Mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa amesema amejiandaa na yupo tayari kuwaongoza Watanzania akiwa rais wa awamu ya tano.
Akizungumza kwenye Uwanja wa Ruanda Nzovwe- Mbeya Mjini, Lowassa alisema: “Ninatosha, nitumeni kwa kura zenu… nipeni kura za kutosha niwatumikie.”
Lowassa ambaye alisema anasikia deko kutokana na wingi wa watu, alisema misamaha ya kodi kwa sasa ni Sh1.6 trilioni na kwamba atahitaji Sh1.3 trilioni kati ya hizo kwa ajili ya elimu itakayolipiwa na serikali kuanzia chekechea hadi chuo kikuu.
Pia, aliendelea kuwasisitizia wananchi, umuhimu wa kulinda kura zao baada ya kupiga hadi kitakapoeleweka.
“Wana Mbeya, kuna rafiki yangu aliniambia umeshinda, mwingine akasema huwezi kushinda kwa sababu wataiba kura. Mimi nasema nipeni kura nyingi hata wakiiba zitoshe, kaeni kituoni mpaka kieleweke, huu ni mwaka wa kuitoa CCM madarakani,” alisema Lowassa.
Lowassa aliueleza umma huo, kwamba kuna watu wanapita mitaani kutoa rushwa na kununua shahada za kura, lakini wasiwe na hofu nao.
“Wakikupa hizo hela, kula, akikupa laki tano, mwambie akupe milioni moja, akishakupa na akaendelea kukusumbua, mwambie asikusumbue hizo ni pesa za Lowassa.
“Mimi nataka mnitume nikawafanyie kazi, sina mchezo, nitaunda Serikali itakayofanya kazi kwa spidi ya 120 kwa saa,” alisema Lowassa.
LOWASSA: Najisikia Kudeka Ninapoyaona MAFURIKO Haya.........Nipeni Kura Za Kutosha Niwatumikie ila Msisahau Kulinda Kura Zenu
October 19, 2015
Tags