Jeshi la Polisi Zanzibar kwa kushirikiana na Jeshi la Wananchi (JWTZ), limefanikiwa kuteguwa bomu lilitegwa eneo la Mkunazini karibu na kituo cha polisi mjini Zanzibar.
Bomu hilo lilitegwa na watu wasiofahamika na jeshi la polisi lilipata taarifa ya kutegwa kwa bomu hilo kutoka kwa wasamaria wema.
Akizungumza na mwandishi wetu, Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Hamdani Omar Makame, alisema baada ya kupata taarifa kutoka kwa wananchi kuwa eneo hilo kuna kitu kimetegeshwa, jeshi la polisi lilifanya uchunguzi na kubaini kuwa ni bomu na kufanikiwa kulitegua kwa kuliripua ili kuepusha maafa.
“Ni kweli kulikuwa na kishindo kikubwa baada ya jeshi la polisi kuliripua bomu hilo lakini hakuna madhara yoyote yaliotokea,” alisema.
Aidha alisema kuwa jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi ili kubaini ni aina gani ya bomu lililotegwa na aliyefanya kitendo hicho.