Usiri wa Mali Katika Ndoa ni Janga Pale Mmoja Anapofariki Ghafla

Wapendwa leo ningependa tujadili juu ya usiri wa mali katika ndoa,Katika jamii ambayo imenizunguka kwa mwaka huu tu nimepata kuona jambo hili likijitokeza mara tano katika misiba tofauti tofauti iliyotokea na mingine ikiwa ni ya ndugu zangu jamaa na marafiki, na katika misiba hiyo bahati mbaya yote inawahusu wanaume ambao wametangulia mbele ya haki huku wakiwa wameacha watoto pamoja na wake zao.

Mbaya zaidi katika familia hizo hakuna yoyote hata wake zao anayejua Mali za hao waume zao ziko wapi zaidi ya Nyumba wanazoishi walizoachiwa na marehemu,moja ya msiba ulionishangaza na kunisikitisha sana ni kuona rafiki ya marehemu anajua Mali nyingi karibu kila kitu cha marehemu alichoacha kuliko hata mkewe na la zaidi marehemu ana watoto wakubwa tu ambao angeweza kuwaambia au kuwashirikisha mambo yake.

Mwanaume na mwanamke wanapoamua kuungana nakuwa mwili mmoja ina maana wamekuwa ni wamoja ,chochote kinachopatikana kinakuwa ni mali ya wote, Ina maana mmeridhiana na kuaminiana na kuamua kukabidhiana maisha yenu kwa faida ya ninyi wote wawili,mtu ambaye umemkabidhi maisha yako unalala naye,anaujua undani wako ,ana usalama wa afya yako, amebeba dhamana ya maisha yako na uzao wako unamficha mali ulizonazo kweli? Hajui hata kama una au huna account bank? Sasa unatafuta kwaajili ya nani na ili iweje?

Basi kama mwanaume una hofu na mwanamke uliye naye basi weka Mali zako kimaandishi kuliko kuweka siri mwisho unaacha kizazi chako kikiteseka ili hali Mali zinapotea bure wanafaidi wengine ambao hata hawakuhusu. Na hiyo hofu inatoka wapi? Ili hali mwanaume wewe ndo kichwa cha Nyumba na mtawala Mkuu, ule utawala wa chini utaenda vile utawala wa juu uko,kama mwanamke amekuwa hajitambui au ana hila ni makosa ya mwanaume katika utawala wake. Tunajua upendo wa kweli ni utimilifu wa mambo yote, na katika Pendo Hamna hofu na huyo mwenye hofu hakukamilika katika Pendo.

Ni wito wangu wanandoa tuache usiri usio na tija,mshirikishe mkeo au mumeo kwa Mali ulizonazo,tuambiane kweli,mpaka mtu unaamua kuingia katika ndoa ina maana umeridhika na huyo uliyemchagua,usiri hauna maana yoyote zaidi ya kuwatesa tu watoto na kuwaacha katika mateso makubwa,hakuna mwenye dhamana ya maisha akajua anaondoka lini duniani,hatukuja na kitu duniani na hatutaondoka na kitu vyote tutaviacha.

Wanaume wafundisheni wake zenu kutafuta ili wajue kuheshimu na kuvitunza vile vinavyopatikana kwaajili ya familia,msiwafungie wake zenu majumbani mwenu kama mifugo matokeo yake Mungu anapowachukua mnawaacha wanateseka na watoto wenu maana walizoea kuletewa kila kitu,na wakati mwingine hata zile Mali mlizoziacha zinapotea maana zinakuwa hazina msimamizi tena kwasababu kila kitu kiliendeshwa na mwanaume.

Nawatakia ndoa zenye furaha,amani na baraka tele, Mwenyezi Mungu awe nanyi daima.karibuni wote kwa mjadala zaidi.

By everlenk/JF
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad