Kinyang'anyiro cha Uspika wa Bunge...Samweli Sita na Zungu Kushikana Mashati ...Wengine ni Hawa Hapa

Wakati Bunge la Kumi na Moja likitarajiwa kuanza vikao vyake wiki ijayo mjini Dodoma, Samuel Sitta  na Anne Makinda, waliokalia kiti cha Spika wa mabunge mawili yaliyopita, wanatajwa kuwamo kwenye mchuano mwingine wa kuwania nafasi hiyo ya kuongoza chombo hicho cha kutunga sheria.

Majina ya makada hao wawili wa CCM, ambao mwaka huu hawakugombea ubunge kwenye majimbo yao, ni miongoni mwa watu kadhaa wanaotajwa kuwania kuongoza Bunge la 11 ambalo linatarajiwa kuanza vikao vyake wiki ijayo.

Kada mwingine wa CCM ambaye amekuwa akitajwa kwa muda mrefu ni mbunge wa Ilala, Mussa Hassan Zungu ambaye anatarajiwa kutoa upinzani mkubwa kwa wawili hao endapo ataingia kwenye mchakato wa kuwania nafasi hiyo.

Wengine wanaotajwa kuitaka nafasi hiyo ni mbunge mteule wa Peramiho, Jenister Mhagama, mbunge mteule wa Kibakwe, George Simbachawene na Job Ndugai ambaye ni Naibu Spika wa Bunge lililomaliza muda wake.

Kiti cha spika kinaweza kuwaniwa na mtu yeyote ambaye atapitishwa na chama chake bila ya kujali kama ni mbunge.  CCM hutoa fursa kwa wanachama wake kuomba nafasi hiyo na baadaye kikao cha wabunge wa chama hicho hukutana kupitisha jina la mgombea mmoja.

Iwapo mgombea hatakuwa mbunge mteule, ni lazima jina lake lipitishwe na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Iwapo wawili hao wataingia kwenye kinyang’anyiro hicho, Sitta, aliyeongoza Bunge la Tisa ambalo linasifika kwa kuruhusu hoja zilizoibana Serikali, na Makinda, aliyeongoza Bunge la Kumi lililoibua kashfa zilizolazimisha mawaziri kujiuzulu, watakuwa wakipambana kwa mara ya pili baada ya kukutana mwaka 2010 wakati CCM ilipomtosa Sitta kwa hoja ya “kutaka Spika mwanamke”.

Habari kutoka kwa watu walio karibu naye zinasema Sitta, ambaye ni Waziri wa Uchukuzi, atapeleka jina lake CCM kwa ajili ya kuteuliwa kuwania nafasi hiyo.

Taarifa hizo zilithibitishwa na msemaji wa mbunge huyo wa zamani wa Urambo Mashariki, John Dotto ambaye alilieleza gazeti hili kuwa Sitta atawania nafasi hiyo kutokana na uwezo na uzoefu alionao wa kuendesha Bunge.

 Alisema Sitta anaamini kuwa uwezo wake aliouonyesha katika kuendesha Bunge la Tisa (2005 hadi 2010) akitumia kaulimbiu yake ya “Spika wa Kasi na Viwango”, utamfanya aendane na kasi ya utendaji wa Rais Mteule, Dk John Magufuli.

Habari zaidi zinaeleza kuwa Sitta ana nafasi kubwa ya kuibuka mshindi kutokana na rekodi yake na pia kukubalika na wabunge wengi wa CCM na hata wa vyama vya upinzani.

Hata hivyo, Sitta hakupatikana kueleza kiundani kuhusu suala hilo kutokana na kuwa nje ya nchi. Alitarajiwa kurejea jana jioni.

Baada ya kuongoza Bunge lililomlazimisha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kujiuzulu, Sitta alijaribu kutetea nafasi yake mwaka 2010, lakini akagonga mwamba.

Baadhi ya watu walimuona kuwa ni mtu aliyekuwa akiruhusu mijadala ya kuibana Serikali, kitu kilichofanya ajijengee uadui na baadhi ya vigogo.

Wakati alipowania nafasi hiyo mwaka 2010 alijikuta akipambana na Andrew Chenge, mpinzani aliyeonekana kuwa na sifa na nguvu inayolingana naye ndani ya CCM, hali iliyokifanya chama hicho kupata mwanya wa kutumia hoja ya “zamu ya wanawake” na wote wawili wakakosa nafasi.

Sitta, ambaye amekuwa mbunge kwa vipindi tofauti kati ya mwaka 1975 na 2015, alipambana tena na Chenge kuwania uenyekiti wa Bunge la Katiba mwaka 2013.

Kabla ya kuanza kwa kampeni za uchaguzi huo, Chenge alijitoa na kumuachia Sitta ambaye aliwashinda kirahisi wagombea wengine. Makinda hakutarajiwa kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho mwaka 2010, lakini alipoingia mara moja akawa anapewa nafasi kubwa.

Watu wa karibu na Makinda, ambaye kwa mara kadhaa alikuwa akilaumiwa na wabunge wa upinzani bungeni kwa kile walichodai ni kuibeba CCM, walilithibitishia Mwananchi kuwa Spika huyo wa Bunge la Kumi atawania tena nafasi hiyo. “Subiri tu utaona, pengine anaweza kutangaza ama akajitosa tu kimya kimya. Anaonekana kuitaka nafasi hii,” alisema mtu aliye karibu naye ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe.

