Baraza Kuu la Chama cha Wananchi (CUF), limekutana na kusisitiza kuwa hawatarudia uchaguzi wa Zanzibar.
Mkutano huo ulifanyika jana mjini hapa ambapo walijadili mkwamo wa kisiasa nchini na juhudi zinazoendelea katika kukabiliana na hali hiyo.
Naibu katibu mkuu wa CUF, Nassor Ahmed Mazrui alikaririwa akisema baada ya kikao hicho, “Wanaosema uchaguzi urejewe waachieni wenyewe, sisi katika CUF hakuna habari hiyo. Kwa sasa kutangaza matokeo ya uchaguzi ndiyo msimamo wetu, ili mshindi atangazwe na kuapishwa .” alisema Mazrui
Awali Kaimu Mwenyekiti wa Taifa wa CUF, Twaha Taslima akiwa na safu ya juu ya uongozi wa chama hicho, walisema kuna haja ya kuendelea kutafuta haki ya Wazanzibari kwa kuitaka Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kutangaza matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka huu, ili mshindi ajulikane na aweze kuapishwa.
Taslima alisema pia baraza hilo lilibariki juhudi za mgombea urais wa Zanzibar kupitia CUF akiungwa mkono na Ukawa, Maalim Seif Sharif Hamad kutafuta suluhisho la mkwamo huo baada ya Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha kufuta matokeo ya uchaguzi wa visiwani humo hatua iliyopingwa taasisi za ndani na za kimataifa.
Juhudi hizo ni pamoja na mazungumzo ya Maalim Seif na wanadiplomasia wakiwamo mabalozi mbalimbali waliopo nchini, yaliyofanyika katika Ofisi za Ubalozi wa Canada, Mtaa wa Mirambo Na. 50, jijini Dar es Salaam.
Aliongeza kuwa, Maalim Seif pia alizungumza faragha kwa saa moja na Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, Ikulu Dar es Salaam.
Katika juhudi hizo, Maalim Seif aliliarifu Baraza Kuu jinsi alivyoishawishi jumuiya ya kimataifa isimame pamoja na ukweli, kwamba kilichotendeka Zanzibar ni kupinduliwa kwa demokrasia hivyo kutaka wananchi wapewe haki yao.
“Tumesikia na kushuhudia kauli za mataifa zikishinikiza Serikali na hata utawala mpya ulioingia madarakani, katika Jamhuri ya Muungano kwamba maamuzi ya Wazanzibari yaheshimiwe kwa ZEC kumtangaza mshindi ili aweze kuapishwa,” alisema Maalim Seif. Huku akinukuu taarifa ya Pongezi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerr kwa Rais mpya Dk John Magufuli.
Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ambayo bado ipo katika muundo wa Umoja wa Kitaifa aliongeza kuwa , “Tunashukuru dunia nzima inatuunga mkono kwa jambo hili”.
Kabla ya kikao hicho kilichoanza saa 8.30 mchana kilitanguliwa na Kamati Tendaji ya Taifa ya CUF ambacho kilizungumzia uteuzi wa viti maalum katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Chanzo: Mwananchi
Baraza Kuu La CUF Lakataa Kurudia Uchaguzi Zanzibar!
2
November 08, 2015
Tags
Tanganyika wajinga kura wameibiwa kwanini hawakubari
ReplyDeleteWawape tuu nchi yao
ReplyDelete