Rais Magufuli Afanya Ziara Ya Kushtukiza Muhimbili..Akuta Hali ya Kusikitisha....Avunja Bodi Ya Uongozi Wa Hospitali, Ateua Uongozi wa Muda

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli , leo mchana amefanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kukutana na hali ya kumsikitisha.

“ Rais  amesikitishwa na kuhuzunishwa na hali ya huduma kwa wagonjwa hususan wanaolala chini. Pia amekasirishwa na hali ya kutokujali wala kushughulikia vifaa vya kufanyia kazi ambapo amekuta mashine muhimu za uchunguzi wa magonjwa kama vile MRI na CT-SCAN zikiwa hazifanyi kazi kwa muda wa miezi miwili sasa, ilihali mashine kama hizo katika Hospitali za binafsi zinafanya kazi na wagonjwa wanaelekezwa kwenda kutafuta huduma huko”.  Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue amesema na kutoa maelekezo yafuatayo :

Rais amevunja Bodi ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambayo ilishamaliza muda wake na amemteua Prof. Lawrence Mseru , kukaimu nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa Muhimbili kuanzia kesho tarehe 10 Novemba, 2015.

Dkt. Hussein L. Kidanto ambaye ndiye anayekaimu hivi sasa, amehamishiwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ambako atapangiwa kazi nyingine.

Balozi Sefue pia amesema,   Rais ametoa wiki moja na kwa vyovyote si zaidi ya wiki mbili kwa uongozi mpya wa Muhimbili kuhakikisha kuwa mashine zote za uchunguzi wa magonjwa ambazo hazifanyi kazi zinafanya kazi na kuhudumia wananchi kama ipasavyo.

Tayari Wizara ya Fedha imetoa shilingi bilioni 3 kwa ajili ya kazi hiyo na kulipa madeni ya ukarabati wa mashine za uchunguzi wa magonjwa nchini.

Hata hivyo Katibu Mkuu Kiongozi amesema kuanzia sasa hospitali zote nchini zinatakiwa kutenga fedha kutoka kwenye mapato yao wenyewe na kuhakikisha mashine na vifaa vyote vya kazi vinafanya kazi wakati wote (Regular Maintenance).

Balozi Sefue pia metumia nafasi hii kuwaagiza watendaji na viongozi wote katika sehemu za kazi kuhakikisha wananchi wanahudumiwa ipasavyo na kazi za umma zinatekelezwa ipasavyo.

“Hakutakuwa na huruma kwa watumishi wa Umma wasiojali wananchi na mahitaji yao” Amesisitiza Balozi Sefue.

Imetolewa na;

Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
Ikulu – Dar es Salaam.
9 Novemba, 2015

Post a Comment

3 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. NGUVU YA SODA HIYO.

    ReplyDelete
  2. Huyo ndio bwana magufuli bana

    ReplyDelete
  3. Daah!yaani mwenzenu nimetokea kumuamini huyu baba,Mungu akupe uzima,uendelee na mwendo huohuo.Tanzania tunataka kupelekwa mchakamchaka maana hatujui kujituma,watu
    wanaitwa watendaji,mabibi na mabwana afya wako tu maofisini hawawajibiki kuangalia mazingira,hata kipindupindu ni ugonjwa ambao unaweza kutokomezwa kabisa isipokuwa ni uzembe na uchafu uliokithiri.MUNGU IBARIKI TANZANIA.

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad