Lowassa Kuongea na Watanzania Leo jijini i Arusha

Aliyekuwa mgombea wa urais wa Chadema, Edward Lowassa anatarajia kuhutubia mkutano wa kumnadi mgombea wa ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema na kuwashukuru Watanzania kwa kura walizompa katika Uchaguzi Mkuu uliopita.

Jeshi la Polisi limeridhia mkutano huo utakaofanyika viwanja vya Shule ya Msingi Ngarenaro, lakini limepiga marufuku maandamano yoyote.

Huu utakuwa mkutano wa kwanza wa hadhara kwa Lowassa tangu matokeo ya uchaguzi mkuu yalipotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ambayo yalimpa ushindi mgombea wa CCM, Dk John Magufuli. Lowassa alipata kura 6,072,848, sawa na asilimia 39.97 wakati mshindi Dk Magufuli alijikusanyia kura 8,882,935 sawa na asilimia 58.46

“Tunatarajia kesho (leo) aliyekuwa mgombea wa urais wa Chadema chini ya mwavuli wa Ukawa, Edward Lowassa atahutubia mkutano wa kampeni wa kawaida akiongozana na viongozi wengine wa kitaifa,” alisema Katibu wa Chadema Wilaya ya Arusha, Lewis Kopwe, alipozungumzia kukamilika kwa maandalizi yote ya mkutano huo jana.

Kopwe alisema mkutano huo ni sehemu ya mikutano ya kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arusha Mjini na amehimiza amani na utulivu vitamalaki katika mkutano huo.

Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Liberatus Sabas jana alisema wamepiga marufuku maandamano ya aina yoyote katika mikutano ya kampeni inayoendelea.

Alionya Jeshi la Polisi halitasita kumchukulia hatua mtu yeyote ambaye ataandamana na kusababisha kuvunjika kwa amani katika Jiji la Arusha. “Kuna watu, kwa maslahi yao, wanataka kutuvunjia amani, sasa tunaonya tutachukua hatua kali kwa yeyote ambaye atavunja sharia,” alisema Kamanda Sabas.

Pamoja na onyo hilo, alisema kuwa hadi jana jeshi hilo, lilikuwa halijapata barua yoyote ya kutaka maandamano na hata ikiwapo hawatakuwa tayari kuruhusu yafanyike. Pia, alisema jeshi hilo liko vizuri na limejipanga kuhakikisha amani na utulivu vinadumu kama ilivyokuwa wakati wa Uchaguzi Mkuu Oktoba 25 mwaka huu.

Katika hali inayoonyesha kwamba Jeshi la Polisi halitanii, jana jiji la Arusha lilikumbwa na taharuki kutokana na magari makubwa ya kurusha maji ya kuwashwa kupitishwa mitaani huku yakiwa kwenye mwendo kasi.

Kamanda Sabas alisema kilichokuwa kinafanyika ni mazoezi ya kawaida ambayo yanathibitisha kuwa polisi ipo imara. “Haya ni mazoezi ya kawaida, tunajua uchaguzi bado unaendelea na tumejipanga kulinda amani ya Arusha,” alisema.

Lema, ambaye anajiandaa kutetea kiti hicho alisema kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni kwamba Lowassa atazungumza leo na Watanzania, pia kuwashukuru kwa kumpigia kura nyingi.

Naye Mbunge mteule wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi “Sugu” alisema katika mkutano huo Chadema watatoa tamko zito la kwanza mara baada ya uchaguzi huo wa madiwani, wabunge na rais kumalizika.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad