CCM Yajipanga Kurudia Uchaguzi Zanzibar.......Yawataka Wanachama Wake Kujitokeza Kwa Wingi

KAMATI Maalumu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar chini ya Mwenyekiti wake Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein imewataka wananchi na wanachama kujiweka tayari na hatimaye kujitokeza katika uchaguzi mkuu wa marudio.

Kwa mujibu wa taarifa ya Katibu wa Itikadi na Uenezi Zanzibar, Waride Bakari Jabu, wananchi wametakiwa kujiandaa kwa uchaguzi wa marudio na kuachana na propaganda zinazotolewa na watu wachache kwa lengo la kupotosha ukweli.

“Kikao cha Kamati Maalumu ya CCM Zanzibar kilichokutana hapa chini ya Mwenyekiti wake Rais wa Zanzibar, Dk Shein kimewataka wananchi, wanachama na wafuasi wa CCM kujitayarisha kwa uchaguzi mkuu wa marudio ambao tarehe ya kufanyika kwake itatangazwa na taasisi husika,” imesema taarifa hiyo ya Waride.

Matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa Oktoba 25 ulifutwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha kwa kile alichoeleza ni kuwepo kwa ukiukwaji wa kanuni na sheria za uchaguzi huru wa kidemokrasia.

Katika kikao cha jana kilichohudhuria pia na viongozi kadhaa wa kitaifa akiwemo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kilijadili ajenda mbili ikiwemo hali ya kisiasa mara baada ya uchaguzi mkuu kwa upande wa CCM.

Katika taarifa hiyo, chama hicho kimesema kimeridhishwa na mwenendo wa hali ya kisiasa na kimewapongeza wanachama waliojitokeza kwa wingi kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25.

Aidha chama kimepongeza na kutoa baraka kwa mazungumzo yanayoendelea ya viongozi wakuu wa kisiasa yakiwa na lengo la kuleta amani ya kudumu. Kamati ya mazungumzo ya hali ya kisiasa Zanzibar yenye lengo la kusaka amani ya kudumu iliyovurugika kutokana na kufutwa kwa uchaguzi mkuu inaundwa na viongozi wastaafu wakiwemo marais, Dk Salmin Amour, Amani Abeid Karume, Balozi Seif Ali Iddi ambaye ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Seif Sharif Hamad na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein.

Akizungumza juzi Ikulu, jijini Dar es Salaam, Rais wa Zanzibar, Dk Shein alisema mazungumzo hayo yanaendelea vizuri na taarifa kamili yatakapofikia tamati. Alipoulizwa kuhusu hatma ya CCM kama uchaguzi mkuu utarudiwa, Waride alisema chama bado kiko imara na hakijatetereka.

“Wapo wanaosema CCM imeyumba, si kweli wala CCM haijapoteza majimbo kwa sababu kura hazikumalizwa kuhesabiwa,” alisema.
Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Ewe Mwenyezi Mungu Baba nizidishie uvumilivu na ujasiri wa moyo,amani na maisha na kukubali,kuwa Tanzania haina demokrasi ya kweli,haiheshimu weledi wa kuheshimu sheria na utawala bora,kimsingi ni nchi ya utawala wa chama kimoja CCM,haiheshimu maamuzi ya 'wengi wape',ni nchi yenye matatizo makubwa sana ya kustawisha maendeleo ya wananchi wake,imejawa -full kabisa-chuki,husuda,uongo wa longolongo,CCM imepangwa na kujipanga KUITAWALA NCHI KWA MIAKA ISIYO NA UKOMO KWA MSAADA WA SHERIA KANDAMIZI[MWIKO KUZIJADILI],naomba nisiendelee kuchambua maana ninazo sababu za ukweli nyingi kiasi cha kuwachanganya kabisa waliokua HAWAJUI! TUNASTAHILI KUPEWA POLE NA WALIMWENGU YAANI "POLENI WATANZANIA JANGA MNALO".

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad