Hivi Ndivyo Helikopta Ilivyomuua Shujaa Deo Filikunjombe...Mashuhuda Waelezea Kilichotokea

Chopa
Polisi na wananchi wakiwa eneo la tukio  baada ya Chopa kuteketea kwa moto.
AJALI ya chopa (helikopta) iliyotokea usiku wa kuamkia jana, Oktoba 16, 2015 katika Hifadhi ya Selous, eneo la Msolwa mkoani Morogoro, imeyakatisha maisha ya aliyekuwa Mbunge wa jimbo la ludewa, Mhe. Deo Filikunjombe (43), pamoja na watu wengine watatu waliokuwa ndani ya helikopta hiyo.
Deo-Filikunjombe
Deo Filikunjombe.
Kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa na Kamishna wa Oparesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja, Mhe. Filikunjombe aliyekuwa akitetea ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), alikuwa na watu wengine watatu kwenye helikopta hiyo, akiwemo rubani, Kepteni William Silaa ambaye ni baba wa Jerry Silaa, Vitalis Blanka Haule anayetajwa kuwa ndugu wa Filikunjombe na Egdi Mkwera, Ofisa Tawala wa Mkoa wa Tarime na mtaalam wa mifugo.
chopa 2
Chopa (helikopta) aliyokuwa akitumia Mbunge wa jimbo la ludewa, Mhe. Deo Filikunjombe (43).
Chagonja alieleza kuwa helikopta hiyo yenye namba za usajili, 5Y-DKK ilikuwa ikitokea jijini Dar es Salaam kuelekea kusini huku taarifa nyingine zikieleza kuwa ilikuwa ikielekea jimboni kwake, Ludewa kabla ya kupata hitilafu ya injini ikiwa angani, baadaye ikaanguka na kulipuka, ikisababisha eneo lote la ajali kugubikwa na vumbi na moshi mzito.
chopa
Deo Filikunjombe akiwa kwenye helkopta anayodaiwa kupata nayo ajali.
Habari zisizo rasmi zilizolifikia gazeti hili, zilieleza kuwa helikopta hiyo iliondoka jijini Dar es Salaam majira ya saa 9 alasiri. Kabla ya kuruka angani, vyanzo vyetu vinaeleza kuwa helikopta hiyo ilipata hitilafu ndogo za kiufundi ambazo hata hivyo zilirekebishwa na safari ikaanza bila matatizo.
“Ilipofika kwenye Hifadhi ya Selous, rubani aligundua kwamba kuna hitilafu kwenye injini, akawa anajaribu kutafuta sehemu ya kutua kwa dharura ndani ya hifadhi hiyo lakini kabla hilo halijatimia, helikopta ilipoteza mwelekeo kabla ya kudondoka na hatimaye kulipuka,” kilieleza chanzo chetu kwa sharti la kutotajwa jina gazetini.
12107262_10203566066031418_6703966378237878945_n (1)
...Wakiendelea kufanya uchunguzi eneo la tukio.
Habari nyingine zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii, zinaeleza kuwa helikopta hiyo ilianza kuwaka moto ikiwa angani kabla ya kuanguka kandokando ya Mto Ruaha unaopita ndani ya hifadhi hiyo ambapo baadhi ya maoni yalidai huwenda chopa hiyo ilihujumiwa na hivyo kutaka uchunguzi zaidi. 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu usiku wa kuamkia jana, aliandika kuhusu ajali hiyo kupitia mitandao ya kijamii ambapo alieleza kupata taarifa kutoka kwa askari wa wanyamapori ndani ya hifadhi hiyo kubwa kuliko zote nchini Tanzania na kueleza hatua zilizochukuliwa:
“Mashuhuda wa ajali ya helikopta iliyotokea Selous walikuwa kitalu R2 na walishuhudia ikianguka na kulipuka ng’ambo ya Mto Ruaha Kitalu R3, maafisa na askari wanaelekea eneo la tukio kutokea Msolwa na Matambwe na tumeagiza vikosi vilivyo kwenye doria Selous kushiriki uokoaji.”
Habari zaidi kutoka vyanzo vyetu, zinaeleza kuwa kutokanana jografia ya eneo ajali hiyo ilipotokea, iliwachukua muda mrefu maafisa usalama na askari kufika eneo hilo, kutokana na ugumu waliokutana nao kuvuka Mto Ruaha hasa wakati huo wa usiku. Hata hivyo, askari na maafisa hao waliendelea kuhangaika usiku kucha mpaka siku iliyofuatia (jana Ijumaa), walipofanikiwa kufika eneo la tukio lakini tayari walikuwa wamechelewa kwani Mhe. Filikunjombe, Kepteni Silaa na wenzao wawili, tayari walishakata roho.
Naye Jerry Silaa, Meya wa Manispaa ya Ilala ambaye pia ni mtoto wa rubani wa helikopta hiyo, jana mchana aliandika kupitia ukurasa wake wa Instagram: “Kwa masikitiko makubwa nimepokea taarifa rasmi kutoka kwa timu ya uokoaji iliyofanikiwa kufika eneo la ajali na kukuta abiria wote na rubani wamepoteza maisha.
12065789_952647898130144_658653796879178835_n (1)
Kifo cha Filikunjombe, kimetokea siku 9 kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania na muda mfupi baada ya vifo vya wanasiasa wengine wawili, aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda na Dk. Emanuel Makaidi, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha NLD na Mwenyekiti Mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Baadhi ya wananchi wa gazeti hili waliopata nafasi ya kutoa maoni yao kufuatia mfululizo huo wa vifo vya viongozi wa kisiasa, walionesha wasiwasi mkubwa na kuhoji kinachoendelea nchini huku wengine wakihisi ni mambo ya kafara.
Enzi za uhai wake, ukiachilia mbali ubunge, Mhe. Deo Filikunjombe alipata kuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) iliyosimamia kidete sakata la ufisadi wa Escrow na kusababisha viongozi kadhaa wakubwa serikalini kung’oka kwenye nyadhifa zao. Mungu azilaze roho za marehemu wote mahalipema peponi, Amen!

Source:GPL

Top Post Ad

Below Post Ad