Leo Mh. Jakaya Kikwete Anaachia Rasmi Madaraka ya Nchi na Kumkabidhi Jembe Dk. John Magufuli.....Mzee wa Viwanda

Hatimaye Tanzania inatarajia kuanza safari mpya ya mabadiliko ya kweli masaa machache yajayo baada ya Rais Mteule Dkt. John Magufuli kuapishwa jijini Dar es Salaam, zoezi litakalo hitimisha uongozi wa Rais Jakaya Kikwete.

Kuapishwa kwa Dkt. Magufuli kutafungua ukarasa mpya wa Tanzania ya Viwanda aliyoiahidi katika kila jukwaa alilopanda kuwaomba kura watanzania katika maeneo mbalimbali, “Tanzania ya Magufuli, itakuwa ya viwanda.”

Ahadi ambayo endapo itatekelezwa itasaidia kuongeza ajira, kuinua uchumi wa nchi kwa kuongeza uzalishaji wa bidhaa badala zitakazouzwa ndani na nje ya nchi kwa bei nzuri badala ya kuuza malighafi kama ilivyo sasa.

Matumaini ya watanzania
Katika saa zinazohesabika kumpokea Dkt. Magufuli, watanzania wanamatumaini ya kupata huduma bora zaidi za afya, kuondokana na tatizo la maji, elimu bora na bure hadi kidato cha nne, mitaji ya shilingi milioni 50 kwa kila mtaa zilizoahidiwa, kuanzishwa kwa mahakama ya mafisadi pamoja na uboreshaji wa kilimo na mifugo.

Aidha, watanzania wanatarajia kuianza safari ya ‘kazi tu’ yenye kasi ya maendeleo, utendaji uliotukuka pamoja na uadilifu katika sekta zote za umma.

Sherehe za kuapishwa kwa Dkt. Magufuli zitakazofanyika leo katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, zinatarajiwa kuwa za kihistoria zitakazohudhuriwa na viongozi wa serikali na vyama vya siasa kutoka nchi mbalimbali, huku kiongozi maarufu wa kanisa la Synagogue Church of All Nations, T.B Joshua akihudhuria. T.B Joshua jana alikutana na viongozi wa Ukawa baada ya kukutana na Dkt. Magufuli, Rais Kikwete na Edward Lowassa.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik ametoa wito kwa watanzania kuhudhuria kwa wingi sherehe hizo na kuwataka kuanza kuingia uwanjani kuanzia saa 12 asubuhi kutokana na idadi kubwa ya watu inayotarajiwa kuhudhuria.

“Ugeni huu ni mkubwa, sio wa hapa nchini tu bali na nchi za nje. Kwa hiyo tunaomba wana Dar es Salaam wawe waungwana na wastaarabu na waoneshe upendo wa dhati kwa wageni wetu watakaokuja kuhudhuria shughuli hii ya kumuapisha Rais wa awamu ya Tano,” alisema Mkuu huyo wa mkoa wa Dar es Salaam.

“Lakini pia watashuhudia rais aliyeko marakani sasa hivi (Rais Kikwete) akiachia madaraka ya nchi kwa utamaduni wetu tuliojenga watanzania kukabidhiana madaraka kwa amani na utulivu,” aliongeza.

Sherehe hizo zitapambwa na burudani kutoka kwa vikundi mbalimbali vya sanaa pamoja na gwaride maalum la Majeshi ya Ulinzi na Usalama.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad