Zigo la Z’bar ni la Magufuli au Kikwete?

Wakati majadiliano ya kina yanaendelea visiwani ili kufikia mwafaka wa kuendelea na mchakato wa kutangaza matokeo ya uchaguzi mkuu Zanzibar uliofanyika Oktoba 25 au kurudiwa upya, imeelezwa kuwa suala hilo linaweza kupata ufumbuzi iwapo litashughulikiwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Jakaya Kikwete au Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli.

Kikwete ametupiwa zigo hilo kwa sababu ya wadhifa wake wa uenyekiti wa chama tawala ambacho kwa Zanzibar kinapambana na chama cha upinzani cha CUF.

Hata hivyo, kundi jingine linasema suala la Zanzibar linaweza kutatuliwa na Rais wa Tanzania, Dk Magufuli kwa sababu ndio mwenye dola.

Lakini baadhi ya wasomi wamesema jambo hilo litamalizwa na Wazanzibari wenyewe.

Wakitoa maoni yao kuhusu mtanziko wa kisiasa uliovikumba visiwa vya Unguja na Pemba tangu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha alipotangaza kufuta matokeo ya uchaguzi mkuu, wiki iliyopita wamesema hali ya sasa inafafana na iliyotokea miaka ya nyuma ambapo ilimalizwa kwa aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Amani Karume na Katibu Mkuu wa CUF, Seif Sharrif Hamad kukutana na kumaliza tofauti zao.

Baada ya viongozi hao kujali maslahi ya Wazanzibari walikubaliana kurekebisha Katiba ya Zanzibar ambapo vyama vilivyotofautiana kwa asilimia ndogo ya ushindi vishiriki kuunda Serikali. Mwafaka huo ndio uliozaa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) ambayo ilimaliza mpasuko na uhasama wa kisiasa uliokuwapo awali.

Profesa Kopoka

Profesa wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Peter Kopoka amesema viongozi wa vyama vya siasa vya CCM, CUF, na vingine vinavyohusika pamoja na ZEC, hawana budi kufikia mwafaka kwani mgogoro wowote ulimwenguni humalizwa na pande husika hivyo wakae na kumaliza wenyewe na siyo kutegemea zaidi watu wa nje.

“Wazungumze bila kulala wao kwa wao kupitia ZEC. Isitumike nguvu zaidi ya busara na kwa hali ilivyo wangefikia mwafaka hata leo,” alisema Profesa Kopoka.

“Kadri muda unavyokwenda bila kupatikana mwafaka ndivyo hatari inavyokuwa kubwa na huo ndiyo ukweli, hivyo Wazanzibari wenyewe wayamalize na hawa watu wa nje wawe ni wa kutoa mapendekezo tu.”

Dk Benson Bana

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Dk Benson Bana amesema kuwa tatizo la Zanzibar ni zaidi ya uchaguzi. “Kinachotokea Zanzibar kwa sasa ni aina ya muundo wa Muungano tu na si kingine,” alisema.

Kwa mtazamo wake ili migogoro ya kisiasa imalizike visiwani humo lazima upatikane muundo mwafaka ambao ni Muungano wa Serikali Moja badala ya huu wa sasa.

“Nje ya Serikali moja ‘makandokando’ hayataisha. Mjadala wa Serikali moja unaweza kufanyika taratibu tu na Dk Magufuli, Samia (Suluhu Hassan-Makamu wa Rais) na Maalim Seif mpaka mwafaka utapatikana. Busara iliyotumika kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa itumike kumaliza sintofahamu iliyofanywa na Jecha. Mvutano huu wala hauwezi kumalizwa na mataifa ya nje ni Wazanzibari wenyewe na Watanzania,” alisema

Dk Bana alisema kuwa hata mwaka 2010, Maalim Seif alilalamika kuwa amepokonywa ushindi, lakini mazungumzo yalifanyika na hali ikawa shwari.

Dk Ave Semakafu

Mratibu wa Umoja wa Wanawake Wanasiasa Tanzania (Ulingo), Dk Ave Maria Semakafu alisema mwenendo unaoendelea kutatua mgogoro huo ndiyo sahihi kwa kuwa pande zinazohusika zimeonekana kuchukua hatua stahiki na subira zaidi inahitajika.

Alisema ni wazi kuwa katika uchaguzi huo kulikuwa na tatizo la msingi ambalo mojawapo ni uvunjaji wa Sheria ya Uchaguzi kwa mmoja ya wagombea kujitangazia ushindi, hivyo mazungumzo baina ya pande hizo yanahitajika na kuongozwa na busara.

“Kwa hali ilivyo ni heri tuwaache wajadili wenyewe, watafakari kwa kina ili watakapokuja na mwafaka uwe unajitosheleza na kumaliza kabisa mgogoro, hakuna haja ya kuharakisha mazungumzo hayo,” alisema.

Aidha, alisema mgogoro huo hautakiwi ujadiliwe na kuchukulia kama wa watu binafsi, yaani wa Maalim Seif na Dk Shein badala yake uangaliwe kwa mustakabali wa Wazanzibari wote.

Profesa Mpangala

Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Ruaha alisema vyombo vya juu vya CCM vikiongozwa na Mwenyekiti wao, Rais Kikwete vina dhamana kubwa ya kutatua mgogoro huo.

Alisema matatizo yanayoendelea Zanzibar yanaeleweka kwa kuwa CCM huwa hawapo tayari kuachia madaraka hivyo hata kama mazungumzo yataendelea baina ya pande hizo mbili au kutekelezwa kwa uamuzi wa ZEC wa kurudia uchaguzi, hakutakuwa na matunda yoyote.

 “CCM ngazi ya taifa waamue kukubali hali halisi, iwapo wameshindwa katika uchaguzi wakiachie chama kilichoshinda zaidi ya hapo mgogoro wa Zanzibar unakuzwa bila sababu. Kwa maana hiyo ZEC isitishe kufuta uchaguzi, iendelee na kutangaza matokeo na aliyeshinda apatiwe madaraka kwa kuwa kurudia uchaguzi siyo utatuzi sahihi,” alisema Profesa Mpangala.

Profesa Penina Mlama

Mwenyekiti wa Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Penina Mlama amesema kuwa mvutano huo utamalizwa na watu kutoka nje ya Zanzibar.

“Sidhani kama Wazanzibari wenyewe wanaweza kufikia muafaka wa suala hili. Rais Kikwete bado ni Mwenyekiti wa CCM, yeye pamoja na Rais Magufuli wanaweza kuweka mambo sawa. Bila shaka kuna mazungumzo yanaendelea sidhani kama viongozi wako kimya. Kama wakishindwa wanaweza kuwashirikisha viongozi wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki maana hata Tanzania huwa inasuluhisha migogoro ya nchi nyingine,” alisema.

Historia

Hii ni mara ya tatu unatokea mgogoro wa kisiasa Zanzibar ukihusisha matokeo ya uchaguzi mkuu. Mwaka 1995 ulizuka mgogoro mkubwa lakini Jumuiya ya Madola ilipatanisha na viongozi wa CUF na Serikali walitiliana saini lakini mwafaka haukuheshimiwa.

Baada ya uchaguzi mkuu wa 2005, Rais Kikwete alianzisha rasmi juhudi za kupatanisha na zilipoelekea kukwama Rais Karume na Maalim Seif walikutana, wakajadiliana, wakaafikiana kubadili Katiba na baada ya uchaguzi mkuu wa 2010 ikaundwa SUK.

Mvutano wa sasa ulizuka baada ya Jecha kufuta matokeo yote ya uchaguzi wote wa urais, wawakilishi na madiwani uliofanyika Oktoba 25, kwamba utarudiwa ndani ya siku 90.

Jecha alitaja sababu za kufuta uchaguzi huo kuwa ni baada ya kujiridhisha kuwa kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa sheria na taratibu na kwamba mmoja wa wagombea urais, Maalim Seif alishajitangazia matokeo yanayompa ushindi.

Uamuzi huo wa Jecha ulipingwa na watu wa kada mbalimbali, wakiwamo makamishna wa ZEC, jumuiya za kimataifa; waangalizi wa uchaguzi wa kimataifa na wa ndani pamoja na CUF wote wakishinikiza Tume iendelee na mchakato wa kumtangaza mshindi.

Tayari Maalim Seif, na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein wamekutana kujadili suala hilo. Kilichojadiliwa hakijawekwa wazi lakini viongozi wa CUF wamekuwa wakisisitiza kuwa hawatakubali kurudiwa kwa uchaguzi huo.

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Zigo ni la CCM haijarishi nani yupo madarakani

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad