MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete amesema tayari mgombea urais wa chama hicho, Dk John Magufuli ameshashinda uchaguzi.
Amesema hatua hiyo inatokana na sababu mbalimbali, lakini kubwa ni kwa mgombea huyo kuzunguka nchi nzima na kuwahakikishia wananchi, bila kupepesa macho, kwamba atapambana na rushwa na ufisadi huku wagombea wengine wakisita kuzungumzia rushwa.
Katika hatua nyingine, Dk Magufuli ametaja mambo manne atakayoanza nayo kuwa ni umasikini, tatizo la ajira, mapambano dhidi ya rushwa na amani.
Pia, aliwapa pole Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa na Rais Kikwete kwamba katika utawala wao, bila kujua waliwaweka madarakani mafisadi waliochelewesha maendeleo ya serikali zao.
Rais Kikwete na Magufuli waliyasema hayo katika viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam jana wakati wa mkutano wa kufunga kampeni za uchaguzi mkuu kwa Jiji hilo. Mkutano huo ulihudhuriwa na maelfu ya watu na viongozi mbalimbali wa CCM, Serikali na viongozi kutoka nje ya nchi.
Akimnadi Dk Magufuli, Rais Kikwete alisema kutokana na kampeni alizozifanya nchi nzima kwa gari, ni wazi kwamba mgombea huyo wa CCM ameshashinda uchaguzi huo. Alisema wagombea wengine pamoja na kutumia helikopta, lakini walishindwa kuzungumza majukwaani.
Alisema pamoja na kuelezea mambo mbalimbali atakayowafanyia wananchi kwa kila kundi, amekuwa mgombea pekee ambaye bila kupepesa macho amezungumza waziwazi azma yake ya kupambana na rushwa na kuwakabili mafisadi ili kuwatokomeza.
Alisema tangu kuanza kwa kampeni zake Dk Magufuli ametembea kilometa 46,000 nchi nzima, umbali aliosema umemwezesha kukutana na wananchi wengi vijijini. Alisema wakati yeye alipofanya kampeni mwaka 2005, alitembea kilometa 32,000 kwa gari na kuwa hoi katika siku za mwisho za kampeni.
Alisema pamoja na kuzungumzia rushwa, Dk Magufuli amezungumzia masuala mengine mengi kama kupambana na umasikini, ajira, amani, mikopo kwa wakulima, wavuvi na wafugaji, kushusha kodi kwa wafanyakazi, kufuta ada kuanzia darasa la kwanza hadi kidato na nne, lakini pia kuanzisha viwanda.
Akirejea taratibu zilizomwezesha Dk Magufuli kuteuliwa na chama hicho kugombea urais, Rais Kikwete alisema hakuna jipya lililofanyika katika kumpata mgombea huyo, badala yake ni taratibu zile zile zilizotumika mwaka 1995 kumpata Rais mstaafu Mkapa na mwaka 2005 alipoteuliwa yeye.
“Ni taratibu zilezile ndizo zilizotumika, hakuna utaratibu mpya. Katiba ya CCM inasema Kamati Kuu itapitisha majina ya watu wasiozidi watano na kuyapeleka kwenye Halmashauri Kuu, inaweza kuwa chini ya hapo lakini wasiozidi watano,” alisema Rais Kikwete akimjibu Kingunge Ngombale- Mwiru anayedai kupitia majukwaa ya Ukawa kuwa CCM ilikiuka taratibu.
Akizungumzia mikopo kwa wanafunzi, Rais Kikwete alisema ni faraja kuona kuwa Dk Magufuli amepania kukabiliana na usumbufu wanaokumbana nao.
Alisema wakati alipoingia madarakani mwaka 2005, alikuta Sh bilioni 40 tu zikitolewa kwa wanafunzi, huku wanafunzi 16,000 tu wakinufaika, na sasa Sh bilioni 350 zinatumika na kuwanufaisha wanafunzi 98,000.