John Magufuli, Edward Lowassa Waendeleza Tambo..Kila Mmoja Adai Atashinda...

By Waandishi Wetu, Mwananchi
Dar/mikoani. Wagombea urais jana walikuwa miongoni mwa mamilioni ya Watanzania waliojitokeza kupiga kura, huku Dk John Magufuli wa CCM na Edward Lowassa wakiendeleza tambo za ushindi.

Baadhi ya wagombea urais walitumia haki yao ya kidemokrasia nyumbani kwao na waliobaki wapiga kura jijini Dar es Salaam.

Wakati mgombea wa CCM, Dk John Magufuli akipiga kura katika kituo cha Shule ya Msingi Magufuli, Kata ya Muungano mkoani Geita, mgombea wa Chadema anayeungwa mkono na Ukawa, Edward Lowassa alikuwa jimboni kwake Monduli.

Mgombea wa ACT-Wazalendo, Anna Mghwira alipiga kura katika kituo cha Shule ya Msingi Kibaoni mkoani Singida, huku Hashim Rungwe wa Chaumma alipiga kituo cha Shule ya Msingi Ushindi, Mikocheni B, jijini Dar es Salaam.

Fahmi Dovutwa alipiga kura eneo la Kagera, Magomeni jijini Dar es Salaam, Jankeni Kasambala wa NRA (Minazi Mirefu, KIwalani), Chief Yemba wa ADC (Buguruni), na Macmillan Lyimo TLP aliyepiga kura kituo cha Njiapanda, Vunjo baada ya kutokea sintofahamu ya kitambulisho chake cha mpigakura.

Magufuli Chato

Baada ya kupiga kura, Dk Magufuli aliwataka Watanzania kumtanguliza Mungu kwa kila jambo kwa kuwa yeye ndiye muweza wa kila kitu na kuwasisitiza kuendelea kuilinda na kuitunza amani ya nchi.

Magufuli aliyeongozana na mkuu wa mkoa wa Geita, Fatma Mwasa, mkuu wa wilaya ya Chato, Shaban Ntarambe na kamanda wa polisi wa mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo, alisema anaamini ana baraka za Mungu kutokana na kuanza kuonyesha baada ya kumaliza kupiga kura.

Kwa mujibu wa Ofisa uchaguzi jimbo la Chato, Gaston Misungwi, wananchi 186,688 wamejiandikisha kupiga kura kati yao wanawake ni 94,056 na wanaume ni 92,832 huku vituo vya kupigia kura ni 521.

Lowassa: Nitashinda

Mjini Monduli, Lowassa baada ya kupiga kura kituo cha Ngarashi, Monduli alisema ana uhakika atashinda uchaguzi na hatakubali matokeo kama kutakuwapo wizi wa kura.

Hata hivyo, alisema upigaji kura ulikuwa unakwenda vizuri katika maeneo mengi ya nchi. “Nina uhakika wa kushinda kama uchaguzi ni huru na haki na sitakubali matokeo iwapo hautakuwa huru wala haki,” alisema Lowassa aliyeambatana na mkewe Regina.

Mgombea mwenza wa Lowassa, Juma Duni Haji alipiga kura kituo cha Bwawani saa 5:30 asubuhi.

Maalim Seif

Kwa upande wake, mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF, Maalim Seif Shariff Hamad alisema ni Mungu pekee yake anayefahamu kitakachotokea Zanzibar ikiwa uchaguzi hautakuwa huru na haki.

Alisema hayo baada ya kuulizwa nini hatima ya Zanzibar ikiwa uchaguzi huo hautakuwa huru na haki.

“Kama nikishindwa katika uchaguzi ambao ni huru na haki nitampongeza aliyeshinda, lakini kama nitashindwa na uchaguzi ambao si huru na haki, sitakubali matokeo,” alisema Maalim.

Maalim Seif alisema hayo jana baada ya kupiga kura katika kituo Namba 13 cha Mtoni Kidatu, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Mgombea TLP ajichanganya

Katika hatua nyingine, mgombea urais wa TLP, Macmillan Lyimo jana alitoa maelezo yaliyojichanganya, awali akisema ameshindwa kupiga kura baada ya kwenda kituoni bila kitambulisho, lakini baadaye akatoa kauli nyingine tofauti.

Lyimo alifika kituo cha Ghala Njipanda saa 2:30 asubuhi na kutakiwa kujaza fomu maalumu kwa wagombea urais endapo mgombea anapiga kura tofauti na kituo alichojiandikishia.

Msimamizi msaidizi wa kituo hicho, Aliko Mkumbo alimkabidhi fomu hiyo na kumtaka aijaze na kisha ampe kitambulisho, ndipo Lyimo alipojipapasa na kugundua hakuwa nacho.

Kutokana na hali hiyo, msimamizi huyo alimweleza kuwa asingeweza kupiga kura bila kuwa na kitambulisho cha mpiga kura, na Lyimo aliafiki, akisema anakwenda kukitafuta.

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya kituo hicho, Lyimo alisema uamuzi wa msimamizi huyo ulikuwa ni sahihi na kwamba yeye alijiandikishia Dar es Salaam na sio jimbo la Vunjo.

Hata hivyo baadaye, Lyimo alibuka na kudai kuwa hakukuwa na fomu Namba 19 inayojazwa kwa mpigakura nje ya kituo alichojiandikisha, jambo ambalo NEC imeeleza kuwa ilikuwapo.

Baadaye mgombea huyo alipiga kura saa 6:00 mchana kwa kile alicholiambia gazeti hili kuwa ni baada ya kuitwa na msimamizi msaidizi wa uchaguzi kuwa fomu imepatikana.

Ajitetea aliifichia siri NEC

Baadaye Lyimo alisema si kweli kwamba hakuwa na kitambulisho cha mpigakura, bali alitaka kuifichia siri NEC kutokana na kutokuwapo fomu Namba 19.

“Nilitumia hekima tu kutoka pale, lakini inabidi niseme ukweli kwa vile tayari dunia nzima imeshajua sijapiga kura,” alisema.

Mgombea huyo alisema msimamizi msaidizi wa kituo hicho, amechukua namba yake ya simu kwamba pale watakapokuwa wameshapata fomu hiyo, wangemwita apige kura.

“Niko hotelini nasubiri waniite. Hii Tume imekaa kinamna namna. Kama mimi mgombea urais inakuwa hivi, watu wa kawaida inakuwaje? Wameniambia ‘we katulie mahali tutakuita’,” alisema.

Ilipofika saa 5:21 asubuhi, mgombea huyo alimpigia simu mwandishi wetu na kumjulisha kuwa tayari Tume wamemwambia aende kupiga kura kwa vile wameshapata fomu hiyo.

Lyimo alifika katika kituo hicho tena saa 5:50 na kwenda moja kwa moja kwa Msimamizi Msaidizi ambaye alimkabidhi fomu Namba 19 na kuijaza kisha kupewa karatasi ya kupigia kura.

Kura ya mlinzi

Kabla ya kupiga kura, kulitokea ubishani kati ya msimamizi msaidizi na Lyimo, baada ya msimamizi huyo kumzuia mlinzi wake ambaye ni polisi kupiga kura ya rais.

“Huyu ni sajini wa polisi, kwa nini asipige kura ya rais? Asipopewa fursa na mimi sitapiga kura,” alisema Lyimo hali iliyomfanya msimamizi huyo kuwasiliana kwa simu na mamlaka ya juu yake.

Hata hivyo, baada ya kuzungumza kwa simu, bado msimamizi huyo alishikilia msimamo kuwa maelekezo ni kwamba asingeweza kupiga kura lakini wakati huo, Lyimo tayari alikuwa amepiga kura.

Msimamizi wa Uchaguzi majimbo ya Vunjo na Moshi Vijijini, Fulgence Mponji alikanusha madai ya mgombea huyo kuwa katika kituo hicho hakikuwa na fomu Namba 19.

“Yeye hakujiandikishia Vunjo wala hakujiandikishia Mkoa wa Kilimanjaro. Utaratibu lazima ujaze fomu Namba 19, sasa yeye alipopewa aijaze akasema ooh ngojeni nakuja,” alisema.

Imeandikwa na Raymond Kaminyoge, Salma Said, Rehema Matowo, Daniel Mjema na Zephania Ubwani



Top Post Ad

Below Post Ad