Juzi tumetangaziwa kamati ya ushindi itakayo hakikisha Stars inachomoka na ushindi katika mchezo ujao dhidi ya Algeria, mchezo ambao umechachawisha na kukurupisha akili za watu makini tunaowaamini.
Tumewahi kuwa na kamati za aina hii ambazo hazikusaidia chochote, kamati zilizosheheni watu wa mipango na wenye ushawishi mkubwa kwa Watanzania, pamoja na kuwa na wajumbe mahiri haikutimiza lengo lake. Leo hii inaundwa kamati ya ‘kisela’ na kuwapa ujumbe ‘washikaji’ na kutuaminisha wanaweza kuifanya kazi iliyo shindwa kufanywa na watu ‘wenye akili zao’.
Sijajua vigezo walivyotumia kuwapa ujumbe hawa ‘washkaji’ ambao kila siku wanahusika na timu
hii, sasa kama sio upuuzi ni nini? Upigaji au Mazingaombwe? Sasa kuna haja gani kuunda kamati ya ushindi ya wadau wa TFF ambao michango yako imeshindwa kusaidia timu? Watapata wapi mawazo mapya, connnection mpya na changamoto mpya? Hamuoni ni sawa na abiria kusukuma gari wakiwa ndani ya gari? Watalisogeza kwa miujiza gani?
Labda tuelezwe kamati hii ina dhima tofauti na kamati zilizopita, zilizoundwa na watu sahihi
kama aliyekuwa mbunge wa jimbo la Kigoma Kaskzani Mheshimiwa Zitto Kabwe, alikuwemo
pia Mkurugenzi wa Shirika la Hifadhi za jamii NSSF Dr. Ramadhan Dau, kamati iliyoundwa baada ya Taifa Stars kuifunga moja ya timu ngumu barani Afrika, timu ya Morroco kwa mabao 3-0, na baada ya ushindi huo mtamu tukaamini tumeshafuzu kombe la Dunia.
Lakini safari tuliyoitegemea na kuamini tumeshafika, tukawapa jukumu wadau hawa
wakubwa wenye uwezo kiushawishi na hata kifedha ili kushika usukani, tulijikuta gari inakata kona na kurudi Dar es Salaam. Sasa TFF haikumbuki au ni makusudi? Kuna faida gani ya kamati hii?
Moja ya kazi za kamati ya juzi ya ‘kisela’ ni hamasa kwa wachezaji na mashabiki, sasa tujiulize ni kweli tunahitaji kamati itufanye kazi hiyo? Wachezaji wanapewa hamasa na kamati? Na kuhusu mashabiki jamani tuna kitengo cha habari TFF ambacho mkuu wake wa Idara ni mjumbe wa kamati hii pia, rafiki yangu Baraka Kizuguto, sasa kama alishindwa kutumia nafasi yake kama mkuu wa Idara ataweza vipi kuitumia leo akiwa kwenye kamati? Huku sio kusukuma gari ukiwa ndani ya gari?
Kuwapa hamasa mashabiki ni kwanini TFF isishirikiane na media kufanya kazi hiyo? Kwanini TFF isipunguze au kuondoa viingilio katika michezo ya Taifa Stars? Mambo madogo haya ya kuamua mara moja mpaka kuwe na kamati? Hamasa haijengwi kwa maneno, fanya yanayooneka.
Dhima nyingine tutaambiwa ni ukusanyaji wa pesa. Hapa ndio nilipochoka kabisaa! Ni kweli
kwa sasa Taifa Stars udhamini wake haujitoshelezi mahitaji yake kiasi kwamba tunatakiwa tuwe na kamati ya kuitafutia pesa?
Kwa nini badala ya kuwa na kamati hii, Rais wa TFF Ndg. Jamal Malinzi asiimarishe kitengo cha masoko cha TFF ili kifanye kazi ya kiuweledi zaidi kutafuta co-sponsors (wadhamini pacha) wa Taifa Stars kitu ambacho ninaamini ni cha kudumu maana ukipata udhamini kwa miaka mitano unakuwa na uhakika wa kupata fedha za kuigharamia timu kwa miaka mitano na sio fedha ya kamati ambayo ni ya hisani na tutambue hisani hua inatoka pale tu timu inapofanya vyema, lakini ikiboronga kamati hua zinakufa ‘automatically’.
TFF irejee na ituambie tija iliyopatikana wakati ule ilipoundwa kamati ya kina Dr Ramadhan Dau
na kina Mh. Zitto, je lengo la Taifa stars lilifanikiwa? Hamasa ilikuwepo? Kwa bahati mbaya sana watu ambao wako mbali na TFF hudhani watu wa hizi kamati huwa wanatoa pesa zao mfukoni kuchangia timu hapo ndipo tunakosea, hizi kamati zitakwenda kutumia pesa za TFF imefika mahali hata vikundi vya kushangilia vinalipwa pesa na hata tiketi vingine vinapata, je hii ndio hamasa?
Huu ni nini kama siyo mpango wa upigaji na kuimomonyoa TFF? Mna sababu gani za kuungwa mkono na wadau wa soka la Tanzania? Hiyo haitoshi basi tuje na ‘vivid example’ nchi fulani imefanikiwa katika mashindano kwa kuwekeza kwenye kamati kama hizi.
Kila siku mwenyewe Malinzi anakiri Madagascar wanafanikiwa sasa hivi katika soka kwa kuwa wamewekeza katika soka la vijana wamewekeza katika ujenzi wa miundombinu ya soka, sasa kama tunaifahamu njia ya mafanikio kwanini hatutaki kufanya kama wenzetu wanaofanikiwa na badala yake sisi tunataka njia zetu za upigaji tu?
Wiki iliyopita kituo cha kulelea vipaji cha Kidongo Chekundu kimefunguliwa hatukuona coverage kubwa kupewa hicho kituo wala TFF haijatuambia itakitumiaje hicho kituo katika kuendeleza soka la vijana lakini kamati za ‘upigaji’ zinapewa covourage kubwa kwa kua zina watu wenye fedha na majina mjini, hapana sio kila kitu kina tija.
Tunahitaji Malinzi aje na mpango mkakati imara kwa ajili ya timu ya Taifa na sio hizi kamati za vipindi kama ‘tumbo la period’ kwa kina dada, Watanzania wanapenda mpira sana huhitaji kamati kuwapendesha, unachohitaji ni kuwaonesha tumaini katika kiwanda cha soka, ‘otherwise’ niwatakie upigaji mwema wa pesa za serikali ambazo tunaambiwa hazina macho, pia niwatakie magumashi mema na mzidi kula na sisi vipofu, lakini siku tukifumbua macho kama Bartholomayo mnatueleza nini mmefanya wakati tupo gizani.
Source: Shaffih Dauda