Mbowe Amshukia Rais Kikwete Kuhusu Idadi ya Wapiga Kura na Zuio la Wananchi Kulinda Kura Vituoni

Mwenyekiti  wa  Chadema, mh Freeman Mbowe  amemtaka Rais Kikwete kutovuruga amani ya nchi na badala yake   amemtaka aondoke  madarakani  na kuiacha  nchi ikiwa  salama.

Mbowe alitoa  kauli hiyo jana jioni  katika mkutano  wa kampeni uliofanyika Mbogwe, wilayani Geita.

Alisema Rais Kikwete  anatakiwa aondoke madarakani salama kama walivyofanya marais wenzake wastaafu.

“Rais Kikwete ameamua kuwa mpiga debe wa Magufuli (mgombea wa CCM), sasa mimi naomba nimjibu yeye kama mpiga debe na si rais,”alisema Mbowe.

Alisema Rais Kikwete ameamua kuwaaminisha  Watanzania kuwa wapiga kura wapo milioni 28 badala ya milioni 22 kama ilivyotangazwa na Tume ya Taifa ya Taifa ya Uchaguzi (Nec).

“Sasa nataka kumuuliza Rais Kikwete hao wapiga kura wengine milioni sita wametoka wapi?” alihoji Mbowe na kuongeza:

“Naomba kumwambia Rais Kikwete kuwa hii nchi si yake, hii nchi si ya CCM na hii nchi si ya familia yake...hii ni nchi ya Watanzania,” alisema.

Alisema hatua ya Rais Kikwete na CCM inayoungwa mkono na Nec kuwataka wananchi wapige kura na kuondoka vituoni haiwatendei haki Watanzania.

“Kikatiba Watanzania wana haki ya kulinda kura zao kwa sababu zile ni kura zao, nashangaa Rais Kikwete anawaambia watu waondoke,”alisema.

Mbowe, aliwaomba Watanzania wote kwenda kwenye vituo kwa ajili ya kupiga kura ikiwa ni pamoja na kuzilinda kura zao.

Pia alisema anashangazwa na kauli ya Rais Kikwete ya kuliagiza Jeshi la Polisi kuwaondoa wananchi kwa nguvu katika vituo vya kupigia kura.

“Hao askari walioagizwa na Rais Kikwete, nao wana watoto na familia zao, naomba nikwambie Rais Kikwete kuwa huwezi kuzuia mabadiliko. Zimebaki siku 11, Mungu atajibu maombi yetu...nawaambia wananchi nendeni mkapige kura kaeni mita 200 lindeni kura zetu,” alisema.

Akiwa  mjini Dodoma jana  wakati wa kilele cha Mwenge wa Uhuru kilichoenda sanjari na kumbukumbu ya miaka 16 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rais  Kikwete  alitaja  idadi  kubwa  ya  wapiga  kura  kuliko  iliyotolewa  na Tume  ya  Taifa  ya  Uchaguzi.

Hata  hivyo, jana  jioni  Ikulu  ililitolea  ufafanuzi  suala  hilo  na  kudai  kuwa  idadi  kamili  ya  wapiga  kura  ni  milioni 22  na  si  vinginevyo.

"..... Katika Kilele cha mbio za mwenge wa uhuru , kumbukumbu ya Baba wa Taifa , Mwalimu JULIUS Nyerere na wiki ya vijana Kitaifa, Rais  Jakaya Mrisho Kikwete katika hotuba yake amezungumzia idadi ya watu waliojiandikisha kupiga kura.

"Kwa uhakika amesema kuwa idadi ya wapiga kura ni 22,751, 292 kwa upande wa Bara na 503,193 wa Zanzibar.  Hii ndiyo idadi kamili ambayo imo kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais na hii ndiyo idadi kamili kama ilivyotolewa na Tume ya Uchaguzi Tanzania.."  Ilisema  Sehemu  ya  Tamko  hilo  la  Ikulu  jana.
Tags

Top Post Ad

Below Post Ad