Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad amesema hakubaliani na maamuzi ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kufuta matokeo yote ya uchaguzi na kuahirisha uchaguzi huo.
Akizungumza jana na wanahabari makao makuu ya chama hicho, Mtendeni, Maalim Seif alisema wamepata taarifa kwamba uchaguzi huo umeahirishwa kutokana na kuwa haukuwa haki jambo ambalo anasema kuna njama zinazofanywa na sio kweli kama uchaguzi huo haukuwa wa haki.
“Tunatamka wazi kwamba CUF hatuutambui uamuzi huo binafsi wa Mwenyekiti wa Tume na tunaitaka Serikali na CCM kuiacha Tume iendelee na kazi yake ya uhakiki wa matokeo ya uchaguzi na kisha kutangaza mshindi,” Alisema Maalim Seif.
Maalim alisema mwenyekiti hana mamlaka ya kufuta matokeo bila ya kuwashirikisha makamishna wake ambao ndani yake kuna makamishana kutoka chama cha wananchi CUF.
“Ametangaza mwenyewe binafsi bila ya kuwashirikisha makamishna wenzake wa Tume ya Uchaguzi, kwamba eti ameufuta uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 25 Oktoba, 2015” alisema Maalim.
Aidha Maalim Seif alieleza kushangazwa na mwenyekiti wa tume kutoonekana pamoja na mkurugenzi wake katika kituo kikuu cha kutangazia matokeo ambapo Jumatano ilikuwa ni siku ya mwisho kutangazwa mshindi.
“Mwenyekiti huyo amefanya hivyo baada ya kutoonekana tokea asubuhi katika kituo cha majumuisho ya matokeo ya uchaguzi wa Rais kilichopo Hoteli ya Bwawani. Mkurugenzi wa Uchaguzi, Salim Kassim Ali, naye hakuonekana tokea asubuhi na haijulikani yuko wapi,” aliongeza.
“CUF imeshtushwa na hatua hii inayokwenda kinyume na Katiba na Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar na inaichukulia kauli ya Mwenyekiti huyo ni yake binafsi hasa baada ya kujiridhisha kwamba hakukuwa na kikao chochote cha Tume kilichofikia maamuzi hayo. Mwenyekiti kwa nafasi yake hana mamlaka ya kufuta uchaguzi huo,” anasema Maalim Seif.
Kutokana na hatua hiyo, Maalim Seif anasema kuna njama ambazo zinafanywa kwa makusudi katika kuhujumu mchakato mzima wa uchaguzi.
“Inaonekana kuna njama za makusudi kutaka kuvuruga demokrasia ya Zanzibar na kuingiza nchi katika machafuko,” alisema mwanasiasa huyo.
Hata hivyo, Maalim Seif aliwaambia wandishi wa habari kwamba mwenyekiti huyo hakutafakari kwamba kuufuta uchaguzi mkuu wa Zanzibar kunaathiri pia uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu wapigakura walikuwa ni wale wale waliomo kwenye Daftari la Wapiga Kura la ZEC.
Katibu Mkuu huyo anasema wanatambua kwamba hatua hiyo imekuja baada ya majaribio yote ya kutaka kulazimisha ushindi usiokuwepo wa CCM kushindikana ambapo uhakiki wa matokeo ya uchaguzi wa majimbo yote 36 ya Unguja na majimbo 4 ya Pemba uliokuwa umekamilika kabla ya zoezi hilo kusitishwa umethibitisha matokeo ambayo CUF ilikuwa imeyakusanya.
Katika hatua nyingine, Maalim Seif ameziomba jumuiya za kimataifa na marafiki wa Tanzania kuingilia kati suala hili hasa kwa sababu waangalizi wa kimataifa wameshuhudia hatua zote hizi pamoja na uhakiki wa matokeo ulivyokuwa unakwenda.
Alisema CUF imeonekana wazi kwamba ni mshindi wa uchaguzi wa Rais pamoja na majimbo yote 18 ya Pemba na majimbo mengine tisa ya Unguja.
Seif aipinga ZEC Kufuta Matokeo...... Ataka jumuiya ya Kimataifa kuingilia kati
0
October 29, 2015
Tags