Kafulila Aibuka Kupinga Matokeo ya Mwilima..Adai CCM ilimpora Kura

Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini(NCCR-Mageuzi), David Kafulila ametangaza rasmi kwenda mahakamani siku yoyote kuanzia sasa ili kudai haki yake baada ya Msimamizi wa Uchaguzi(Nec),katika Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza Ruben Mfune kumtangaza Hasna Mwilima wa CCM kuwa mshindi.

Kupitia uchaguzi uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu, Mfune alimtangaza Hasna kuwa Mbunge wa jimbo hilo kwa madai ya kupata kura 34,453 akifuatiwa na Kafulila aliyedai kupata kura 33,382 lakini alipingana na matokeo hayo akibainisha kuhujumiwa.

Akizungumza jana na waandishi wa habari jijini hapa, Kafulila aliyekuwa mbunge kinara katika kuibua ufisadi wa sakata la Escrow alisema matokeo halisi yaliyokusanywa kwenye kituo ni tofauti na matokeo aliyoyatangaza msimamizi huyo.

“Nitakwenda kufungua kesi katika Mahakama Kanda maalumu ya Tabora kanzia wiki ijayo, kwa sasa tunaandaa utaratibu na wanasheria wangu kabla ya kufungua kesi,najua nitashinda na haki yangu haitapotea ...madai ya kesi ni kuitaka mahakama itangaze mshindi wa matokeo halisi ya vituo vyote 382 katika Kata zote 16 za jimbo hilo,” alisema Kafulila.

Licha ya kudai mazingira ya kuhesabu kura za jimbo hilo kuwa na utata, alisema kura halisi alizopata ni 34, 149 dhidi ya mshindani wake Hasna aliyepata kura 32, 982 lakini alimtuhumu msimamizi huyo kupanga njama za kutangaza matokeo batili kwa madai ya kupata shinikizo la viongozi wake ngazi za juu.

“Kwenye kuhesabu matokeo kulikuwa na askari wasiopungua 400, wakuu wa wilaya, mkoa walikuwapo, tulitumia masaa 17 kutangaziwa matokeo na yalikatishwa mara kdhaa lakini bado nilifanikiwa kushinda jimbo hilo kwa kura nyingi.Nawaomba watanzania wasife moyo, bado nitapambana kuhakikisha haki yangu inapatikana,”alisema mgombea huyo aliyetumikia jimbo hilo tangu 2010 hadi 2015.

Hata hivyo, Msimamizi huyo wa uchaguzi, Mfune aliliambia gazeti hili kuwa endapo mgombea huyo atakuwa hajatendewa haki, afuate njia sahihi za kudai yake. Alisema kila mgombea anayo haki ya kulalamika endapo hataridhishwa na matokeo.

“Lakini matokeo niliyotangaza ndiyo matokeo halisi niliyoyaamini mimi, utaratibu wa kulalamika unafahamika.”

Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Kafulila umefulia, ulijifanya mjanja saana, ukadiriki kumsemea mbofumbofu mtu alosababisha uwe hapo Mh. Zito Kabwe,...sasa umeona?? Utakula jeuri yako, kamwombe radhi ZITO.........hapana chezeya ZITO weweeeeee.......NCCR magauni nyang'a nyang'a, mwenyekiti kawa ndio katibu mwenezi wa chadema ha ha ha......kavuta chake kwa 'mamvi' shwaaaari....

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad