Zitto: ACT - Wazalando itashirikiana na Magufuli

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe amesema chama cha ACT-Wazalendo kitashirikiana na Rais John Magufuli katika vita dhidi ya ufisadi.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Zitto alisema nchi inanuka uvundo wa ufisadi na kwamba Taifa limepata kiongozi mwenye nia ya dhati ya kupambana nayo kwa dhati na hivyo Watanzania wanalo jukumu la kumuunga mkono.

“Nilipokuwa mwenyekiti wa Kamati za Bunge nimekuwa nikitoa taarifa mbalimbali dhidi wizi na uporaji uliofanywa katika ubinafsishaji, sasa tumepata Rais ambaye kaamua kupambana na ufisadi kwa dhati, kaamua kurejesha viwanda vyetu vilivyouzwa ovyo, ni wajibu wetu kumuunga mkono,” alisema.

Alisema asilimia 60 ya masuala yaliyotajwa na Rais Magufuli katika hotuba yake yanatoka kwenye ilani ya ACT ambayo walimkabidhi wakati alipotangazwa kuwa mshindi wa nafasi hiyo.
Akizungumzia kitendo cha Zitto kutoungana na wabunge wa Ukawa kususia hotuba ya Rais, mshauri wa ACT-Wazalendo, Profesa Kitila Mkumbo alisema huo ni msimamo wa chama hicho kwa kuwa matatizo ya Zanzibar yatatatuliwa kwa njia za kisheria na kisiasa.
Alisema chama hicho kinamtambua Dk Magufuli kama mshindi halali wa kiti cha urais.
“Katika hili la Zanzibar tunafanana katika msingi wa hoja lakini tunatofautiana katika mkakati wa utekelezaji wa hoja husika na hili halina ubaya wowote, ni afya kabisa kwa demokrasia yetu,” alisema Mkumbo.

Niwemugizi  ataka aungwe mkono
Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu wa Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Severine Niwemugizi amesema hotuba ya Rais Magufuli ni nzito inayohitaji kuungwa mkono na watendaji wote wa Serikali kuanzia ngazi ya chini hadi Taifa.
Kauli ya kiongozi huyo inatokana na Rais Magufuli kuwahakikishia Watanzania kuwa atapambana kufa na kupona dhidi ya vigogo ambao wamekuwa wakihujumu maendeleo ya umma kutokana na rushwa, ufisadi na uzembe.

Alisema kutokana na nchi ilipofikia, Watanzania wanapaswa kumuunga mkono katika mkakati wake wa kupambana na ufisadi.
Askofu  huyo alitoa kauli hiyo jana kwenye ibada maalumu iliyofanyika kwenye Parokia ya Chato, kwa lengo la kumwombea Rais Magufuli ili aweze kutimiza majukumu yake katika kuwaletea maendeleo Watanzania.

“Hotuba ya mheshimiwa Rais Magufuli ilinifurahisha sana... lakini iliitia woga sana kwa sababu ya wale viongozi wanaoona wamemuingiza madarakani mwenye kuziba mianya ya rushwa, hivyo watajitahidi sana kuhujumu afya yake na hata malengo yake kwa kuwa amejiita ni mtumbua jipu.
“Mtakumbuka kabla ya kuhitimisha hotuba yake aliwaomba Watanzania tumwombee, ndiyo maana sisi kama kanisa tumeamua kumwombea ili Mungu amtangulie katika mambo yote... tunatambua atakutana na vigingi vya kila aina.”

Mbali na kumwombea kutimiza wajibu wake, ibada hiyo pia imetumika kuliombea Taifa kudumisha amani upendo na mshikamano kwa kuwa bila ya amani, nchi haitaweza kutawalika.
“Tunatakiwa kutumia muda wetu mwingi kuliombea Taifa amani... Rais Magufuli atapata wakati mgumu sana kuiongoza nchi hii iwapo hapatakuwa na amani,” alisema.
Akizungumza katika ibada hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Chato, Shaaban Ntarambe alisema kwa sasa Watanzania wanatakiwa kuwa wamoja kwa kumuunga mkono Rais aliyeko madarakani ili aweze kutimiza majukumu yake.

Alisema ili wananchi waweze kufikia maendeleo ya kweli, wanapaswa kufanya kazi kwa bidii kutimiza falsafa ya “hapa kazi tu” hatua itakayowasaidia kuinua uchumi wao.

Profesa Lipumba ajadili hotuba
Akizungumzia hotuba ya Dk Magufuli, Mwenyekiti wa zamani wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema ili afanikiwe kutekeleza sera ya viwanda, dawa pekee ni kuwanyang’anya wawekezaji waliohodhi bila kuviendeleza.
Tayari Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru ametoa tangazo la kuwataka wawekezaji walionunua mashamba na viwanda vya Serikali kuwasilisha taarifa za utekelezaji wa mikataba ya mauzo ili kuwabaini waliokiuka masharti.
Mikataba yote ya mauzo ya viwanda na mashamba iliyoingiwa kupitia ubinafsishaji, itarejewa upya na kwamba  hatua stahiki zitachukuliwa ikiwamo kurejesha viwanda na mashamba hayo kwenye miliki ya Serikali kwa waliokiuka masharti.

CCM Zanzibar yailaani Ukawa
Katika hatua nyingine, CCM Zanzibar imelaani kitendo cha kuzomewa kwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein pamoja na Makamu wake wa Pili, Balozi Seif Ali Idd kilichofanywa na wabunge wa Ukawa wakati akiingia bungeni kwa ajili ya kushuhudia uzinduzi wa Bunge la Kumi na Moja.
Katibu Kamati Maalumu ya NEC, Waride Bakari Jabu alisema kuwa kitendo hicho ni miongoni mwa vitendo vya ukosefu wa nidhamu kwa wabunge hao.

* Imeandikwa na Tumaini Msowoya, Joyce Mmasi na Haji Mtumwa.


Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. KIBWETERE ZITTO KABWE.ALISIMAMISHA WAGOMBEA WA UBUNGE 219 AKAISHIA KUPATA KITI KIMOJA AKE TENA CHA KWAKE MWENYEWE KWA MBINDE NA USHINDI MWEMBAMBA WAGOMBEA 218 CHALI.HUYU BWANA ANASUMBULIWA NA MAONO TATA.TUISHIE HAPO MFUATILIENI MTAKUJA SEMA.

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad