Chama cha Wananchi CUF Zanzibar kimesema hakipo tayari kupokea maazimio ya mazungumzo ya kutafuta mwafaka wa Uchaguzi Mkuu kama yatakuwa yanakwenda kinyume na maamuzi waliofanya wananchi kupitia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 Mwaka huu.
Tamko hilo limetolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi na Mipango wa Chama hicho, Omar Ali Shehe katika mahojiano maalum na Nipashe Jumapili juu ya mazungumzo ya kutafuta mufaka wa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar.
Mazungumzo hayo yanaogozwa na Rais wa Zanzibar DK. Ali Mohamed Shein na kuwashirikisha Makamo wa kwanza wa Rais wa Zanzibar na Mgombea urais kupitia CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi pamoja na marais wastaafu wa Zanzibar. Alisema CUF kiko tayari kupokea maamuzi na kuyaheshimu kutoka katika Kamati hiyo ya mazungumzo kama yatakuwa yamezingatia maamuzi ya wananchi waliyoyafanya kupitia Uchaguzi Mkuu huo.
Inaaminika kuwa matokeo yaliyofutwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) yalikuwa yakimpa ushindi Hamad. “Sisi tunasubiri matokeo ya mazungumzo yao tukiamini kwamba mazungumzo hayo hayatokwenda kinyume na maamuzi waliyofanya wananchi kupitia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba Mwaka huu,” alisema Shehe.
Alisema kuwa Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salum Jecha hakuwa na mamlaka ya kikatiba na kisheria kufuta matokeo ya uchaguzi huo ambao tayari ulikuwa umekamilika kwa asilimia 70 na matokeo ya majimbo 31 yakiwa yametangazwa katika uchaguzi huo.
Shehe alisema siri ya kufutwa kwa matokeo ni baada ya Mwenyekiti kuona CCM wapo katika hatari ya kuanguka katika uchaguzi huo na hakuna sababu nyigine. “Mchezo wa kufuta matokeo kwa sababu tu chama tawala kiko katika hatari ya kuanguka utaendelea kufanyika kama tukiacha hivi hivi,” alisema.
“Huku ni kuvuruga demokrasia ya nchi yetu.” Alisema miezi miwili sasa imemalizika lakini hakuna mtu yoyote aliyefikishwa Mahakamani kwa kuharibu uchaguzi au Mwenyekiti kuweka vielelezo na ushahidi wa kuharibika kwa uchaguzi huo.
Aidha, alisema msimamo wa Baraza Kuu la CUF ndiyo muongozo wa chama kuwa Tume ya Uchaguzi wa Zanzibar warudi kazini wakamilishe ujumlishaji wa matokeo ya uchaguzi wa awali na kumtangaza mshindi wa uchaguzi huo.
Alisema kuwa hali ya kisiasa ya Zanzibar ipo katika giza kutokana na wananchi kushindwa kufahamu lini watapata viongozi wa kidemokrasia huku wakiendelea kushuhudia kupanda kwa gharama za maisha Visiwani humo.
Hata hivyo alisema kuwa mazungumzo hayo yamesaidia kwa kiasi kikubwa kutuliza hali ya amani na kuondoa hofu wananchi lakini alitaka yakamilike kwa wakati ili wananchi wajue hatia yao ya kupata viongozi.
Aidha alisema kuwa CUF inatambua kuwepo kwa watu wanaotaka kupindisha uchaguzi uliyofanyika Oktoba 25 mwaka huu lakini alisema hawatafanikiwa kutokana na ripoti za waangalizi wa ndani na nje kuweka wazi kuwa uchaguzi ulikuwa huru na wa haki Zanzibar.
“Wakati Mwenyekjiti wa ZEC anatangaza kufuta matokeo tayari matokeo katika Majimbo 54 yalikuwa yamekamilika na kubandikwa matokeo na Wagombea kupewa vyeti vyao vya ushindi hoja ya kufuta matokeo Mwenyekiti katoa wapi?” Aliuliza.
“Haiwezekani kufanyika uchaguzi wa marejeo kabla ya uchaguzi wa mwanzo kukamilika Zanzibar, sawa na kusherekea harusi kabla ya ndoa kufanyika.”
Alisema wakati Mwenyekiti Jecha anafuta matokeo hayo katika meza yake majimbo tisa yalikuwa yanamsubili kutangaza matokeo baada ya uhakiki kukamilika na kubakia Majimbo 14 ya Wilaya tatu za Kisiwani Pemba.
Aidha alisema kuwa Mwenyekiti wa Tume hiyo alivunja kanuni na sheria kutokana na kitendo cha ZEC kuhakiki matokeo ya Urais mara mbili wakati tayari kazi kama hiyo ilikuwa imefanyika katika Majimbo na kumalizika na kumalizika salama kabla ya kufutwa kwa matokeo hayo.
“Mwenyekiti arudi kazini atangaze marokeo na mshindi wa urais wa Zanzibar uchaguzi wa marudio hatutaki kusikia Zanzibar,” alisema Shehe.
Jecha alisema aliamua kufuta matokeo ya uchaguzi huo baada ya kutawaliwa na vitendo vya udaganyifu ikiwemo idadi ya wapiga kura kuzidi katika baadhi ya vituo kinyume na idadi ya watu waliosajiliwa katika daftari la wapiga kura Visiwani humo.