CCM Watuhumiana kwa Unafiki Kila Kona Kwa Kushindwa Ubunge na Udiwani Baadhi ya Majimbo

Baada ya upepo wa Uchaguzi Mkuu kuanza kutulia, baadhi ya makada wa CCM wameanza kutuhumiana kuwa unafiki na hujuma zilizofanywa na baadhi ya wanancha wa chama hicho zimesababisha kishindwe kufanya vizuri katika baadhi ya maeneo kwa ngazi za udiwani na ubunge.

Baadhi ya makada hao kwa nyakati tofauti wamekuwa wakieleza kuwa CCM ina ‘wanafiki’ wengi ambao wanaangalia zaidi masilahi yao kuliko chama.

Hata Rais mteule, Dk John Magufuli amekuwa akizungumzia suala hilo tangu kipindi cha kampeni, akilalamika kuwa kuna watu waliokuwa naye mchana lakini usiku wanahamia Ukawa.

Dk Magufuli alipigilia msumari suala hilo alipozungumza na wafuasi waliojitokeza kumpokea katika ofisi ndogo za CCM, Lumumba baada ya kupatiwa cheti cha ushindi wa urais na Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC), akisema kuna haja ya kukijenga upya chama hicho kwa kuwaondoa wanafiki wote.

Dk Magufuli alimweleza mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete huku akimuomba radhi kwa maneno aliyoyazungumza kuwa akiona mnafiki amfukuze mara moja kwa kuwa hakuna sababu ya kuwa na makada wengi ambao ni wanafiki, ni bora kubaki na wachache waaminifu.

Nisiposema nitakuwa mnafiki, msema kweli ni mpenzi wa Mungu. Watubu wajirekebishe. Ni heri mara kumi kuwa na mpinzani kutoka nje kuliko ndani ya chama. Mipango yenu mtaipanga mchana usiku wataitoa nje, ni afadhali uwe na mchawi atakuroga ufe kuliko mtu mnafiki,” alisema Dk Magufuli.

Tuhuma za unafiki zimeendelea kutawala ndani ya chama hicho, aliyekuwa mgombea ubunge wa CCM Jimbo la Moshi Mjini, Davis Mosha juzi alitangaza kuachana na siasa akidai kuwa chama hicho kimejaa wanafiki waliochangia kuanguka kwake.

Mosha, ambaye alisema ataendelea na biashara zake badala ya kufanya siasa, alisema kushindwa kwake kulisababishwa na viongozi wa CCM kuanzia Serikali za Mitaa, kata, wilaya hadi mkoa ambao alidai kuwa waliweka mbele masilahi yao binafsi.

“Viongozi wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro ni ndumilakuwili na nia yao si ushindi kwa chama, bali wapo kimasilahi zaidi na hawana nia njema, ndio maana chama kinashindwa,” alisema Mosha alipokuwa akiwashukuru wakazi wa Moshi Mjini baada ya kumalizika kwa uchaguzi.

Mfululizo wa tuhuma za hujuma umeendelea katika maeneo mbalimbali nchini, huku baadhi ya wanachama wa chama hicho katika Jimbo la Iringa Mjini, wakimtuhumu Mwenyekiti wa chama hicho mkoani Iringa, Jesca Msambatavangu na viongozi wengine kwa kukihujumu chama hicho.

Wanachama hao, walishinikiza Msambatavangu, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Iringa Mjini (UVCCM), Kaunda Mwaipyana na Mwenyekiti wa UVCCM Kata ya Mkwawa, Salum Keita waachie ngazi au wachukuliwe hatua na chama kwa kusababisha kupoteza jimbo na kata 14.

Hata hivyo, Msambatavangu alikana tuhuma hizo na kuanisha kuwa kuna mambo mengi yaliyofanyika kinyume na utaratibu na kusababisha jimbo hilo kupotea kwa mara nyingine na kata 14.

Hali hiyo imejitokeza pia wilayani Kilombero ambako baadhi ya wanachama wa CCM wamewataka viongozi wao wa wilaya kung’atuka ndani ya siku 21 kuanzia jana, wakiwatuhumu kusababisha kupoteza majimbo mawili ya Mlimba na Kilombero ambayo yamechukuliwa na Chadema.

Wanachama hao 16 walioongozwa na Dismas Lyassa, walisema dalili za kuanguka kwa chama hicho zilianza kuonekana mapema wakati wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa Desemba, mwaka jana, lakini hakuna hatua za dhati zilizochukuliwa.

Jambo hilo limezidi kuwakera wengi kiasi cha kuwafanya wanachama wasiopungua 400 wa UVCCM Jimbo la Babati Mjini mkoani Manyara, kufanya maandamano juzi hadi ofisi ya CCM mkoa wakiwatuhumu baadhi ya viongozi wa wilaya kuhujumu uchaguzi na kusababisha jimbo hilo kuchukuliwa na Chadema.

Vijana hao wakiwa na mabango yaliyokuwa na maandishi yaliyokuwa yakiwatuhumu viongozi wanane wa juu wa chama hicho, waliandamana na kupokelewa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Manyara, Lucas Ole Mukus.

Miongoni mwa waandamanaji hao, Steven Kairo alisema madai hayo yakithibitishwa, watuhumiwa wote wafukuzwe uanachama.

Alisema kama viongozi hawatayafanyia kazi madai yao, wao watakuwa wa kwanza kurudisha kadi.

Tumehangaika kuusaka ushindi wa CCM Babati Mjini, lakini ndumilakuwili wakatuangusha, tunaomba mbariki ombi letu la kuwawajibisha viongozi hao, watupishe, hata sisi tunaweza kuongoza,” alisema Kairo.
Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Wasenge hao tangu mwenyekiti wao Kunchu

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad