Maguri Auzwa TP Mazembe Kwa Sh Mil 100

Na Sweetbert Lukonge
STAND United imekubali kumuuza straika wake Elias Maguri kwa TP Mazembe ya DR Congo kwa dau la dola 50,000 ambazo ni zaidi ya Sh milioni 100.
Timu hiyo imetoa kauli hiyo baada ya kuwepo kwa taarifa mbalimbali zinazomhusisha Maguri kujiunga na Yanga na TP Mazembe na sasa ipo tayari kumuachia straika huyo mwenye mabao 10 msimu huu.
Maguri ambaye yupo katika kikosi cha Kilimanjaro Stars kinachoshiriki Kombe la Chalenji huko Ethiopia, amefunga mabao tisa katika Ligi Kuu Bara, pia ana bao moja kwa timu ya taifa alililoifungia Taifa Stars dhidi ya Algeria katika sare ya mabao 2-2 Novemba 14, mwaka huu.
Ofisa Habari wa Stand United, Deo Makomba, ameliambia Championi Jumamosi kuwa, klabu yake imekubali kumuuza Maguri kwa dola 50,000 kwa TP Mzembe au timu nyingine ya nje ya nchi inayomtaka.
“Tupo tayari kumuachia Maguri ajiunge na TP Mazembe kwa dau la dola 50,000, kilichobaki sasa ni kufuatwa kwa taratibu za klabu na klabu ili mchezaji aweze kwenda DR Congo.
“Hii si kwa TP Mazembe pekee, timu yoyote ya nje ya nchi inayomtaka Maguri ijue hilo ndilo dau lake lakini kwa timu ya hapa nchini, inatakiwa kulipa Sh milioni 50 ili tuwaachie Maguri,” alisema Makomba.
Yanga ndiyo klabu pekee ya Tanzania iliyotajwa kumuwania Maguri na hata mchezaji mwenyewe aliwahi kunukuliwa kuwa tayari kuichezea timu hiyo badala ya Simba ambayo aliachana nayo hivi karibuni.
Hata hivyo, Maguri ameliambia gazeti hili: “Nilizungumza na Yanga kuhusu kujiunga nayo lakini sasa nimebadili mawazo na akili yangu yote ipo kwa TP Mazembe, nataka kufika mbali zaidi.
“Hata kama Yanga watakuja na dau kubwa kushinda Mazembe, nitaichagua timu hiyo ya DR Congo.”
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad