‘Mzimu’ wa Kanuni Wamwandama Naibu Spika..Wasomi Wadai Amekiuka Kanuni za Utumishi wa Umma

Ushiriki wa aliyekuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Tulia Ackson katika masuala ya siasa na hatimaye kuchaguliwa Naibu Spika wa Bunge, umezidi kuibua maswali huku akidaiwa kuwa amekiuka kanuni za watumishi wa umma.

Wasomi, wanaharakati na wanasheria wameeleza kushangazwa na uteuzi huo, kama ilivyokuwa Alhamisi alibobanwa kwa maswali bila majibu kuhusu ni lini msomi huyo wa sheria alichukua kadi ya CCM na kuwania uspika na baadaye unaibu spika kupitia chama hicho.

Hata hivyo, Dk Ackson amekanusha kukiuka kanuni za utumishi wa umma akisema ile inayolalamikiwa kukiukwa (Kanuni za Utumishi wa Umma 2009), ilifutwa kupitia waraka mpya uliotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Januari, mwaka huu.

“Angalia hiyo ‘circular’ kifungu cha (5), kinasemaje, usiangalie hiyo kanuni tena kwani imefutwa na huo waraka, ukisoma unaonyesha wazi. Zote hizo unazoniambia nilizifahamu kabla ya kuchukua hatua yoyote, sijakurupuka tu,” alisema.

Wiki iliyopita Dk Ackson akiwa mwanasheria wa Serikali alichukua fomu ya kuwania uspika wa Bunge kinyume na matakwa ya kanuni za utumishi wa umma, lakini baadaye alijitoa katika kinyang’anyiro hicho na kuwania unaibu spika, baada ya kuteuliwa na Rais John Magufuli kuwa mbunge.

Mchakato wa Dk Ackson kuteuliwa kugombea hadi kushika nafasi hiyo umezua maswali watu mbalimbali wakihoji ukiukaji wa kanuni hiyo inayozuia wanasheria wa Serikali kujiunga na mambo ya siasa.

Akijibu maswali ya wabunge wakati akiomba kuchaguliwa kuwa naibu spika, Dk Ackson alishindwa kueleza ni lini alichukua kadi ya CCM, hadi Spika wa Bunge Job Ndugai alipoingilia kati akamruhusu kwenda kuketi.
Wachambuzi

Akizungumzia suala hilo, mwanaharakati kutoka HakiElimu, Godfrey Bonaventure alisema kitendo cha Dk Ackson kuteuliwa kushika nafasi hiyo kinaleta maswali mengi katika kanuni za utumishi wa umma na masuala ya siasa.

“Miongozo iliyopo imeweka bayana kuwa wapo watumishi wa umma ambao hawatakiwi kujihusisha na siasa kutokana na unyeti wa majukumu yao,” alisema.

Alisema suala kubwa ambalo Dk Ackson anatakiwa kujibu kwa usahihi ni je, lini alianza kuwa mwanachama wa CCM?

“Watu wanaotakiwa kuhusika kwenye uamuzi mkubwa hawatakiwi kujihusisha kwenye siasa. Hili suala lina mitego ambayo inavuruga mfumo wetu wa uwajibikaji, inatupa shaka kwa sababu hawa watu maamuzi yao ni magumu, uspika ni wajibu mkubwa,” alisema.

Bonaventure aliitaka Serikali kuheshimu miongozo yote ya utumishi wa umma ili vyombo hivyo viwe huru kufanya uamuzi.

“Alipoulizwa swali bungeni kuhusu lini alikuwa mwanachama  wa CCM hakuweza kutoa jibu sahihi, bila shaka angesema ni lini angeibua maswali mengi zaidi,” alisema.

Alisema iwapo Dk Ackson angesema amekuwa mwana CCM kwa muda mrefu angeibua maswali, lakini pia angesema amechukua kadi ya CCM hivi karibuni angeibua hoja atawezaje kukifahamu chama na kujua namna ya kuliongoza Bunge katika kipindi kifupi?

Mwanasheria wa kujitegemea, George Shayo alisema sheria inaweka wazi kuwa watumishi wa Serikali hawatakiwi kushiriki katika siasa.

Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah Safari alisema sheria zinakataza watumishi wa umma kujihusisha na siasa.

Profesa Safari ambaye pia ni wakili, alisema ingawa baadhi ya vipengele vimefanyiwa marekebisho lakini wafanyakazi wa Mahakama na wanasheria wa Serikali hawatakiwi kujihusisha na siasa.

“Ndiyo maana hata wakati Jaji Augustino Ramadhani alipochukua fomu ya urais, tulimsema sana. Hata hizi sarakasi za Dk Ackson zinachekesha, zinashangaza,” alisema.

Mhadhiri  wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es  Salaam, Dk Alexander Makulilo alisema anafahamu kuwa kuna sheria kuhusu wafanyakazi wa umma lakini haiwakatazi kujihusisha na siasa bali upo utaratibu wa kufanya hivyo.

“Iko miongozo ya Serikali kuhusu watumishi wa umma lakini si kwamba sheria inakataza, kwa mfano miongozo hiyo inawataka waache nafasi zao pindi wanapotaka kuingia katika siasa,” alisema.

Post a Comment

3 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Aliyewatuma ni mufilisi!

    ReplyDelete
  2. Tulia ni mwanasheria, hawezi kufanya jambo ambalo anajua atakuwa amevunja sheria. ANAJITAMBUA.
    Chadema badala ya kunyamaza ili Tulia atoe maeleze alitumia kifungu gani, kwa ujinga wao wakampigia makelele na kumzomea...., kama wangempa nafasi tungejua alitumia kifungu gani, na alijiunga lini na CCM, matokeo yake wakakosa MWANA na MAJI YA MOTO, na sasa haohao wanamwita MUHESHIMIWA NAIBU SPIKA.....hahahaha HAPA KAZI TU......

    ReplyDelete
    Replies
    1. Sheria ya kubebwa na Migiro UDSM

      Delete

Top Post Ad

Below Post Ad