Kamati ya Saida Taifa Stars ishinde imemaliza kazi na kuvunjwa rasmi jana, lakini nyuma yake imeacha maswali mengi kuliko majibu kuhusu utendaji na uhusiano wake na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Rais wa TFF, Jamal Malinzi aliunda kamati hiyo ili kuhamasisha Stars iishinde Algeria na kufuzu hatua ya makundi kusaka tiketi ya kucheza Kombe la Dunia mwaka 2018, badala yake Stars ikaishia kufungwa jumla ya mabao 9-2.
Jambo kubwa lililozua mkanganyiko ni suala la usafiri wa ndege kwa ajili ya Stars kwenda Algeria kwa ajili ya mchezo wa marudiano.
Awali, kamati hiyo chini ya Mwenyekiti Farough Baghozah, ilidai kupata udhamini kutoka kwa Kampuni ya Fastjet waliotoa punguzo la gharama za tiketi kwa wachezaji kufikia dola 700 (Sh. Milioni 1.4) kwenda na kurudi kwa mtu mmoja.
Hata hivyo, wakati kamati hiyo ikiandaa mipango ya usafiri kupitia Fastjet, TFF ikaja na mipango yake na kuamua kutumia ndege ya Uturuki (Turkish Airways) kwa gharama ya dola 1,200 (Sh.milioni 2.5) kwa mtu mmoja.
Isitoshe, ilielezwa kuwa Fatjet ingetumia muda mfupi (saa nane) hadi Algeria, wakati ndege hiyo ya Uturuki ilisafiri kwa saa 11 hadi Algeria.
Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Michael Wambura jana alisema wakati akizungumza na waandishi wa habari kuwa suala la mabadiliko ya usafiri liliamuliwa na TFF wenye mamlaka safari ya timu hiyo.
"Kamati ilifanya kazi yake, lakini mwisho wa siku TFF iliamua timu isafiri na ndege nyingine," alisema Wambura.
Aidha, alipoulizwa kama hakukuwa na mawasiliano baina ya Kamati na TFF kuhusu usafiri, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Farough Baghozah alisema kwenye vikao vya kamati hiyo kulikuwa na viongozi wa TFF na walikuwa wakifahamu kila kilichokuwa kikiendelea.
"Siwezi kumnyooshea kidole mtu, lakini kulikuwa na watu wa TFF kwenye kamati, tulishangaa na maamuzi yaliyotoka," alisema Baghoza.
Baghoza alisema walishafanya utaratibu (booking) Fastjet na uamuzi wa TFF kukataa kutumia ndege hiyo, umeingiza gharama kamati ya Sh. Milioni 75.
"Gharama hii ya kufuta safari ambayo tayari ilishaandaliwa, tunalazimika kulipa sisi kama kamati,” alisema Baghozah.
Alisema kuwa kamati hiyo ilifanikiwa kukusanya Sh. milioni 120, ambazo walizitumia kwa ajili ya kambi ya timu hiyo nchini Afrika Kusini pamoja na kukaa hotelini jijini Dar es Salaam wakati wakisubiri mchezo dhidi ya Algeria.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa aliikosoa kamati hiyo akidai haikuwa inafanya kazi kwa uwazi na kwamba mambo mengi hayakuwa na ukweli.
"Hiyo (Kamati) iseme ukweli. Ni jambo la kushangaza tuache kutumia usafiri wa bei nafuu na kwenda wenye gharama kubwa. Ukweli ni kwamba, Fastjet hawakutoa punguzo lolote kama kamati inavyodai, ila walikuwa wanatafuta abiria," alisema Mwesigwa.
“Hatukutaka aibu ya kushindwa kusafisha timu kwa kutegemea Fastjet ambayo hatukuwa na uhakika nayo.”
Akiikosoa zaidi kamati hiyo, Mwesigwa alidai kuwa kamati hiyo haikuwahi kuonyesha mkataba wowote wa makubaliano na Fastjet kuhusu kuipunguzia gharama na TFF.
“Sisi hatuwezi kukubali taarifa za mdomoni, tulitaka mambo yafanyike kimaandishi,” alisema na kuongeza:
“Kama kamati ingeonyesha mkataba waliosaini na Fastjet, tungeacha kutumia Ndege ya Uturuki, lakini hilo halikufanywa, sasa kwanini tuweke mategemeo kwenye kazi zisizo na uhakika?”
KINACHOSHANGAZA
Taifa Stars ina mdhamini, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) wenye jukumu la kuigharamia timu katika mambo mengi, lakini hapohapo kamati inadai imetumia Sh milioni 120 walizopata kutoka kwa wadau mbalimbali.
Awali, Kamati ilidai ilihitaji zaidi ya Sh.bilioni 1 kwa ajili ya gharama zote katika mechi mbili za Stars dhidi ya Algeria, lakini imeshindwa kupata hata robo ya fedha hizo.
Bado kamati hiyo ikifahamu haina fedha, ilitoa ahadi ya Sh. Milioni 500 kwa timu kama ingeiondoka Algeria kwenye michuano hiyo. Kama Stars ingefanikiwa, hizo milioni 500 ziketoka wapi?
Kamati Saidia Stars na TFF Wasutana na Kuonyooshea Vidole Mchana Kweupe....
0
November 29, 2015
Tags