Ninachokiona; Serikali ya Magufuli Inayokuja na Shaka iliyopo...

Ndugu zangu,
Naziona kila dalili, na nimelisema hili zaidi ya mwezi mmoja uliopita, kuwa mgombea urais wa CCM, John Pombe Magufuli ndiye atakayeunda Serikali ijayo ya Awamu ya Tano. Na sasa naiona pia shaka moja kubwa katika utawala ujao wa John Magufuli. Ni shaka ya kweli na naamini ndiyo kimsingi imetufikisha hapa tulipo leo.

Kwenye kampeni zake, John Magufuli amefaulu kuibeba ajenda ya kupambana na rushwa na ufisadi. Kupambana na watendaji wazembe. Kati ya nyingi, ukweli hizo ndio kero kubwa za Watanzania. Ni bahati mbaya kwa UKAWA ikiongozwa na Chadema, kuwa hii ndio ilikuwa ajenda yao waliyoibeba huko nyuma , nayo ikawabeba kisiasa. Wameipoteza, hivyo kupoteza pia dira kisiasa. Zikiwa zimebaki siku nne tu kabla ya Watanzania kupiga kura, ni miujiza tu ya kisiasa itakayopelekea Ukawa waliopoteana kurudi kwenye reli kuu na kupewa na wapiga kura, dhamana ya kuunda Serikali.
Na kwa hakika, ujio wa John Magufuli utaambatana na matarijio makubwa ya umma juu yake. Shaka kuu inajengwa na swali la je, atakidhi matarajio hayo katika mazingira ambayo yamepelekea Chama chake kuwa mbali na wanyonge kwa kukubali wafanyabiashara kuwa karibu sana na chama, na pengine hata baadhi ya viongozi wa dini ? Na bahati mbaya umma hautataka kusubiri mwezi mmoja upite, utataka kusikia kwa kauli na matendo utekelezaji wa yale ambayo John Magufuli amekuwa akiyahubiri kwenye majukwaa ya kampeni.

John Magufuli anayekuja, atakuwa na nafasi ya kipekee inayofanana na ya Mwalimu Nyerere kwa kuweka rekodi ya kuingia madarakani kwa kufanya kampeni ambazo hazikuhusisha sana matumizi makubwa ya fedha ambayo mara nyingi huambatana na michango ya wafanyabiashara wakubwa. Hivyo, John Magufuli hatakuwa na wadeni wake wa kuwalipa fadhila, isipokuwa, kuwahakikishia wafanyabiashara hao, uwepo wa mazingira mazuri ya kufanya biashara zao na walipe kodi ili zisaidie maendeleo ya wananchi wengine walio wengi. Kuna haja ya kutenganisha biashara na siasa, kuwa hata watendaji wakiwamo mawaziri, mbali ya Magufuli kuwasainisha mikataba, lakini umma ungetaka pia kwenye mikataba hiyo mawaziri na watendaji wakuu wawe tayari kutenganisha uongozi wa kisiasa/utendaji wa kiserikali na shughuli zao za kibiashara.

Na kwa kweli hili za kampeni za urais kuchangiwa na wafanyabiashara wakubwa lina mifano hai ya athari hata kwa wenzetu walioendelea kidemokrasia mfano wa Marekani.
Kwenye kampeni za kuwania Urais wa Marekani mwaka 1996, ambapo, mbali ya Bill Clinton kupambana na George Bush ( Baba) alikuwepo mgombea binafsi bilionea Ross Perrot aliyegharamia kampeni za urais wake kwa fedha za mfukoni mwake. Wamarekani hawakuwa tayari kutawaliwa na Rais bilionea Ross Perrot, na pamoja na ushindi wa Bill Clinton, Wamarekani walitilia shaka pia michango aliyopewa Bill Clinton na wafanyabiashara wakihofia kuwa wafanyabiashara hao wangenufaika zaidi kwa misamaha ya kodi. Katika hili, Bill Clinton mwenyewe, mwaka ule wa 1996, alikiri udhaifu huo kwa kutamka;

" Mistakes were made in raising money for my re-election campaign, but contributors did not buy influence with me and the system is not corrupt.." ( Mwandishi, The Guardian, Juni 30, 1996)
Tafsiri hapo ni kuwa, Clinton alikiri kuwa makosa yalifanyika katika kuchangisha fedha kumwezesha kushinda awamu ya pili ya urais, lakini, wachangiaji wa fedha hawakuweza kununua ushawishi kwake na kwamba mfumo haujaathirika na rushwa/ufisadi.
Kimsingi, katika nchi zetu hizi, hatari ya Rais na chama cha siasa kutokuwa na mipaka inayoonekana wazi yenye kutenganisha siasa na biashara, ina matokeo ya rais aliye madarakani na chama husika, kuwa mbali na wanyonge walio wengi.

Kuna wakati, akiwa madarakani, Benjamin Mkapa aliwaambia wazi wana CCM wenzake kule Dodoma, kuwa kihistoria, TANU na CCM imekuwa kimbilio la wanyonge. Mkapa akabainisha, kuwa CCM ya sasa inakimbiliwa na wafanyabiashara. Hili ni kosa la kisiasa.
Na nilipata kuandika, kuwa kama Chama Cha Mapinduzi kina nia ya kupunguza kupotea kwa imani ya umma kwa chama hicho, basi, kutahitajika, si tu kufanyika mabadiliko makubwa ndani ya muundo wa Serikali na uongozi wa Chama Cha Mapinduzi, bali kufanyika kwa mabadiliko makubwa yenye kishindo. Moja ya matarajio ya umma sasa, sio tu Wana-CCM, ni kuwa kwenye urais wake, John Magufuli ataongoza mabadiliko hayo makubwa na ya kishindo.

Kuna watakaopuuza, lakini, ni ukweli, kuwa tuhuma za ufisadi zimekipaka matope mno Chama Cha Mapinduzi. Kwenye macho ya umma, chama hicho kimechafuliwa na tuhuma hizo za ufisadi. John Magufuli ni ' kofia mpya' kiutawala. Jumapili ijayo, kwa hali ilivyo sasa, Watanzania watakwenda kuchagua ' Kofia Mpya'. Hivyo, watakuwa na matarajio makubwa yanayoweza kugeuka anguko kuu la Magufuli na CCM kwa chaguzi zijazo, kama Magufuli asipotimiza matarajio hayo.

Na matokeo ya uchaguzi wa mwaka huu yawe ni fundisho kwa chama tawala. Kama CCM itataka kubaki kwenye mioyo ya Watanzania wengi, kuwa na uhalali wa kubaki madarakani, basi, ina lazima ya kujipambanua kwa vitendo kutoka kwenye yote makubwa yenye kuhusiana na ufisadi na maovu mengine. Ibaki kuwa kimbilio la wanyonge. Isifike mahali, chama kikajikuta katikati ya mgogoro na umma. Hilo laweza kuharakisha mazishi ya chama hicho, yasiyo na kisomo.
Maggid,
Iringa.

Top Post Ad

Below Post Ad