Ili kuondoa shaka miongoni mwa wananchi kutokana na tetesi zinazosambazwa juu ya ubora wa kalamu za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu Damian Lubuva amesema kila mtu anaruhusiwa kuja na kalamu yake kupigia kura Oktoba 25, mwaka huu.
Kauli hiyo imetolewa leo na NEC wakati ilipofanya mkutano wake na wahariri wa vyombo vya habari nchini ikiwa ni siku ya tatu ya kukamilisha utaratibu wa kuzungumza na wadau wa uchaguzi baada ya kufanya hivyo kwa wawakilishi wa walemavu na wamiliki wa vyombo vya habari nchini.
Akisisitiza juu ya ushiriki wa wadau kutoa elimu ya mpiga kura, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Lubuva amesema kipindi hiki cha kampeni kimeshuhudia kuzuka kwa maneno mengi yasiyokuwa na uhakika ambayo yanawachanganya wananchi.
“Kalamu yoyote inaruhusiwa kupigia kura hivyo watu wasiogope kwenda na kalamu zao ila wasiokuwa nazo watatumia zetu tulizoziandaa. Hazifutiki kama inavyosemwa huko mitaani,” amesema Jaji Lubuva.
Ametumia nafasi hiyo pia kubainisha mkakati wa kuzuia uwezekano wowote wa wizi wa kura kama inavyosemwa na baadhi ya wagombea na viongozi wa vyama vya siasa na kutoa wito kwa mtu au taasisi yoyote inayoona mwanya wa hilo kujitokeza ili hatua stahiki zichukuliwe.
Vile vile amewataka wanasiasa wote kuachana na maneno machafu wawapo majukwaani pamoja na kushambulia tume hiyo au baina ya wenyewe kwa wenyewe na badala yake wajikite kwenye kunadi sera zao.
“Tunaumizwa sana na matumizi ya maneno kama ‘tume inaandaa bao la mkono’ kwenye vyombo vyenu. Hakutakuwa na wizi na sisi tunaamini ushindi utatokana na wingi wa kura alizopata mgombea husika,” amesema na kuongeza:
“Kama chama cha siasa kimeishiwa sera za kunadi kwa wananchi basi ni vyema kikampumzisha mgombea wake na kusubiri siku ya uchaguzi badala ya kutoa lugha zisizofaa. Matumizi ya kauli za matusi, dhihaka au kejeli dhihi ya wagombea wengine ni kinyume na maadili ya uchaguzi. Hata kuituhumu tume bila kutoa ushahidi siyo jambo jema na kutowatendea haki wananchi.”
Mwenyekiti huyo ametoa kauli hizo baada ya kupata michango kutoka kwa wahariri waliomueleza changamoto walizonazo katika kuruhusu matumizi ya baadhi ya maneno yanayotolewa majukwaani.