Mwanza. Ugonjwa wa kipindupindu umeendelea kuleta maafa mkoani hapa, baada ya kusababisha vifo vya watu 17 na wengine 268 kulazwa katika vituo mbalimbali vya afya tangu Septemba, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Dk Faisal Issa, Daktari Bingwa wa Hospitali ya Mkoa ya Sekou Toure, Dk Magret Magambo alisema mlipuko wa ugonjwa huo ulianza Septemba 16 katika Kisiwa cha Irugwa wilayani Ukerewe.
“Vifo viwili viliripotiwa katika Zahanati ya Irugwa na sita vilitokea ndani ya jamii ya kisiwa hicho. Baadaye ugonjwa huo umeripotiwa kutokea katika maeneo mengine ya wilaya hiyo ambayo ni vijiji vya Kagunguli, Katunguru na Kazilankanda ambapo hadi leo (jana) jumla ya wagonjwa 192 na vifo 12 vilitokea katika Wilaya ya Ukerewe.
“Hata hivyo juhudi kubwa za kupambana na mlipuko katika Kijiji cha Irugwa zimefanyika na kwa siku kadhaa hakuna wagonjwa wapya wanaoripotiwa.
Wilaya nyingine iliyoathirika ni Sengerema ambako vijiji vya Kanyala na Bulolo vimesharipoti wagonjwa takriban 73 na vifo vitano,” alisema.
Dk Magambo alisema Wilaya ya Nyamagana imepokea wagonjwa watatu ambao walitoka sehemu mbalimbali, ambazo zilikuwa na mlipuko wa ugonjwa huo na kwamba, walitibiwa na kuruhusiwa.
“Kwa ujumla hadi leo (jana) Mkoa wa Mwanza wamejitokeza wagonjwa wengi, kati ya hao vifo ni 17. Wanaoendelea na matibabu ni 33 wakati waliotibiwa na kuruhusiwa wako 217. Ugonjwa huo umesambaa katika Wilaya ya Sengerema na kuripotiwa kuwa na wagonjwa 73 na vifo vitano, Ukerewe katika maeneo mbalimbali wagonjwa na kifo kimoja na Nyamagana,” alisema Dk Magambo.
Kwa upande wake, Ofisa Afya wa Mkoa wa Mwanza, Fungo Masalu alizitaka halmashauri zote ziunde kamati hai za udhibiti wa kipindupindu kulingana na miongozo ya udhibiti wa ugonjwa huo.
“Halmashauri zote ziimarishe hali ya usafi wa mazingira katika maeneo yao, zihakikishe taka zinakusanywa na kuondoshwa katika mitaa ili kuepuka mrundikano unaoweza kushawishi makazi ya wadudu waenezao kipindupindu, kazi hizo zifanyike chini ya kamati za udhibiti wa kipindupindu,” alisema Masalu.
Ofisa huyo alisema Serikali itaendelea kufuatilia na kuhamasisha jamii ili iweze kuepukana na ugonjwa huo.
Ugonjwa wa Kipindupindu Wahamia Mwanza, Wauwa Watu 17
0
November 02, 2015
Tags