande gani Moze ni mzazi mwenzio, mumeo mtarajiwa au mchepuko?.
Aunt: Moze ni mzazi mwenzangu na kuhusu ndoa siwezi kuongelea maamuzi hayo hutoka kwa mwanaume, ila kwa upande wangu nina malengo naye, nitamzalia watoto hata 8.
Msomaji: Ugomvi wenu na Wolper najua ni mambo ya uchaguzi, ukiisha mtasaidianaje kimaisha?
Aunt: Sina ugomvi na Wolper na wala siwezi kugombana naye, hayo ni mambo madogomadogo tu tunawekana sawa.
Chanzo: GPL