Polisi nchini Ujerumani wameonya wazazi dhidi ya kuweka picha za watoto wao hadharani katika mtandao wa kijamii wa Facebook.
Katika ujumbe kwenye ukurasa wao wa Facebook, polisi wa eneo la Hagen wametahadharisha wazazi kuwa picha hizo zinaweza kunakiliwa au kubadilishwa na kutumiwa vibaya na watu wanaovutiwa kimapenzi na watoto.
Aidha, watoto wahusika huenda wasipendezwe na picha hizo kuwa wazi mitandaoni watakapokomaa na kuwa watu wazima.
Wazazi wameshauriwa kuhakikisha kuwa picha hizo, ikilazimu, zinatazamwa na marafiki zao pekee na si kila mtu mtandaoni.
Ushauri huo wa polisi hao umeenezwa sana mtandaoni na kuvutia hisia mseto.
Afisa msemaji wa Polisi wa Hagen ameiambia BBC kwamba walishangazwa na jinsi ujumbe huo wa tahadhari ulivyopokelewa.
Amesema wanakadiria kuwa umesomwa na watu zaidi ya milioni 12.
"Tunataka kuwaambia watumiaji wote wa mitandao ya kijamii kwamba ni muhimu kuwa makini na kila kitu wanafanya kwenye mtandao," amesema Hanki Ulrich .
"Ni bora kufikiria mara mbili - mtandao hausahau kamwe "
Bw Hanki ameongeza kuwa ujumbe huo haujaongozwa na matukio yoyote mapya ya kesi za uhalifu au watu wanaovutiwa na watoto kimapenzi huko Hagen.
Picha zilizobadilishwa
Shirika la kujitolea linalohusika na ulinzi wa watoto NSPCC katika taarifa yao wamesema: " Wazazi wote wanapaswa kujisikia huru na kufurahia kuchukua picha za watoto wao na kushirikiana nao na marafiki na familia. Hata hivyo, tunapaswa wote kuwa makini wakati wa kuziweka picha hizo mitandaoni.
"Tunajua kwamba wahalifu wa ngono wana uwezo wa kubadilisha picha za watu wasiokuwa na hatia, na maendeleo katika programu za kuhariri picha zimefanya hili kuwa rahisi sana.
" Hivyo kama wazazi watachapisha picha za watoto wao kwenye mitandao, wanapaswa kuchukua hatua ili kuhakikisha kwamba wanachunguza hali yao ya faragha na kuhakikisha wanaridhishwa na watu watakaotazama picha hizo."
Shirika hilo limeongeza kuwa iwapo wazazi wana wasiwasi kuwa picha ya mtoto wao imeanguka mikononi mwa watu wabaya, wanapaswa kuwasiliana na Internet Watch Foundation, Child Exploitation na Online Protection Centre (Ceop) au kuwasililiana na NSPCC kupitia numbari ya msaada ya simu ya 0808 800 5000 ambapo watapokeza usaidizi.