CCM inapenda kutoa taarifa ifuatayo kwa wanachama, wapenzi na washabiki wake na kwa umma Watanzania.
Tathmini ya Upigaji Kura
Kama tulivyoeleza jana, tumeridhishwa na amani na utulivu uliotawala katika sehemu kubwa ya nchi yetu wakati wa zoezi la upigaji kura. Licha ya changamoto zilizojitokeza, ambazo baadhi zimeshughulikiwa, kwa jinsi zoezi la kupiga na kuhesabu kura lilivyoendeshwa kwa uwazi, matokeo ya uchaguzi huu yatakuwa ni kielelezo cha utashi halisi wa Watanzania na kutakuwa hakuna sababu ya mtu yoyote kukataa matokeo.
Kupokea na Kutangaza Matokeo
Kipindi cha kupokea na kutangazwa matokeo ni muhimu kama ilivyo kipindi cha kampeni na siku ya kupiga kura. CCM inahimiza utulivu kwa wafuasi wake na wananchi kwa ujumla na kuziachia mamlaka husika zifanye kazi yake. Katika kipindi hiki, kazi za vyama ni kupokea matokeo na na kazi ya Tume ni kutangaza matokeo.
Tunasikitishwa na propaganda zinazoendeshwa na wapinzani wetu kuhusu matokeo ya uchaguzi. Tunaona matokeo yanayotangazwa na wafuasi wa vyama vya upinzani, hasa mitandaoni. Bahati nzuri, propaganda hizi zinakosa maarifa kiasi cha kutoa hata matokeo ya Ubunge katika majimbo ambayo uchaguzi wa Wabunge haukufanyika, mfano Handeni na Masasi.
Tunawataka wana-CCM wapuuze matokeo yanayotembezwa kwenye mitandao ya kijamii. Matokeo rasmi yatatolewa na Tume. Bahati mbaya sana, wenzetu wanatoa matokeo ya uongo mapema ili Tume ikitoa matokeo rasmi waseme wameibiwa kura na kutafuta kisingizio cha kuingia mitaani na kufanya vurugu.
Pia tunabaini jitihada na nguvu kubwa za wapinzani wetu kupeleka kilio chao kwa waandishi wa habari wa nje ya nchi pamoja na mataifa ya nje kwa ujumla. Wameajiri magwiji wa propaganda kutoka nje ya nchi kwa fedha nyingi kujenga taswira kwenye Jumuiya ya Kimataifa kwamba Tanzania ni kama nchi nyingine yoyote ya Kiafrika ambapo hakuna ustaarabu wala utaratibu wa kidemokrasia na Serikali hukandamiza watu wake.
Mkakati wao ni kuitaka Jumuiya ya Kimataifa itumie nguvu yake ya misaada kwa nchi yetu kulazimisha matokeo ambayo hayatokani na utashi wa Watanzania. CCM haitalikubali jambo hili.
Matokeo ya CCM
Kwa kuwa matokeo kwenye vituo vya kupigia kura matokeo yamebandikwa hadharani na Wasimamizi wa Vituo, na nakala kupewa mawakala wetu, kwa mujibu wa matokeo yaliyobandikwa vituoni , CCM hadi sasa imekwishapata majimbo 176 kati ya majimbo 264 katika mikoa kadhaa ambayo tumefanikiwa kujumlisha hadi sasa. Pia, hadi sasa, tumeweza kukomboa majimbo 11 ambayo yalikuwa upinzani katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Tunawaomba wana-CCM watulie, wasiwe na hofu, wawe na subira hadi Tume imalize kazi yake. Matokeo ya Urais, ambayo yanaendelea kutangazwa na Tume, hayana tofauti na mwenendo tunaouona katika kura za Ubunge.
Imetolewa:
January Makamba
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa
Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya CCM
26.10.2015