Kwa kawaida Makinda si mzungumzaji sana na vyombo vya habari, hasa kwa masuala yake binafsi.

Kwa upande wa Zungu, ambaye alikuwa mmoja wa wenyeviti wa Bunge la Kumi, hakutaka kukanusha wala kuthibitisha suala hilo alipoulizwa na gazeti hili.

Zungu aliliambia gazeti hili jana kuwa chama chake bado hakijatoa mwongozoo wowote hadi kufikia jana jioni na hivyo hawezi kuzungumzia suala hilo.

Mtu mwingine anayetajwa kwenye kinyang’anyiro hicho ni Naibu Spika anayemaliza muda wake, Job Ndugai, ambaye pia hakutaka kuzungumzia suala hilo kwa madai kuwa bado anauguza ‘majeraha’ ya Uchaguzi Mkuu.

Ndugai, ambaye amerudi bungeni akiliwakilisha Jimbo la Kongwa, alisema wiki hii atavieleza vyombo vya habari kama atawania nafasi hiyo.

Jibu kama hilo lilitolewa na Mhagama, ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa Bunge la Kumi kabla ya kuteuliwa kuwa waziri. Mbunge huyo wa Peramiho alisema hawezi kuzungumzia  vyema suala hilo kwa sababu yupo katika matayarisho ya hafla fupi ya kuapishwa kwa Rais Mteule.

Juhudi za kumpata Simbachawene ziligonga ukuta.

Kuhusu kupitisha wagombea wa kiti hicho, makamu mwenyeki wa CCM, Philip Mangula alisema mchakato wa chama hicho kupokea majina ya wanaotaka kugombea uspika, bado haujaanza kutokana na kutotangazwa rasmi.

Wakati hali ikiwa haijapamba moto ndani ya CCM, mwanasheria mkuu wa Chadema, Tundu Lissu jana alisema vyama vinavyounda Ukawa-Chadema, NCCR-Mageuzi, NLD na CUF- havijaanza mikakati ya kupitisha mtu atakayegombea uspika, badala yake vinaandaa kambi imara ya upinzani  kwa ajili ya kuibana Serikali bungeni.

Akizungumzia utaratibu wa kumpata Spika, mkurugenzi wa shughuli za Bunge, John Joel alisema wagombea wanaruhusiwa kutoka vyama mbalimbali vya siasa na kwamba mchakato huo utaanza baada ya rais kuapishwa na kuitisha Bunge.

“Nafasi hii haigombewi na mgombea binafsi. Ni lazima apitishwe na chama. Kama ni mbunge mteule jina lake linaletwa moja kwa moja katika ofisi za Bunge ila kama ni mwanachama wa kawaida lazima athibitishwe na NEC kuona kama ana sifa,” alisema Joel.

Alisema rais akishaitisha vikao vya Bunge, chombo hicho cha kutunga sheria ndio kitaanza mchakato wa uchaguzi wa spika na kazi ya kwanza itakuwa kupokea majina ya wagombea kutoka vyama mbalimbali.

Post a Comment

2 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. BABU MZEE SAMWELI SITA,SHIKAMOO.HIVI UNA UMRI GANI? UNA TAMAA MBAYA NA CHAFU.UBUNGE USEME UMESTAAFU UNAWAACHIA VIJANA,MARA TAMAA YA KULA IMERUDI,TENA KWA NGUVU,NI MLAFI UNATAMANI USPIKA.UTAANGUKA VIBAYA MNO,MNO.KWANZA UELEWE HUNA HATA KURA MOJA YA WABUNGE WA UKAWA,HATA MOJA.WABUNGE WA UKAWA SAFARI HII NI WENGI MNO NI ZAIDI YA 106.MARA ALFU KURA ZOTE ZA UKAWA APEWE ZUNGU.UTAANGUKIA PUA. USHAURI KAA NA BABU WENZIO WASSIRA NA MREMA WAKUONYESHE VYETI VYA HOSPIALI,WANAUMWA.UKIWATAJA UKAWA WANAWEWESEKAOVYO.NGOJA TUKUVUE NGUO.

    ReplyDelete
  2. bwana sitta inaonekana kuna kitu ulikisahau pale kwenye kiti cha uspika.ulifukia nini pale?ndio maana mama anna makinda amehenyeshwa na, hana hamu napo.waombe watumishi wa bunge wakusaidie kuifukua hirizi hiyo ikakusaidie kule unako kwenda.historia inaonyesha kuwa wewe ndiye uliye iasisi UKAWA bila kujijua.ukawa wameungana na wamepeleka kilio kikuu ccm.si unashuhudia ZANZIBAR ilivyoangukia mikononi mwa ukawa.unajua ilikuwaje? Marafiki wa Mheshimiwa Lowassa walioko Unguja ndiye waliidhoufisha kabisa ccm unguja na kura zile ziltosha kuubadili upepo wa uchaguzi wa rais wa zanzibar toka kwa Shein kuhamia kwa Seif shariff hamad.kabla ccm hawajaanza kukujadili ujue wakianza,WATAKUFUKUZA si umemsikia rais wetu mpya mheshimiwa john magufuli akimpasha rais mstaafu kikwete 'live' kuhusu wabaya wa ccm ndani ya ccm?kwenye orodha natumai hutokosa.

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad