Mwenyekiti wa Taifa wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema, amesema hata kama vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vimefanikiwa kumwangusha kwenye kinyang’anyiro cha ubunge katika Jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro, bado ana nguvu ya kuendelea kuwania nafasi mbalimbali za kisiasa na wala hajakata tamaa ya kukisuka upya chama chake.
Mrema aliangushwa katika kiti hicho na hasimu wake kisiasa, James Mbatia, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha NCCR-Mageuzi, aliyevunja rekodi ya kupata kura nyingi kwa upande wa wabunge wa upinzani, baada ya kuibuka na ushindi mnono wa kura 60,187 dhidi ya 6,416 alizoambulia Mrema (TLP) aliyekuwa akishikilia jimbo hilo huku mgombea wa CCM, Innocent Shirima, akipata kura 16,097.
Alikuwa akihojiwa jana na kituo kimoja cha redio mkoani Kilimanjaro kuhusu majaliwa yake kisiasa, baada ya yeye na chama chake kukosa uwakilishi kwenye Bunge na Halmashauri za Wilaya. Mbali ya kupoteza kiti cha ubunge, TLP haikuambulia hata kiti kimoja cha udiwani.
“Chama changu hakifi na wala sijakata tamaa, tutaanza moja na ninawaomba wanachama wa TLP watulie…Nitashirikiana na Rais ajaye aliyetangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), na tutakijenga chama chetu…Hata Dk. John Magufuli, anajua mimi ni mchapakazi na alinipigia debe na wananchi wakapuuza,” alisema Mrema.
Katika Mkoa wa Kilimanjaro wenye majimbo tisa ya uchaguzi, viti saba vya ubunge vimenyakuliwa na baadhi ya vyama vinavyounda Ukawa vya Chadema na NCCR-Mageuzi, huku majimbo mawili ya Mwanga na Same Magharibi, yakiangukia CCM.
Kwa mujibu wa matokeo hayo, Chadema iliyovuna wabunge sita na NCCR-Mageuzi yenye mbunge mmoja mkoani Kilimanjaro, sasa zitaunda halmashauri tano za wilaya ambazo ni Moshi Mjini, Hai, Siha, Rombo, Moshi Vijijini na Vunjo; wakati CCM ikiwa imeambulia Halmashauri mbili za Mwanga na Same.
Majimbo hayo na idadi ya kata ambazo Chadema na NCCR-Mageuzi zitaunda halmashauri zake ni kama ifuatavyo;
Moshi Mjini, Chadema imeshinda Kata 19 kati ya 21 na CCM imepata Kata mbili za Bondeni na Kilimanjaro, wakati Jimbo la Hai, Chadema imeshinda kata 16 kati ya 17, ambapo Kata moja ya Bomang’ombe ndio pekee haijafanya uchaguzi kutokana na mgombea wa CCM kufariki dunia wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu.
Aidha, Chadema iliyoshinda kata 27 kati ya 28 za Wilaya ya Rombo, ndiyo itakayounda halmashauri ya wilaya hiyo, huku NCCR-Mageuzi iliyoshinda kata nane, kati ya 16 na Chadema iliyoshinda viti 15 vya udiwani katika Jimbo la Moshi Vijijini, sasa zitaunda Halmashauri moja ya Wilaya ya Moshi.
Katika Jimbo la Moshi Vijijini, CCM imeshinda kata moja tu.